STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
4.1.2015
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa lengo la Mapinduzi Matukufu ya
Januari 12, 1964 ni kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi wote popote pale
walipo tena bila ya ubaguzi wa rangi, dini, kabila ama kwa itikadi ya kisiasa.
Dk. Shein
aliyasema hayo leo huko Umbuji, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja
katika uzinduzi wa barabara ya
Njia nne- Umbuji iliyojengwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia
Mfuko wake wa Barabara, ikiwa ni miongoni mwa maadhimisho ya miaka 51 ya
Mapinduzi ya Zanzibar ambapi pia, Dk. Shein aliridhia barabara hiyo kuitwa jina
lake kama alivyoobwa na wananchi wa kijiji hicho.
Katika uzinduzi
huo viongozi mbali mbali wa vyama na Serikali pamoja na wananchi walihudhuria
akiwemo Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd.
Katika hotuba yake
aliyoitoa mara baada ya kuizindua barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 5.1, Dk. Shein alisema kuwa suala la
maendeleo halina mjadala na haliusiani kabisa na itikadi za vyama vya siasa
kwani misingi ya kuwepo kwa vyama vya siasa ni maendeleo kwani hiyo ndio nia ya
Serikali anayoiongoza.
Dk. Shein alisema
kuwa Serikali ina wajibu wa kuwapelekea
maendeleo wananchi wake popote pale walipo na ndio maana imechukua juhudi za
makusudi za kuwajengea barabara wananchi wa kijiji cha Umbuji ikiwa na azma ya
kuwafikishia maendeleo wananchi wake.
“Leo suala la
barabara kwa wananchi wa Umbuji tumelimaliza na kama alivyosema Katibu Mkuu wa
Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano lengo ni kuhakikisha barabara hii
inajengwa hadi Uroa hatua kwa hatua...jambo ambalo lilikuwa linaniumiza roho
basi ni barabara hii ya Umbuji”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alisema Zanzibar itajengwa na
Wazanzibari wenyewe kwani hilo ndio lengo la Mapinduzi matukufu ya Januari 1964
huku akieleza kuwa wazee wameanza kutekeleza juhudi za maendeleo na hivi sasa
vizazi viliopo ni lazima viendeleze kwani hilo ndio lengo la Mapinduzi.
Dk. Shein alisema
kuwa wakati Zanzibar inaadhimisha miaka 51 ya Mapinduzi tayari kuna mtandao
mzuri wa barabara nchi nzima hali iliyowezesha kuunganisha vyema miji na vijiji
katika maeneo yote ya Unguja na Pemba na kutoa pongezi kwa uongozi wa Wizara
hiyo kwa ujenzi wa barabara hiyo sambamba na nyenginezo zinazoendelea.
Alisisitiza kuwa
hizo ni juhudi za makusudi zilizochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
ya kutafsiri kwa vitendo shabaha ya Mapinduzi kwa kuwafikishia huduma wananchi wake
wote popote walipo tena bila ya ubaguzi huku akiahidi utekelezwaji wa ombi lao
la ujenzi wa barabara ya Pagali hatua kwa hatua.
Aidha, Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kwa kuwanasihi madereva wakataotumia barabara hiyo
kuzingatia sheria za usala wa barabarani kwa kuacha kwenda mwendo wa kasi,
kutopakia abiria zaidi ya kiwango kilichokubaliwa sambamba na kuacha kufanya
matengenezo ya magari barabarani.
Pia, Dk. Shein
aliwataka wananchi kuwacha kutumia barabara kama vikao vya mazungumzo na kutoa
agizo kwa wananchi kufuata taratibu zilizowekwa
za hifadhi ya barabara kwa kutojenga katika maeneo yaliowekwa viguzo
wala kufanya shughuli nyengine zozote kwani maendeleo yanazidi kuimarika kwa
hapo baadae njia inawezekana ikawa ndogo na ikahitaji kupanuliwa.
