Na Mwandishi wetu, Beijing
Tanzania na China, zimetiliana
saini mkataba wa maelewano (MoU) ambapo taasisi za China zitawekeza mabilioni
ya dola za Marekani katika uchumi wa Tanzania.
Shughuli ya utiaji saini
imekuwa sehemu ya mkutano wa tatu wa uwekezaji kati ya Tanzania na China
uliofanyika ukumbi wa mikutano wa nyumba ya wageni ya serikali ya Diaoyutai
mjini Beijing, China.
Aidha, utiaji saini huo ambao
utaziwezesha taasisi kadhaa za Tanzania kunufaika na mitaji na uwekezaji kutoka
China ulikuwa sehemu ya ziara rasmi ya kiserikali ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania,Mhe. Jakaya Kikwete China kwa mwaliko wa Rais Xi Jinping.
Miongoni mwa makubaliano
yaliyotiwa saini ni pamoja na ushirikiano wa kimkakati kati ya Shirika la
Nyumba Tanzania (NHC) na kampuni ya China Railway Jianchang Engineering (CRJE)
ambako kiasi cha dola bilioni moja unusu zitawekezwa katika uchumi wa Tanzania.
Kiasi cha dola bilioni moja
zitawekezwa katika ujenzi wa mji mpya wa Salama Creek Satellite, eneo la
Uvumba, wilaya ya Temeke, Dar es Salaam na kiasi cha dola milioni 500
zitawekezwa katika ujenzi wa Financial Square, eneo la Upanga.
Aidha, NHC itapata kiasi cha
dola za Marekani milioni 200 kutoka kampuni ya Poly Technologies kwa ajili ya
ujenzi wa mradi wa Valhalla, eneo la Masaki, Dar es Salaam.
Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) pia limetiliana saini makubaliano na kampuni ya Hengyang Transformer
ambapo kampuni hiyo itapata mamilioni ya dola za Marekani kwa ajili ya mradi wa
kusambaza umeme vijijini.
Aidha, TANESCO limetiliana
saini makubaliano ya ujenzi wa mradi wa umeme wa Kinyerezi IV.
Halmashauri ya manispaaa ya
Temeke, Dar es Salaam imetiliana saini makubaliano na kampuni ya Jiangyin
Tianhe Gasses Group ya ujenzi wa barabara ya lami ya Kikwete Friendship Highway
katika wilaya ya Temeke.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Saidi Mecky Sadiq na Mkuu wa wilaya ya Temeke, Sofia Mjema, walishuhudia utiaji
saini makubaliano hayo.
Vile vile, mkoa wa Pwani,
umetiliana saini makubaliano na kampuni ya Jiansu Shenli Plastics Group Limited
ya China kwa ajili ya kugharamia na kuendeleza mradi wa viwanda na uchumi
katika eneo la Mlandizi.
Mkuu wa mkoa wa Pwani, Mwantumu
Bakari Mahiza, alitia saini kwa niaba ya mkoa wake.
Wakati huo huo Rais Kikwete,
alisema maendeleo ya haraka ya China ni hamasa kubwa na ya kutosha kwa nchi za
Afrika kuwa nazo zinaweza kuendelea katika kipindi kifupi kama zitaongozwa na
sera sahihi za mageuzi ya kiuchumi.
Rais Kikwete aliyasema hayo
jana wakati alipokutana kwa mazungumzo rasmi na Mwenyekiti (Spika) wa Bunge la
China, Zhang Dejiang, ikiwa ni moja ya shughuli za Rais katika ziara yake rasmi
ya China.
Katika mazungumzo hayo kwenye jengo
la Bunge la Great Hall of the People mjini Beijing, Rais Kikwete alimwambia
Dejiang: “China inatuhamasisha kwamba na sisi tunaweza kupata mabadiliko na
maendeleo ya haraka ya wananchi wetu ili mradi tu tuweze kuwa na sera sahihi
ambazo zinalenga katika kuleta mageuzi ya msingi na ya kweli kweli ya
kiuchumi”.
Alisema kwake yeye ambaye
amekuwa anatembelea China kila baada ya wastani wa miaka minne, mabadiliko ya
China yanatia hamasa kweli kuwa nchi za Afrika pia zinaweza kuleta mageuzi
makubwa ya maisha ya watu wake.
“Nilikuja hapa kwa mara ya
kwanza mwaka 1980, na tokea wakati huo nimetembelea nchi hii kila baada ya
miaka minne kwa wastani na kila nikija nashuhudia mabadiliko makubwa
yasiyopimika na wala kufikirika. China ilikuwa nchi masikini sana wakati
nilipofika hapa kwa mara ya kwanza lakini katika miaka 30 tu imebadilika kutoka
nchi masikini na kuwa nchi iliyoendelea na yenye uchumi unaoshikilia nafasi ya
pili kwa ukubwa duniani,” alisema.
“Tunawapongeza kwa juhudi
ambazo zimewafikisheni hapa. Mnatuhamasisha na sisi kuwa ipo siku moja na sisi
katika Afrika tutafikia hatua hii ya maendeleo,” alisema.
Naye Dejiang alimkubusha Rais
Kikwete mazungumzo kati yao wakati walipokutana kwa mara ya kwanza miaka saba
iliyopita Ikulu, mjini Dar es Salaam.
Wakati huo, Dejiang alikuwa
Katibu wa Chama Tawala cha Kikomunisti cha China katika jimbo la Guangzhou,
jimbo ambalo linaongoza katika China kwa kufanya biashara na Tanzania.
Kati ya biashara zote ambazo
Tanzania na China zinafanya, asilimia 60 inatokea jimbo la Guangzhou.
Alipongeza uhusiano mzuri kati
ya Tanzania na China katika miaka 50 tokea nchi hizo mbili kuanzisha uhusiano
wa kibalozi Aprili 26, mwaka 1964.
Pia alisema ujenzi wa Reli ya
TAZARA unaendelea kuthibitisha urafiki baina ya watu wa China, Tanzania na
Zambia na kuongeza kwa Tanzania kwa kuimarisha TAZARA na kwa kutilia maanani
utajiri na raslimali zilizopo, ikiwemo nafasi ya kijiografia, utulivu na amani
na idadi kubwa ya watu, Tanzania ina sifa ya kuwa nchi tajiri katika miaka
isiyokuwa mingi ijayo.
No comments:
Post a Comment