Habari za Punde

Tume ‘Opereshen​i Tokomeza’ kwenda Kagera, Geita, Shinyanga, Simiyu, Mwanza na Mara keshokutwa 23 Oktoba

Na Mwandishi Wetu
Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Operesheni Tokomeza Ujangili imetangaza ratiba ya pili ya ziara yake katika Mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Simiyu, Mwanza na Mara ili kukusanya taarifa na kupokea malalamiko yaliyotokana na utekelezaji wa Operesheni hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa mwishoni mwa wiki na Katibu wa Tume hiyo Wakili Fredrick Manyanda (pichani), Tume hiyo itatembelea mikoa hiyo kuanzia keshokutwa Alhamisi, Oktoba 23, mwaka huu hadi tarehe Novemba 18 mwaka huu.

Katika awamu ya kwanza iliyofanyika kuanzia tarehe 17 Septemba, 2014 na kumalizika tarehe 6 Oktoba, 2014 ambapo Tume ilitembelea mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa na Mbeya na kukutana na wananchi katika wilaya za Wilaya za Kibondo, Kasulu, Uvinza, 
Mpanda, Sumbawanga, Mbozi na Mbarali.

Katika awamu ya pili, Wakili Manyanda ameeleza katika taarifa yake kuwa, Tume itatembelea Wilaya ya Bukoba Mjini tarehe 23 Oktoba na tarehe 24 mpaka tarehe 27 Oktoba 2014 itakuwa Wilaya ya Muleba kwa Mkoa wa Kagera. Na kwa Mkoa wa Geita, Tume itatembelea Wilaya ya Chato tarehe 28 na tarehe 29 Oktoba, 2014 na kuanzia tarehe 31 Oktoba, 2014 mpaka tarehe 1 Novemba, 2014 Tume itakuwa katika Wilaya ya Bukombe.


Kwa Mkoa wa Simiyu, Tume itatembelea Wilaya ya Meatu tarehe 5 Novemba, 2014 na Wilaya ya Bariadi tarehe 8 Novemba, 2014. Na kwa Mkoa wa Mara Tume itatembelea Wilaya ya Bunda tarehe 10 na tarehe 11 Novemba, 2014; Wilaya ya Tarime itakuwa tarehe 13 mpaka tarehe 15 Novemba, 2014 na Wilaya ya Serengeti tarehe 17 mpaka tarehe 18 Novemba, 2014.

Aidha, pamoja na mikutano hiyo, Wakili Manyanda amewaomba wananchi kutuma taarifa na malalamiko kwa njia ya barua, simu na barua pepe. Wananchi wanaweza kutuma barua kwa Katibu wa Tume, Tume ya Uchunguzi wa Operesheni Tokomeza Ujangili, SLP 9050, Dar es Salaam na barua pepe kwenda opereshenitokomeza@agctz.go.tz.

Kuhusu ujumbe mfupi wa maandishi, wananchi wanaweza kutuma kwa namba za simu: Tigo: 0714 826826; Vodacom: 0767 826826; Airtel: 0787 826826; na Zantel: 0773 826826. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.