HOTUBA YA RAIS WA
ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA
MAPINDUZI,
MHESHIMIWA AL-HAJ DK ALI MOHAMED SHEIN,
KATIKA BARAZA LA IDD
EL HAJJ, OKTOBA, 2014
(Mwezi 10 Mfunguo Tatu: 1435)
Bismillahi Rahmani
Rahim,
Shukurani zote anastahiki Mwenyezi Mungu
Mtukufu; Mola wa viumbe wote. Mwenyezi
Mungu ndiye anayestahiki kukusudiwa na viumbe wote kwa kumuabudu, kumuomba
msamaha na kumtegemea.
Sala na salam zimshukie Mtukufu wa daraja,
Mtume wetu na kigezo chetu; Nabii wa Mwenyezi Mungu, Sayyidna Muhammad (S.A.W)
pamoja na wafuasi wake wote hadi kitakaposimama kiama. Mwenyezi Mungu atujaalie na sisi tuwe
miongoni mwa wenye kufuata mwenendo wao na kupata malipo mema hapa duniani na
huko akhera twendako. AMIN!
Ndugu Wananchi,
Mheshimiwa Sheikh
Khamis Haji Khamis;
Kadhi Mkuu wa
Zanzibar,
Mheshimiwa Maalim
Seif Sharif Hamad;
Makamu wa Kwanza wa
Rais,
Mheshimiwa Balozi
Seif Ali Iddi;
Makamu wa Pili wa
Rais,
Mheshimiwa Pandu
Ameir Kificho;
Spika wa Baraza la
Wawakilishi,
Mheshimiwa Omar
Othman Makungu;
Jaji Mkuu wa
Zanzibar,
Waheshimiwa
Mawaziri,
Waheshimiwa
Mabalozi,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,
Assalamu Aleikum
Warahmatullah Wabarakatuh
IDD MUBARAK
Nimeanza kwa kushuhudia kuwa hapana Mola
anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah (SW) na kumsalia mbora wa waja;
Mtume wetu Seyyidna Muhammad (S.A.W) pamoja na wafuasi wake. Hapana shaka ni uwezo wake Subhana Wataala kutujaalia neema ya uhai tukaweza
kuidiriki siku hii na kuiadhimisha kwa Takbira nyingi.
Kwa mapenzi yake Mola wetu kwetu, tumeweza
kuungana na Waislamu wenzetu walioko katika Mji Mtukufu wa Makka wanaoendelea
kutekeleza Ibada ya Hija ambayo ni nguzo ya tano ya Uislamu. Waislamu wa Zanzibar na Tanzania nzima kwa
jumla tunaungana na wenzetu duniani kote kumuomba Mwenyezi Mungu awatakabalie
ibada zao zote, awawezeshe kuzingatia mafunzo ya Hija na kuyaendeleza na
awarudishe nyumbani salama ili waweze kuungana tena na familia, jamaa, marafiki
na wananchi wenzao.
Ndugu
Wananchi,
Mwenyezi Mungu ametujaalia Waislamu sikukuu
mbili kubwa kila mwaka; Sikukuu ya Idd
el Fitri na Sikukuu ya Idd el Hajj, tunayoisherehekea leo. Miezi miwili iliyopita na siku kidogo,
tulisherehekea Sikukuu ya Idd el Fitri baada ya kuikamilisha ibada ya swaumu
katika mwezi Mtukufu wa Ramadhan na leo tena tupo hapa Micheweni katika Chuo
cha Kiislamu hapa Kiuyu kwa ajili ya Sikukuu ya Idd Al- Adhha, ambayo
tunasali Idd na kuchinja kama
ilivyoagizwa katika Suratul Kawthar, aya
ya kwanza na ya pili zenye tafsiri
isemayo:
“Hakika tumekupa kheri nyingi”.
“Basi sali kwa ajili ya Mola wako na
uchinje”.
Mbali na wajibu wetu wa kumshukuru Mwenyezi
Mungu kwa kutuwezesha kuzifikia sikukuu hizi tukiwa hai, vile vile, tuna wajibu
wa kuzingatia mafunzo yanayotokana na ibada hizi na kuyaendeleza katika maisha
yetu ya kila siku hapa duniani.
Ndugu
Wananchi,
Ibada ya Hija imekusanya mambo mengi
yanayomkurubisha mja kwa Mola wake. Hija
ni mithili ya taasisi ya mafunzo ya malezi na maarifa kwa Waislamu katika
misingi ya tawhidi kwa kumtukuza Mwenyezi Mungu na huanza kwa kuweka nia safi
na ikhlasi. Mafunzo haya yana mchango
muhimu kwa mja kuwa mcha Mungu kwa kujiepusha na vitendo vyote vitakavyomtoa
katika njia ya Mwenyezi Mungu na mafunzo ya Bwana Mtume Muhammad (SAW)
aliyeletwa kwetu kutupa miongozo.
