Na Mwandishi wetu, Tabora
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete, amesema serikali imeanza kuchukua hatua kuandaa
kura maoni kuhusu katiba mpya na kuwataka wananchi siku itakapofika wakafanye
maamuzi.
Akizungumza katika sherehe za
kumbukumbu ya kifo cha Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere,
ambazo kitaifa zilifanyika Tabora, alisema hata hivyo, katiba inayopendekezwa
ni bora kuliko katiba ya sasa.
Alisema katiba hiyo inatoa
majubu sahihi kwa changamoto zilizopo sasa na kutoa mapendekeo ya kutatua
changamoto za kesho.
Aliwahimiza wananchi kujitokeza
kwa wingi kwenye kura ya maoni na kuiunga mkono katiba hiyo kwa kuipigia kura
ya ndio.
Aidha aliwataka wananchi
kuisoma katiba hiyo ibara moja baada ya nyengine na kuwatahadharisha kuepuka
kuondolewa kwenye malengo yenye maslahi kwao na kubeba ajenda za watu wengine wenye maslahi
yao binafsi.
Kuhusu rushwa, alisema serikali
itaendelea na mapambano na kuwataka wafanyakazi kuwafichua viongozi wanaochukua
rushwa badala ya kuwatukuza au kuwalinda na kufikiria kazi hiyo ni ya TAKUKURU
pekee.
Kuhusu vita vya dawa za
kulevya,alisema mapambano hayo ni magumu mno, ingawa kuna mafanikio
yaliyopatikana.
Alisema zaidi ya watu 6,000
wamekamatwa wakisafirisha dawa za kulevya ingawa bado changamoto za kuwadhibiti
ni kubwa kutokana na kubadilisha mbinu kila mara.
Aliwataka vijana kuacha
kutumiwa kusafirisha dawa za kulevya au kutumia dawa hizo na kwamba serikali
itaongeza mapambano kudhibiti uingizaji wa dawa hizo.
Alilipongeza Bunge Maalum la
Katiba kwa uamuzi wake wa kusimamia kwa vitendo misngi iliyoachwa na Mwalimu
Nyerere kuhakikisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuwa moja.
Kuhusu Ukimwi hasa mkoa wa
Tabora, alisema asilimia tano ya wakazi wa mkoa huo wanaishi na ugonjwa huo
ambapo watu watanao kila watu 100 wameambukizwa ugonjwa huo, kiwango ambacho
alisema ni kikubwa.
No comments:
Post a Comment