Habari za Punde

JK aongeza miezi sita kukamilisha maabara

Na Mwandishi wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, amewaongezea muda wa miezi sita viongozi na wasimamizi wa ujenzi wa maabara katika skuli za sekondari nchini, ili kuwawezesha kukamilisha kazi hiyo ipasavyo.

Aidha alitoa pongezi kwa wananchi wa Tanzania na viongozi kwa kazi kubwa waliyoifanya katika ujenzi wa maabara nchini.

Alisema anachangia shilingi milioni 200 katika Mfuko Maalum wa Dhamana (Endowment Fund For Excellence) wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela.

Alisema hayo jana wakati alipozungumza na uongozi, wahitimu na wana-jumuiya ya taasisi hiyo, baada ya ametunukiwa shahada ya uzamivu ya heshima (PhD honoris causa) ya taasisi hiyo katika mahafali ya pili yaliyofanyika Tengeru, Arusha.

Alitunukiwa shahada hiyo na Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Mhe.Mohamed Gharib Bilal ambaye ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela ni chombo cha elimu ambacho hutoa wahitimu wa shahada za uzamili na uzamivu (PhD) tu katika sayansi na teknolojia na ni moja ya taasisi mbili tu za aina hiyo katika bara la Afrika.

Pia alizungumzia maendeleo ya ujenzi wa maabara ya masomo ya sayansi nchini ambalo lengo lake ni kutekeleza agizo lake la kuhakikisha skuli zote za sekondari nchini zinajenga maabara ya kufundishia masomo ya sayansi.


Alitoa agizo hilo miaka miwili iliyopita, Novemba 2012 na akatoa miaka miwili kukamilisha kazi hiyo ifikapo Novemba 30 mwaka 2014.

Alitoa agizo hilo baada ya kubaini kuwa ukosefu wa maabara kwa ajili ya masomo ya fikizia, kemia na biolojia ilikuwa moja ya sababu ya kuwakatisha tamaa wanafunzi nchini kupenda masomo ya sayansi.

Alisema umuhimu wa kujenga maabara uliongezwa kasi na ongezeko kubwa la skuli za sekondari ambazo ziliongezeka kutoka 828 mwaka 2004 hadi kufikia 3, 551 kwa sasa.

Kati ya hizo ni 88 zilizokuwa na vyumba vitatu kwa ajili ya masomo hayo matatu ya sayansi.


Alisema tathmini ya sasa inaonesha kuwa zinatakiwa zijengwe maabara kwenye skuli 3,463 ambazo ni sawa na vyumba 10,389 na kuwa tathmini hiyo inaonesha hadi Disemba 7, 2014, vilikuwa vimejengwa vyumba 3,867 vya maabara ambavyo ni sawa na asilimia 37.2 ya mahitaji ambavyo vimekamilika, vyumba 5,891, sawa na asilimia 56.7 ambavyo viko katika hatua mbali mbali za kukamilishwa na vyumba 631 ama sawa na asilimia 6.1 ambavyo ujenzi wake haujaanza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.