Mwenyezi Mungu anatukumbusha kwenye Kurani
katika sehemu ya aya ya 7 ya Suratul Hashir yenye tafsiri isemayo:
“…… Na anachokupeni Mtume basi pokeeni,
na anachokukatazeni jiepusheni nacho. Na
muogopeni Mwenyezi Mungu; kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu“.
Kwa mnasaba wa aya hii, Mwenyezi Mungu
anatuasa kuzingatia mafunzo ya Bwana Mtume kwa kufanya yote tuliyoamrishwa na
Mwenyezi Mungu (SW), likiwemo hili la kutekeleza ibada ya Hija na kuzingatia
mafunzo yake na kutubainishia ubaya wa kushindwa kuitekeleza kwa wale
waliojaaliwa kuwa na uwezo. Mtakumbuka katika hotuba yangu ya Idd el Fitri
nilieleza kuwa mafunzo ya Saumu ya Ramadhani ni mfano wa mafunzo ya Chuo Kikuu.
Mafunzo yanayohusiana na utekelezaji wa Ibada ya Hija nayo ni
mafunzo ya daraja la juu. Mwenye kufuzu na kupata hio daraja ya juu, kwa
hakika hupata fadhila kubwa kwa Mwenyezi Mungu, hadhi na heshima hata ya
kumtambua kuwa Al-Hajj kwa mwanamme na Hajjat kwa mwanamke.
Kwa hivyo, tunapaswa kuwapongeza Waislamu
wenzetu waliofanikiwa kwenda kuitekeleza ibada ya Hija na tuwape heshima
wanayostahiki. Pamoja na hayo, tuzidi
kuwaombea hija zao zikubaliwe. Wale watakaofuzu huwa wamefutiwa madhambi yao
yote, kama inavyosema hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Sayyidna Abu Huraira
(RA), Bwana Mtume (S.A.W) amesema:
“Mwenye
kufanya Hijja bila ya kusema maneno
machafu na bila ya kufanya vitendo vichafu, atasamehewa madhambi yake arudi
kama siku aliyozaliwa na mama yake”
Tumuombe Mola wetu (SW) azikubali ibada za
Waislamu wenzetu wote waliokwenda kuitikia wito Wake wa kwenda kufanya ibada
hiyo.
Ndugu
Wananchi,
Jambo jengine muhimu tunalojifunza katika
Ibada ya Hija ni kubainisha hisia za Umoja wa Kiislamu na usawa wa wanaadamu
mbele ya Mwenyezi Mungu. Waislamu kutoka
mataifa mbali mbali, wenye nyadhifa, uwezo na rangi mbali mbali hukusanyika
pamoja katika mji mtukufu wa Makka na Madina, wakiwa na lengo moja la kuitikia
wito wa Mwenyezi Mungu wa kufanya ibada katika nyumba tukufu ili kupata
uongofu. Katika Surat Al- Imran aya ya
96 Mwenyezi Mungu amesema,
“Kwa
yakini Nyumba ya kwanza iliyowekwa kwa ajili ya watu (kufanya ibada) ni ile
iliyoko Makka, yenye baraka na yenye uwongofu kwa ajili ya walimwengu wote”.
Na katika aya ya 97 ya Sura hiyo Mwenyezi
Mungu ameendelea kusema:
“Humo
mna ishara zilizo wazi (za kuonesha utukufu wake na ukongwe wake. Miongoni mwa hizo ni) mahali alipokuwa
akisimama Ibrahimu, na anayeingia (nchi hiyo) anakuwa katika salama. Na Mwenyezi Mungu amewawajibishia watu
wafanye Hija katika Nyumba hiyo, yule awezaye kufunga safari kwenda huko .……”.
Ni faraja iliyoje kwa Muislamu kupata wasaa
katika uhai wake kujumuika katika mkusanyiko mkubwa wa Umoja wa Waislamu wa
kila mwaka katika nyumba tukufu. Katika mazingira haya mahujaji hupata fursa ya
kujadiliana masuala mbali mbali ya kuuendeleza Uislamu na kuzifanyia kazi
changamoto zinazowakabili katika ulimwengu wa leo. Kadhalika, mkusanyiko huu ni
kielelezo cha umoja, udugu na mshikamano wa Waislamu kwamba wanafuata miongozo
ya Kurani Tukufu na Hadithi za Bwana Mtume Muhammad (S.A.W).
Ndugu
Wananchi,
Hapana shaka kwamba maarifa mapya
wanayoyapata mahujaji wetu wanapofanya ibada ya Hija, yatakuwa na manufaa zaidi
iwapo watakuja kuyaendeleza watakaporudi hapa nyumbani. Ni dhahiri kuwa nchi yetu inahitaji sana
kuzidi kuendelezwa kwa hali ya umoja na mshikamano wetu kwani ndio siri kubwa
ya mafanikio tuliyoyapata katika kuimarisha amani tuliyonayo, ustawi wa uchumi
na kukuza maendeleo ya jamii.
Kwa hivyo, kwa kuwa hali hiyo ya umoja na
mshikamano, mtu anaweza kuihisi katika wiki chache tu za kukutana na watu
kutoka nchi mbali mbali kwa mamilioni wakati wa Hija, ni vyema akaiendeleza
wakati anaporudi hapa nyumbani tunapoishi siku zote. Hiyo itakuwa ndiyo namna
bora ya kuyatumia mafunzo hayo yanayotakiwa yadumu katika maisha yetu ya kila
siku na ndio kielelezo bora cha mtu aliyekwishahiji.
Ndugu
Wananchi,
Vile vile, mahujaji wetu hunufaika katika
kuziimarisha imani zao kutokana na kuyatembelea maeneo mashuhuri ya historia ya
Uislamu, wakiwa na amani ya nafsi na ya kimazingira wakati wote. Katika kipindi chote cha Hija ndugu zetu hawa
huwa ni wageni wa Mwenyezi Mungu Mkarimu.
Katika hadithi iliyopokelewa na Sayyidna Anas bin Malik (RA), Bwana
Mtume (S.A.W) amesema:
“Mwenye
kufanya Hija na mwenye kufanya Umra ni wageni wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hupewa wanachoomba, na (Allah) anajibu dua
zao, na hurudishiwa walivyotoa, dirham (au shilingi) moja kwa dirham (au
shilingi) milioni moja” (Al baihaqiy).
Katika hadithi nyengine iliyopokelewa na
yeye Sayyidna Anas bin Malik (RA) vile vile Bwana Mtume (S.A.W) amesema:
Kutoa
kwa ajili ya Hijja ni sawa sawa na kutoa kwa ajili ya jihad; dirham moja kwa
mia saba” (Tabrany)
Riwaya hii imetafsiriwa na baadhi ya Maimamu
kuwa inamaanisha kwamba hata wale wasiokwenda Hija, lakini kwa namna mbali
mbali hushiriki katika kuwaandalia safari Mahujaji wetu, vile vile nao Mwenyezi
Mungu huwalipa malipo makubwa. Napenda
kutoa shukurani zangu kwa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana, kwa kushirikiana
vyema na taasisi zote zilizohusika katika kuwasafirisha Mahujaji wetu kwa
kuwahudumia vyema tangu mwanzo hadi sasa na Inshaallah mpaka hapo watakaporudi
hapa nyumbani. Tumuombe Mwenyezi Mungu sote atupe ilham, afya na uwezo wa
kupata kuitekeleza nguzo hii ya tano ya Kiislamu na kuwasaidia kwa kila namna wenzetu
waliojaaliwa uwezo wa kwenda kuhiji ili sote tuweze kunufaika na fadhila zake.
Ndugu
Wananchi,
Napenda kutumia fursa hii kusisitiza umuhimu
wa kuyaendeleza mafunzo yanayotokana na ibada zetu mbali mbali katika maisha
yetu ya kawaida, hasa suala la kuhimizana kufanya mambo mema na kukatazana
mambo mabaya. Kufanya hivyo ni kuitii
amri ya Mola wetu Mtukufu, kutekeleza mafundisho wa Bwana Mtume (S.A.W) pamoja
na jamii inayozingatia misingi ya sheria na utawala bora.
Mwenyezi Mungu huongeza baraka na neema
katika jamii ambayo huzishukuru neema zake kwa kuzitumia katika njia inayolenga
kunufaisha watu walio wengi.
Kwa kutumia uwezo wa rasilimali ambazo
Mwenyezi Mungu ametujaaliya nchini, Serikali inaendelea na jitihada zake kwa
kushirikiana na washirika wetu wa maendeleo mbali mbali katika kuimarisha
miundombinu ikiwemo barabara, usambazaji wa maji safi na salama, huduma za
umeme na mengineyo.
Katika Mkoa huu wa Kaskazini Pemba, wenyeji
wa Mkoa huu na hata baadhi ya wageni ni mashahidi wa kubainisha jitihada hizo
ambazo naamini matunda yake yanafurahiwa na watu wengi kwani mambo haya ya
maendeleo yaliofanywa ni ukombozi mkubwa wa hali ya maisha ya wananchi.
Serikali kwa kushirikiana na washirika wetu
wa maendeleo imefanya juhudi kubwa ya kuimarisha miundombinu ya barabara katika
Mkoa huu. Ni dhahiri kuwa, kuimarika kwa
miundombinu ya barabara kutasaidia sana katika kuimarisha sekta nyingine za
kiuchumi.