Pamoja na hayo,
Dk. Shein aliwahakikishia wananchi wa Umbuji kuwa Serikali imo katika mchakato
wa kujenga kituo kipya cha Afya katika kijiji chao na kuwataka waendelee kuwa
na subira kwa hilo huku akitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa wananchi wa
Umbuji kukataa kulipwa fidia wakati wa ujenzi wa barabara hiyo.
Katika maelezo
yake Dk. Shein aliwaeleza wanakijiji wa Umbuji kuwa haikuwa jambo la makusudi
Serikali kuchelewesha ujenzi wa barabara hiyo bali hali hiyo imetokana na
kuwepo kwa uhaba wa vifaa vya ujenzi wa barabara hapa nchini jambo ambalo
serikali imo katika juhudi ya kulipatia ufumbuzi.
Nae Waziri wa
Miundombinu na Mawasiliano Mhe. Juma Duni Haji alisema kuwa ni mfano wa kuigwa
kwa kitendo cha wanakijiji wa Umbuji kukataa kulipwa fidia wakati wa kupitisha
ujenzi wa barabara hiyo kitendo ambacho ni cha kizalendo na kueleza matumaini
yake ya kuimarika kwa maendeleo katyika kijiji hicho kutokana na barabara hiyo.
Mapema Katibu
Mkuu wa Wiza hiyo Juma Malik Akil alisema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ulianza
mwaka mwishoni mwa mwaka 2009 na kuendelea hadi
Oktoba 2013 katika hatua ya kifusi na kukamilika rasmi Novemba 24 mwaka
jana kwa kiwango cha lami.
Alisema kuwa
kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kunatokana na jitihada na ahadi za Dk.
Shein katika kuwapelekea wananchi maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.
Alisema kuwa
barabara hiyo ina uwezo wa kupita magari kwa kasi ya mwendo wa kilomita 60 kwa
saa na yenye uzito unaofikia tani 15 ambapo pia, barabara hiyo ni ya mwanzo
kabisa kuwekewa viguzo vya hifadhi ya barabara katika kila upande wa barabara
na kuwaomba wananchi kuziheshimu na kuzitunza alama hizo.
Aidha, alisema
kuwa jumla ya fedha zilzotumika katika ujenzi wa barabara hiyo ni milioni
840.5, gharama ambazo ni nafuu zaidi ikilinganishwa na gharama halisi kutokana
na kutengenezwa na wataalamu wa hapa nchini sambamba na kutumia malighafi za
hapo hapo kijijini.
Alisema kuwa
kutokana na juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha mfumo
wa usafiri hivi sasa Zanzibar imefikia kuwa na mtandao wa barabara wenye jumla
ya kilometa 1,235.52 (Unguja kilometa
704.03 na Pemba kiloeta 531.50).
Nao wananchi
katika risala yao walitoa shukurani kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya
uongozi wa Dk. Shein kwa kujengewa barabara yao hiyo na kumpongeza Dk. Shein
kwa kutekeleza ahadi yake ya kujengwa barabara hiyo wananchi wa kijiji hicho.
Aidha, kwa umoja
wao wananchi hao walimuomba akubali barabara hiyo kuitwa kuitwa jina lake
kutokana na juhudi zake za kuhakikisha
kijiji hicho kinafikiwa na barabara ya lami ambayo itawasaidia katika shughuli
zao za maendeleo ikiwemo kusafirisha bidhaa zao za kilimo pamoja na shughuli
zao za kijamii.
Walieleza kuwa
tayari kwa kiasi kikubwa huduma za maendeleo zimeshawafikia kama vile maji safi
na salama, umeme, skuli za msingi na Sekondari, kituo cha afya pamoja na huduma
nyengine muhimu ikiwemo huduma ya afya ambayo waliomba kujengewa kituo kipya
cha afya cha kisasa ambapo Dk. Shein alisema kuwa tayari mchakato wake
unaendelea.
Uzinduzi huo
ulipambwa kwa burudani mbali mbali ikiwemo ngoma ya Kibati yenye asili ya
Kisiwani Pemba katika Mkoa wa Kusini pamoja na utenzi pamoja na burudani
nyenginezo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment