Habari za Punde

Wanafunzi 15,647 wafeli mitihani

Na Mwanajuma Mmanga
WANAFUNZI 7,503 wa darasa la saba kati ya wanafunzi 10,823 waliofanya mitihani ya majaribio katika baadhi ya skuli za serikali za Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, wamefeli ambao ni sawa na asilimia 69.32.

Aidha wanafunzi 1179 sawa na asilimia 9.82 hawakufanya mitihani hiyo.

Waliofaulu kwa kiwango bora zaidi ni wanafunzi 39 tu sawa na asilimia 0.39, waliofaulu kwa kiwango cha nzuri sana ni 362 sawa na asilimia 3.34 na waliofaulu kwa kiwango cha nzuri ni 1468 sawa na asilimia 13.56 na waliofaulu kwa kiwango cha inaridhisha ni 1451 sawa na asilimia 13.41.

Kwa upande wa wanafunzi wa kidato cha pili, walioshindwa ni wanafunzi 8,144 sawa na asilimia  84.772 kati ya wana 9,607 waliofanya mitihani hiyo.

Waliofaulu kwa kiwango cha bora sana ni mwanafunzi mmoja sawa na asilimia 0.010, kiwango cha nzuri sana ni wanafunzi 144 sawa na asilimia 1.499, waliofaulu kwa kiwango cha nzuri ni 411 sawa na asilimia 4.278 na  waliofaulu kwa kiwango cha inaridhisha ni 906 sawa na asilimia 9.43.

Akitoa tathmini ya ripoti ya matokeo  hayo,Ofisa Elimu Mkoa wa Mjini Magharibi,Khatibu Muhsin, wakati wa hafla ya utoaji wa zawadi kwa wanafunzi bora waliofanya vizuri mitihani hiyo, iliyofanyika skuli ya Skuli Haile Sellasie ikiwa ni sehemu ya sherehe ya kutimiza miaka 50 ya elimu bila malipo, alisema 
matokeo hayo hayaridhishi.

Akizungumzia changamoto walizokabiliana nazo wakati wa ufanyaji wa mitihani hiyo, alisema ni pamoja na  mwamko mdogo kwa baadhi wazazi katika uchangiaji wa fedha kwa ajili ya mitihani hiyo.

Pia alisema kuwepo kwa utoro wa wanafunzi na ukosefu wa nyenzo za uchapishaji mitihani, ilisababisha zoezi hilo kuwa gumu.
Alisema inaonekana wanafunzi wanaofanya vizuri mitihani ya majaribio ndio wanaofaulu mitihani ya taifa.


Alizitaja skuli zilizoshiriki katika mitihani hiyo kuwa ni  Kibweni, Wazazi Amani, Mkunazini, Chumbuni Msingi, Kijichi, Mwenge, Mwanakwerekwe D na B, Kisiwandui na Kilimahewa.

Kwa upande wa kidato cha pili ni Lumumba, Kiembesamaki,Vikokotoni, Benbella, Kiponda, Tumekuja, Skuli ya Biashara Mombasa, Mikunguni, Mikindani Dole na Mwanakwerekwe C.

Skuli bora za msingi zilizofanya vizuri ni Wazazi, Mkunazini na kibweni na skuli za sekondari ni Vikokotoni, Kiembesamaki  na 
Lumumba.

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi, Abdalla Mwinyi Khamis, aliwashauri walimu wakuu kufanya mitihani kwa utaratibu unaoeleweka na kuepuka utitiri wa mitihani.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.