Kwa kipindi kirefu miundombinu ya barabara
ilikuwa ni changamoto kubwa kwa wananchi kwa ajili ya kuendesha maisha yao na
kwa wawekezeji wengi waliokuwa na azma ya kuwekeza katika katika sehemu mbali mbali
nchini. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilitangaza maeneo huru ya uchumi
katika mwaka 1992, ambapo ilitenga eneo la Fumba kwa upande wa Unguja na eneo
la Micheweni kwa upande wa Pemba; kwa
ajili ya kazi hiyo. Ukosefu wa miundombinu ya barabara za kisasa kwa kipindi
kirefu ulikwamisha jitihada zetu za kupata wawekezaji wenye viwango tunavyotaka
katika maeneo huru yaliyotengwa hapa Micheweni na Mkoa wa Kaskazini, Pemba kwa
jumla. Ni dhahiri kuwa, hatua tuliyofikia hivi sasa ya kuimarisha miundombinu,
itasaidia sana katika juhudi zetu za kutafuta wewekezaji tunaowataka.
Ndugu
Wananchi,
Kwa bahati mbaya, wapo baadhi ya wananchi
wachache ambao wanaendelea kuweka mbele maslahi yao kwa kuharibu maslahi ya wengi. Katika maeneo
mengi ya Unguja na Pemba kumekuwa na uharibifu wa makusudi wa miundombinu mbali
mbali, licha ya Serikali kutumia fedha nyingi katika kuiimarisha. Wapo baadhi
ya watu wanaong’oa nguzo na mabati ya alama za barabarani. Kwa upande wa
miundombinu ya umeme, wako wanaokata nyaya za transforma. Kesi za uharibifu wa
transforma ni nyingi ikiwemo iliyotokezea mwezi Agosti, mwaka huu katika eneo
la Mwembe Shauri, Unguja na kesi nyengine kwenye visima vya maji. Kadhalika, funiko za chuma za makaro kwenye
maeneo ya miji zinachukuliwa na kuuzwa kama vyuma chakavu. Mambo haya hayatoi taswira nzuri katika
jamii yetu. Kwa hivyo, sote tunapaswa
tushirikiane ili tuweze kuvizuwia vitendo hivi kwani, vina athari kubwa kwa ustawi wa
maendeleo yetu.
Ndugu
Wananchi,
Wakati huu tunaposherehekea sikukuu hii ya
Idd el Hajj tunaendelea na msimu wa mavuno ya karafuu katika mwaka 2014/2015
tuliouanza mwezi Julai, 2014. Hatuna budi tumshukuru Mwenyezi Mungu (SW) kwa
kutujaalia neema hii kubwa. Kadhalika, napenda
kutoa shukurani za dhati kwa wakulima wote wa karafuu nchini kwa kuendelea
kuziuza karafuu zao katika vituo vya Shirika letu la ZSTC. Nimearifiwa kuwa hadi kufikia tarehe 2 Oktoba
2014 tani 1,347.65 za karafuu zenye thamani ya Tsh.Milioni 18,862.7 zimeshanunuliwa katika vituo vyetu vya ZSTC
Unguja na Pemba. Haya ni mafanikio ya
kutia moyo.
Serikali imejiandaa vyema kuhakikisha kuwa
karafuu zote zinanunuliwa pamoja na kuhakikisha kwamba wakulima wa karafuu
wanapata vifaa vyote wanavyohitaji katika shughuli zao. Aidha, kwa kushirikiana na vikosi vyetu vya
ulinzi na usalama tutaendelea kupambana na magendo ya karafuu, ili faida
inayopatikana kutokana na zao hili iendelee kuwanufaisha wakulima wetu na
kukuza uchumi wa nchi yetu.
Kwa kuzingatia hali halisi ya bei ya karafuu
katika soko la dunia, Serikali haikuweza kupandisha bei ya karafuu kwa msimu
huu wa mwaka 2014, lakini imefanya kila jitihada kuhakikisha kuwa bei inabakia
kama ilivyokuwa katika msimu uliotangulia wa mwaka 2013/2014 ili kuwapa nguvu
wakulima. Siku ya tarehe 9 Julai, 2014
nilipozindua rasmi Msimu wa Karafuu wa mwaka 2014/2015 Serikali ilitangaza bei
mpya ya karafuu kuwa kilo moja ya karafuu ya gredi ya kwanza kuwa ni TShs.
14,000 na gredi ya pili kuwa TShs. 12,000 na TShs. 10,000 kwa gredi ya
tatu. Nimearifiwa kwamba kumekuwa na
mwamko mkubwa kwa wakulima katika kuutunza na kuimarisha ubora wa karafuu zetu,
jambo hili limewawezesha wakulima kupata gredi ya kwanza kwa karafuu nyingi
wanazoziuza na kuinua kipato chao.
