Na Anita Jonas, Maelezo
Umoja wa Mataifa umeshauriwa kuchukua
hatua za haraka kwa maradhi ya mripuko yanayotokea Afrika kama Ebola
kwani yanaathiri uchumi wa mataifa yanayohusika.
Ushauri huo ulitolewa na Waziri
wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, wakati wa maadhimisho
ya miaka 69 ya Umoja wa Mataifa jana Jijini Dar es Salaam.
Alisema umoja huo unatakiwa kuchukua
tahadhari ya miripuko ya maradhi hatarishi na kuyachukulia kama ni maradhi ya kidunia
badala ya kuyaona ni ya Waafrika.
“Kama mataifa yaliyoendelea
yasingepuuza mripuko wa ugonjwa wa Ebola
ulipojitokeza Afrika hali
isingekuwa mbaya kiasi hiki, hivyo
rai yangu kwa Umoja wa Mataifa kwa
kushirikiana na mataifa yanayohusika kuchukua
tahadhari wakati wote,” alisema.
Aidha alisema kutokana na
mabadiliko ya tabianchi, washirika wa maendeleo hawana budi kusaidia mataifa
mengine ikiwemo utekelezaji wa mfuko wa kijani wa hali ya hewa.
Akizungumzia hatua ya Rais
Kikwete kutoa uraia kwa wakimbizi 162,000 wa Burundi, alisema Tanzania
imeonesha ulimwengu kuwa suala la mapambano dhidi ya ukimbizi linaweza
kufanyiwa kazi na kuwafanya wakimbizi kuishi maisha kama binadamu wengine.
Naye Mwakilishi wa makazi wa
Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alvaro Rodriguez, alisema
shirika hilo kwa kushirikiana na serikali na wadau wengine, limepanga kusaidia na kuimarisha miundombinu
ya kiusalama ili kuendeleza amani duniani kwani bila amani maendeleo ni vigumu
kupatikana.
Aliipongeza Tanzania katika
kutekeleza malengo ya millenia katika sekta ya afya ambapo asilimia 96 ya vituo
vyote vya afya nchini vinatoa huduma ya afya ya uzazi kwa mama na mtoto.
Sherehe hizo zimebebwa na kauli
mbiu ya ‘Leave no One Behind’ (asiachwe mtu nyuma) ’ ikiwa na lengo la kuleta maendeleo yenye usawa
duniani.
No comments:
Post a Comment