Habari za Punde

DKT. SHEIN KUWA MGENI RASMI MASHINDANO YA KITAIFA YA RIADHA ZANZIBAR



Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Bi Sharifa Khamis akizungumza na Wanahabari kuhusu Mashindano ya kitaifa ya Riadha yatakayofanyika Disemba 26-27 mwaka huu katika Ukumbi wa wizara ya habari Kikwajuni mjini Zanzibar. Rais Shein anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi wa Mashindano hayo. Picha na Makame Mshenga. 
Mwashungi Tahir-Maelezo Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohammed  Shein anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi katika mashindano ya Kitaifa ya Riadha ya wilaya  ambayo yanatarajiwa kufanyika katika kiwanja cha Amaani Disemba 26-27 mwaka huu.

Mashindano hayo yaliyodhaminiwa na Rais Shein kwa lengo la kukuza sekta ya michezo nchini yametayarishwa na Baraza la michezo la Taifa Zanzibar (BMTZ) kwa kushirikiana na chama cha Riadha (ZAAA)

Hayo yameelezwa leo na Mwenyekiti wa baraza la michezo Bi Sharifa Khamis  katika ukumbi wa wizara ya habari , utamaduni, utalii na michezo huko kikwajuni wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema  mashindano hayo yatakayozishirikisha Wilaya zote 10 za Unguja na Pemba yatajumuisha wanariadha 250 ambapo michezo yote ya riadha ikiwemo kukimbia masafa ya mita 100 , 200, 400, na 1500 kwa wanawake na wanaume itafanyika.

Aidha ameongeza kuwa jumla ya vikundi 12 kutoka Kenya , Uganda na Tanzania Bara vimealikwa kushiriki Mashindano hayo.

Amefahamisha kuwa sambamba na Riadha pia kutakuwa na michezo ya kurusha mkuki , tufe, ,na kisahani.

Amebainisha kuwa Washiriki wa mashindano hayo watapatiwa huduma zote za michezo  bure ikiwemo malazi , mavazi ya michezo , chakula, usafiri na zawadi zote za washindi za vikombe , medali na fedha taslim.


“Lengo kuu la mashindano hayo ni kuinua mchezo wa riadha Zanzibar kuanzia vijijini , maskulini na maeneo mengine mbali mbali kwa nia ya kutafuta vipaji vya wanariadha kutoka katika sehemu hizo ili kuviendeleza vipaji hivyo “ alisema Bi Sharifa.

Amesema dhamira ya Rais wa Zanzibar ni kuona Zanzibar inarejesha hadhi yake ya asili ya ubingwa katika michezo tofauti  ambayo amesema sifa hiyo imepotea kwa kipindi kirefu ikilinganishwa katika miaka 70.

Mashindano hayo nisehemu ya utekelezaji wa sera tya michezo Zanzibar , ambayo inasisitiza kuwa vyama vyote vya michezo Zanzibar vifanye jitihada za makusudi za kuinua michezo ili nchi iweze kupiga hatua kubwa katika michezo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.