Nawapongeza wakulima kwa kuwa na mwamko huu.
Kadhalika, nachukua fursa hii kwa mara
nyengine, kuwataka wale wenye tabia ya kuanika karafuu kwenye barabara au
kutumia njia mbaya za uanikaji na ukaushaji wa karafuu kuacha tabia hiyo, kwa
kuwa ina athari kubwa katika kupata bei bora ya karafuu zetu katika soko la
dunia ambalo hivi sasa limejaa ushindani mkubwa.
Katika jitihada za kulinda hadhi na sifa
pekee za karafuu zetu, Serikali inakamilisha utekelezaji wa mpango wa kuzipa
karafuu za Zanzibar utambulisho maalum (Branding).
Vile vile, Serikali inaendelea kutekeleza
ahadi ya kuimarisha miundombinu ya barabara katika maeneo ambayo wakulima
wanapata usumbufu kuyafikia mashamba yao ya mikarafuu. Serikali tayari imeshatekeleza ahadi ya ujenzi
wa barabara ya Kuyuni – Ngomeni kwa kiwango cha kifusi yenye urefu wa kilomita
3.1. Ujenzi wa barabara hii umegharamiwa
na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mfuko wa Barabara. Hivi sasa tunakamilisha mipango ya kuanza
ujenzi wa barabara ya Kipapo-Mgelema pamoja na barabara ya Mgagadu – Kwa
Utao. Lengo la Serikali ni kuzijenga
barabara hizi kwa kiwango cha lami hapo baadae tutakapopata uwezo. Kumalizika
kwa barabara hizo kutarahisisha vile vile utekelezaji wa shughuli nyengine za
maendeleo kwa wananchi wa maeneo hayo.
Jitihada za Serikali za kurudisha hadhi ya
zao la karafuu zimesaidia sana katika kuinua hali za maisha ya wakulima katika
sehemu mbali mbali hasa hapa Pemba. Zao la karafuu limechangia sana kuimarisha
mzunguko wa fedha ambao umekuwa ukisaidia sana
kuimarisha biashara na shughuli
mbali mbali za kiuchumi.
Kwa mara nyengine tena, napenda kuwanasihi
wakulima wetu wa karafuu waendelee na jitihada zao za kutumia huduma za benki
kwa kuhifadhia fedha zao na kujiwekea akiba.
Uamuzi wao huo ni uamuzi wa kimaendeleo.
Wale ambao bado hawajachukua hatua, ni busara wakafanya uamuzi huo hivi
sasa.
Ndugu
Wananchi,
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema ya
mvua ambayo tumeanza kuipata katika maeneo mbali mbali nchini. Ni vyema tukaitumia neema hii anayoendelea
kuturuzuku Mola wetu katika kuimarisha shughuli zetu za kilimo. Tuzitumie mvua hizi kwa kupanda kwa wingi
miti ya matunda, mboga mboga, mimea ya vyakula vya mizizi na miti ya misitu na
biashara.
Aidha, tuutumie wakati huu kwa kuendeleza
kilimo cha mikarafuu kwa kuyashughulikia ipasavyo mashamba yetu. Nimeelezwa
kuwa idadi ya miche ya mikarafuu 686,854 itatolewa kwa wakulima katika msimu wa
mvua za Masika wa mwaka 2014/2015,
ambapo miche 499,354 iliyoatikwa kwenye vitalu vya Serikali na miche
187,500 iliyoatikwa kwenye vitalu vya watu binafsi. Natoa wito kwa wakulima wayatayarishe vyema
mashamba yao kwa mujibu wa maelekezo ya wataalamu wa kilimo na misitu, ili
juhudi zetu ziweze kuwa na tija zaidi. Tusiusahau msemo mashuhuri wa walimu
wetu kwamba “Jitihada ndiyo ufunguo wa
mafanikio”. Kwa hivyo, tuzitumie fursa zote zilizopo ili kuliendeleza zao
la karafuu ambalo ni tegemeo kubwa kwa uchumi wetu.
Ndugu
Wananchi,
Sote tunafahamu kwamba Hija ya mwaka huu
kama zilivyokuwa Hija za miaka iliyopita, imekuja wakati dunia yetu ikiendelea
kukumbwa na matatizo mbali mbali.
Matatizo hayo yanatokana na sababu mbali mbali za uwezo wa Mwenyezi
Mungu na zikiwemo zinazosababishwa na binadamu.
Matukio ya vimbunga, matetemeko ya ardhi, kuripuka kwa volcano,
mabadiliko ya tabianchi, na kadhalika, yameleta athari kubwa pamoja na kupoteza
maisha ya watu mbali mbali na mali zao. Aidha,
yapo maafa mengine ya maradhi thakili yanayoendelea kuikumba dunia yakiwemo
maradhi ya UKIMWI, Ebola na mengineyo.
Nchi yetu inaendelea kukumbwa na maafa
kadhaa zikiwemo ajali mbali mbali, hasa za barabarani, athari ya mabadiliko ya
tabianchi, kama vile maeneo ya kilimo kuvamiwa na maji ya bahari na visima vya
asili vimeingia maji ya chumvi. Jumla ya
maeneo 145 yameathirika kwa kuingia maji ya chumvi. Kati ya maeneo hayo, maeneo 123 yapo hapa
Pemba.
Tatizo jengine ni kupanda kwa kina cha maji
ya bahari duniani kwa maeneo yaliyo chini ya mita tano kutoka usawa wa bahari. Maeneo
hayo yapo kwenye hatari ya kuathirika zaidi kutokana na hali hiyo. Kwa upande wa Pemba maeneo ya aina hii yana ukubwa
wa mita za mraba 286 na yanakaliwa na asilimia 54 ya watu na kwa Unguja yana
ukubwa wa mita za mraba 328 na yanakaliwa na asilimia 29 ya watu. Kadhalika, tunashuhudia namna misimu ya mvua
inavyobadilika. Baadhi ya wakati mvua
zinachelewa kunyesha na zinapokuja kiwango chake hupungua au hunyesha kwa
kiwango kikubwa sana. Upepo unaovuma nao
hautabiriki. Pepo za Kusi na Kaskazi,
nazo huvuma tafauti na viwango vilivyozoweleka miaka ya nyuma.
Matatizo ya uchafuzi wa mazingira mengine
tunayasababisha sisi wenyewe. Suala la
utupaji taka ovyo, bidhaa chakavu za kemikali na mifuko ya plastiki pamoja na
uchimbaji wa mchanga na mawe madhara yake ni makubwa na lazima tuhakikishe
kwamba sheria inasimamiwa vizuri. Aidha,
hatuna budi tuendelee kuchukua hatua madhubuti kwa mujibu wa sheria kuzuia
ujenzi kwenye vyanzo vya maji na kwenye mabonde yaliyotengwa kwa shughuli za
kilimo.
Ndugu
Wananchi,
Wapo wananchi, walioathirika na kukabiliwa
na shida na matatizo mbali mbali kutokana na maafa yaliyotokea. Serikali zetu mbili, Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na
Jumuiya za Kimataifa na Washirika wetu wa Maendeleo, zinafanya kila jitihada ya
kutekeleza mipango yetu na ya Kimataifa katika kukabiliana na maafa. Masuala ya mazingira na tabianchi na yale
yote yanayosababisha maafa na majanga katika nchi yetu, yanatekelezwa kwa
kuzingatia sera na mipango iliyokwishaandaliwa.
Hata hivyo, hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa yote hayo ambayo
ni mitihani yake kwetu. Ni wajibu wetu
tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu katika sala zetu ili atulinde na atuepushe na
maafa mbali mbali.
Kadhalika, tunapaswa kumuomba Mwenyezi Mungu
atusamehe makosa yetu mbali mbali, ambayo inawezekana mengine yalisababisha
baadhi ya maafa, kama vile uharibifu wa
mazingira na kadhalika. Tuendelee kumcha
na kumuabudu Mwenyezi Mungu kwa dhati ya imani ya dini yetu kwa kufuata na kuzitekeleza
amri zake na mafundisho ya dini tukiwa waumini wa kweli.
Ndugu
Wananchi,
Pamoja na kwamba sherehe za leo
zinadhihirisha furaha yetu baada ya kukamilika kwa ibada ya Hija, tusisahau
kuwa bado maafa yanaweza kutokea wakati wowote na kuikumba jamii yetu. Hali hio inapotokea, sote tunawajibu wa kutoa
mchango wetu ikiwa ni pamoja na kuomba dua, ili kukabiliana na hali hio. Kwani dua ndio silaha ya Muumini kama
alivyosema Bwana Mtume (SAW).
Kwa hivyo, leo ni fursa nzima ya kujiuliza
na kujikumbusha sababu zinazopelekea jamii yetu kukumbwa na mitihani ya
Mwenyezi Mungu (SW). Tunafahamu kuwa
zipo sababu nyingi zinazofanya mitihani hio itokee na kuikumba jamii yetu.
Imani ya dini inatueleza kwamba binadamu
anapofanya maovu na kusahau mafundisho ya dini, kwa hakika anakosa radhi za
Mola wake. Sote tunashuhudia kwamba
katika jamii yetu siku hizi; vitendo viovu vimekithiri kwa kiasi kikubwa. Baadhi ya vitendo hivyo, ni pamoja na vifo vinavyotokana
na ajali za barabarani, mauaji, ubakaji, udhalilishaji wa wanawake na watoto, ujambazi,
ulevi, rushwa, dhulma, uhasama na chuki zisizokuwa na msingi, na kadhalika. Kwa hivyo, sote tunakabiliwa na jukumu la
kupambana na maovu hayo kwa nguvu zetu zote, ili tuweze kuinusuru jamii yetu na
vitendo vinavyotokea kinyume cha maadili yetu.
Ndugu
Wananchi,
Jukumu kubwa liko kwetu na kwa viongozi wetu mbali mbali; la kutuhimiza
waumini na wananchi, ili tuyawache mambo maovu ambayo ni ya kishetani. Viongozi waendelee daima kukemea maovu katika
jamii na kuwahimiza wananchi kuendelea kupendana na kuwasaidia wale
wanaostahili misaada, hasa mayatima, walemavu, wazee, maskini na wengine wote
wasiojiweza.
Ndugu
Wananchi,
Napenda nisisitize kwa mara nyengine tena
kuhusu suala la kudumisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwetu. Nchi yetu imefikia kuwa nchi ya amani
kutokana na misingi ya uongozi bora iliyowekwa na viongozi wa awamu zote zilizopita
za nchi yetu na uwezo wake Mwenyezi Mungu.
Kila mmoja wetu ana wajibu wa kufurahia baraka alizotupa Mwenyezi Mungu
na kufanya kila jitihada ili tuilinde hali hio ya neema na kheri. Ni lazima tuhakikishe kwamba hapana hata
mmoja atakayekuwa ni chanzo cha kuvurugika kwa amani katika nchi yetu, kwa
visingizio vya harakati za kidini, kisiasa na nyengine zo zote zile. Tuiendeleze sifa ya nchi yetu kuwa ni nchi ya
amani kwa kujiepusha na mifarakano na mizozo isiyokuwa na faida yoyote.
Wito wangu ni kwamba ubinafsi usiingie na
kupewa nafasi katika masuala yanayohusu jamii, hasa mambo ya siasa na
dini. Wale wote wanaofanya hivyo,
watambue kuwa wanafanya makosa kwa kufikiri kwamba wana uwezo zaidi kuliko wengine
wa kuondosha matatizo katika jamii kwa kutumia nguvu zao. Ni vyema tukaelimishana juu ya mema na mabaya
kwa busara, badala ya kiburi na dharau.
Tuendelee kujenga imani yetu na kumuabudu
Mwenyezi Mungu hadi mwisho wa uwezo wetu, bila ya kuchoka au kutosheka; ili
atukubalie sala na dua za kuitakia nchi yetu iendelee kuwa na amani, umoja,
mshikamano na maendeleo.
Tusisahau kamwe kwamba amani na umoja ni
misingi ya uhai wa nchi yetu. Waumini na
wananchi kwa jumla; hatuna budi kuepuka kushabikia mambo yanayokwenda kinyume
na maadili mema. Kwa hivyo, waumini na
wananchi wote ni lazima tufanye bidii ya kuendeleza na kuimarisha amani, kwani
kwa namna hio tutaendelea kujenga mazingira mazuri yanayofaa kwa waumini
kuendelea kufanya ibada na kumcha Mwenyezi Mungu na wananchi sote kujiletea
maendeleo yetu. Kwa hivyo, hakuna
mbadala katika suala la wa amani.
Serikali zetu mbili zitasimamia hali ya amani na utulivu kwa uwezo wetu
wote.
Ndugu
Wananchi,
Sikukuu ni furaha lakini kila sikukuu huwa
na sababu zake kama hii ya leo. Kwa hivyo, tuitumie sikukuu yetu hii kwa
kufanya mambo mema yenye mnasaba wa kuonesha furaha na shukurani zetu kwa
Mwenyezi Mungu (SW) kwa kutujaalia kuifikia siku hii. Miongoni mwa mambo mema
ya kuyatekeleza ni lile la kuchinja mnyama kwa matumizi ya familia zetu na
kuwapa sehemu ya mnyama marafiki zetu, mayatima na wenzetu wengine.
Imepokelewa kutoka kwa Abu Rafii (RA) kwamba
Bwana Mtume (S.A.W) alikua akichinja kondoo wawili; mmoja kwa ajili yake na
familia yake na mwengine kwa ajili ya umma wake. Mambo mengine ya kheri baada
ya kusali sala ya Iddi katika siku hii ni kula na kunywa vitu vizuri vya
halali, kuvaa vizuri kama tunavyoonekana hapa pamoja na kutembeleana, kupeana
zawadi, kuwakagua wagonjwa na kuombeana dua. Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa
wafuasi wazuri wa mafundisho na sunna za Mtume wetu (S.A.W) ili tuweze
kufanikiwa hapa duniani na kesho akhera.
