Na Hafsa Golo
Licha ya serikali kujipanga kuhakikisha inaimarisha ulinzi na usalama
katika maeneo ya ukanda wa bahari,bado kumekuwa kukijitokeza changamoto mbali mbali kunakosababishwa na upungufu wa
vitendea kazi.
Hali hiyo imesababisha bidhaa za magendo na
uingizaji wa dawa za kulevya kuiendelea.
Kamanda wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo,
Luteni Hussein Ali Makame, alisema maeneo ya bahari mara nyingi hutumiwa na
maharamia pamoja na watu ambao wanajishughulisha na biashara haramu kuvushia
bidhaa zao.
Alisema kikosi hicho katika doria zake
kimekamata vyombo vidogo venye silaha na mabomu na boti moja ndogo yenye mashine na vifaa vya
matumizi ambayo ilisadikiwa ni ya maharamia.
Aidha alisema tukio jengine walilolibaini katika
doria zao ni wavuvi wa kigeni kutumiwa bahari ya Zanzibar kwa shughuli za uvuvi haramu.
“Tuliwahi
kukamata boti namba 9 ya Maputo Msumbiji ikifanya uvuvi bila kufuata sheria,”
alisema.
“Zanzibar ni visiwa na siku zote doria
zinatakiwa kufanywa lakini kukosekana nyezo za kisasa za doria kunasababisha
shughuli za doria kukwama,” alisema.
Meja Jenerali Rogastian Shabani Laswari wa jeshi
la Wananchi Tanzania,ambae pia ni Kamanda wa kikosi cha majini, alisema eneo la bahari ni kubwa hivyo linahitaji doria za mara kwa
mara jambo ambalo limekuwa changamoto
kutokana na uhaba wa vitendea kazi.
Alisema kutokana na changamoto hizo, itakuwa
vigumu kuzuia kwa asilimia 100, kuwadhibiti wakorofi kutumia bahari hiyo kwa
shughuli zao.
Hata hivyo, alisema suala la usalama kwa jumla
linaridhisha licha ya kuwepo changamoto kadhaa.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini (ZMA),
Abdi Omar, alikiri kuwepo kwa changamoto katika usafiri wa bahari hususan
maeneo ya bandari bububu ambapo zimekuwa zikitumika katika usafirishaji wa
biashara haramu kwa lengo la kukwepa kodi.

No comments:
Post a Comment