Habari za Punde

Kutoka baraza la Wawakilishi: Serikali inajiandaa kuongeza upatikanaji samaki kukidhi mahitaji


Na Abdulla Ali Maelezo-Zanzibar                                              28/01/2015

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Zanzibar Mhe. Abdilahi Jihadi Hassan amesema Serikali ina mipango madhubuti ya kuongeza upatikanaji wa samaki ili kukidhi mahitaji ya hoteli za utalii na walaji kwa ujumla.

Hayo ameyaeleza katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Wilaya ya Magharibi Unguja wakati akijibu swali la mwakilishi wa Jimbo la Kwahani Mhe. Ali Salum Haji.

Amesema mikakati hiyo ni kuwawezesha wavuvi kuvua katika kina kirefu cha maji ambapo hivi sasa Wizara yake imeshawapatia mafunzo ya uvuvi wa bahari kuu Vijana 25 katika chuo cha uvuvi Mbegani na hatua ya kupeleka wengine zinaendelea kulingana na hali ya fedha itakavyoruhusu.

Vilevile amesema mkakati mwengine ni kuwezesha uzalishaji wa samaki kwa njia ya Ufugaji na mazao mengine ya Baharini ambapo mikakati hiyo itaongeza upatikanaji wa samaki kwa wingi na hivyo kupunguza uwezekano wa kuingizwa samaki wasio na uhakika  na usalama kwa walaji nchini.

Waziri Abdilahi amefafanua kwamba itakapotokea uingizaji wa samaki nchini, watachunguzwa na kuhakikishwa ubora wao na mamlaka zinazohusika ikiwemo Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi kabla ya kuruhusiwa kuingizwa nchini.

Wakati huohuo Waziri Abdilahi ametanabahisha wakati akijibu swali la muakilishi wa jimbo la Wawi Mhe. Saleh Nassor Juma kuwa uzalishaji wa samaki bado ni mdogo na unakidhi soko la ndani pekee kwa sasa.

Hivyo Wizara yake imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kuwashawishi Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika Sekta ya Uvuvi ili kuongeza uzalishaji wa samaki ikiwa ni pamoja na kujenga Viwanda vya kusindikia samaki.

Amesema hayo yatatekelezwa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Uwekezaji na Taasisi nyengine na hivi sasa kuna wawekezaji kadhaa ambao wameonyesha nia ya kuwekeza katika sekta ya Uvuvi pamoja na kujenga viwanda hivyo.

Mhe. Abdilahi amesema mazingira ya uwezekezaji yameshawekwa na serikali, hivyo amewataka wawekezaji kujitokeza ili kutimiza lengo hilo na kusaidia kukuza uchumi wa nchi kupitia shughuli za uvuvi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.