Napenda kuwanasihi wazazi wenzangu tuendelee
kusimamia malezi ya vijana wetu ili nao waige maadili mema na mafundisho ya
dini kwa kuziepuka tabia mbaya zisizoendana
na maamrisho ya Mwenyezi Mungu, utamaduni, silka na malezi ya jamii yetu.
Tuwasimamie mavazi yao ili tuone kuwa wanavaa mavazi ya stara yaliyo muruwa na
wanapokwenda kwenye viwanja vya sikukuu hawajisahau na wanarudi nyumbani mapema
na wanayafikia malengo ya sikukuu zetu.
Ndugu
Wananchi,
Kama kawaida yangu, nataka nizungumzie
umuhimu wa matumizi mazuri ya barabara zetu kwa kuepusha ajali zisizo za lazima
hasa katika nyakati hizi za sikukuu. Sheria
za usalama barabarani zimekuwa zikivunjwa kwa kupakia abiria na watoto zaidi ya
wale wanaokubalika kisheria. Baadhi ya madereva huendesha gari zao kwa mwendo
wa kasi, alama za usalama barabarani wanazipuuza na kusababisha ajali ambazo
zingeweza kuepukwa iwapo wangekuwa waangalifu.
Taarifa kutoka katika Jeshi la Polisi
zinaeleza kuwa kuanzia mwezi wa Januari hadi Agosti mwaka huu wa 2014
kumeripotiwa ajali za barabarani 314 zilizohusisha magari na kusababisha vifo
vya watu 53 na majeruhi 377. Matukio yaliyohusisha waendesha vyombo vya moto
vya maringi mawili katika kipindi hicho ni 112 na kusababisha vifo vya watu 25
na majeruhi 161.
Katika hali kama hii, lazima Jeshi la Polisi
liweke mikakati ya kukabiliana nayo na kushirikiana na taasisi zinazowasimamia
madereva na ukaguzi wa vyombo vyao ili kuhakikisha kuwa madereva wanaokiuka
sheria na vyombo vya usafiri wa barabarani ambavyo ni vibovu, na haviwi vyanzo
vya ajali za barabarani. Wananchi wengi wananung’unika juu ya mwenendo mbaya wa
madereva wa magari makubwa yanayobeba mchanga kwa kukosa hadhari barabarani,
Unguja na Pemba. Naziagiza taasisi zote zinazohusika kuyafanyia kazi
manung’uniko haya ya wananchi na wawachukulie hatua kali za kisheria madereva
watakaobainika kuvunja sheria kwa sababu ya ukubwa wa vyombo wanavyoviendesha.
Hatuwezi kuwaruhusu madereva wasiojali
utu kuendelea kukiuka sheria na kusababisha ajali.
Kadhalika, wananchi waendelee kuelimishwa
juu ya masuala ya usalama barabarani na matumizi mazuri ya barabara, ili uzuri
wa barabara zetu tunazoendelea kuzijenga ulete faraja kwa wananchi badala ya
kusababisha madhara ya kupata ulemavu au kupoteza maisha.
Ndugu
Wananchi,
Namalizia hotuba yangu kwa kutoa pongezi na
shukurani zangu kwa Kamati ya maandalizi ya sherehe hizi kwa kazi nzuri ambayo
sote tumeridhika nayo. Natoa shukurani kwa Wizara ya Katiba na Sheria kwa
kushirikiana vyema na viongozi mbali mbali wakiwemo Maafisa Wadhamini wote
katika kila hatua. Ni dhahiri kuwa kufanikiwa kwa sherehe zetu za leo
kumetokana na michango ya kila mmoja wenu. Shukurani zangu za dhati kwa
viongozi na wananchi wote wa Mkoa wa Kaskazini Pemba pamoja na wananchi wote wa
Pemba kwa mapokezi mazuri na mahudhurio makubwa katika sala ya Iddi leo asubuhi
na kwenye Baraza hili la Idd-el-Hajj.
Kwa
pamoja tuendelee kuwaombea dua Mahujaji wetu iwe Hijjah Mabrur kwao na Mwenyezi Mungu awarudishe nyumbani kwa
salama. Mwenyezi Mungu (SW) atuzidishie amani, umoja na mshikamano ili tuweze
kupiga hatua zaidi za maendeleo. Awape afya njema na subira wagonjwa wetu
walioko majumbani na hospitalini.
Awarehemu wazee wetu na awasamehe makosa yao wote waliokwishatangulia
mbele ya haki. Mwenyezi Mungu atupe mvua zenye kheri na baraka na neema ya
mazao. Atujaalie sote turudi nyumbani kwa salama na tusherehekee sikukuu hii
kwa amani, furaha na utulivu.
Wassalamu Aleikum Warahmatullah Wabarakatuhu
IDD MUBARAK, WAKULLU AAM WAANTUM
BIKHEIR
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment