Na
Abdulla Ali Maelezo-Zanzibar 28/01/2015
Wananchi
wametakiwa kujiepusha na vitendo vya kihalifu ili kuepusha uvunjifu wa amani
nchini.
Hayo
yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mhe. Mohamed
Aboud Mohamed katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Wilaya ya
Magharibi Unguja wakati akijibu swali la mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe Mhe.
Salim Abdalla Hamad.
Amesema
endapo mtu atatuhumiwa kutenda vitendo hivyo vya kihalifu sheria zitatumika
bila ya kumuonea au kumkandamiza mtu yeyote ili kuhakikisha amani na utulivu
inabakia na kudumishwa nchini.
Amefafanua
kuwa ni utaratibu wa kisheria katika nchi za Jumuiya ya Madola kwamba nchi ina
mamlaka ya kumfikisha muhalifu mahakamani na kumshitaki iwapo tukio husika la
kihalifu limetokea katika nchi hiyo, hivyo endapo tukio la uhalifu limetokea
Tanzania Bara na endapo limetokea Zanzibar, mahakama za Zanzibar pia zinaweza
kuwashitaki watuhumiwa hao.
Ametanabahisha
kuwa Katiba ya Zanzibar ya 1984, kifungu cha 101 kinaweka masharti ya kikatiba
ya utaratibu wa utekelezaji wa hati za mahakama ndani ya Zanzibar na Tanzania Bara
kwa ujumla na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 124 imeweka
masharti kama yaliyomo kwenye kifungu cha 101 cha Katiba ya Zanzibar.
Waziri
Aboud amesema kwa mujibu wa masharti ya vifungu vya katiba vilivyotajwa ni
utaratibu halali wa kisheria wa mtuhumiwa kukamatwa upande mmoja wa Muungano na
kupelekwa upande mwengine wa Muungano endapo uhalifu umetokea na kutendwa
katika eneo husika.
Aidha
Waziri Aboud amefafanua kuwa misingi ya katiba zote mbili kuna utaratibu pia wa
kisheria ambapo Mzanzibari au Mtanzania yeyote ambae atatuhumiwa kutenda kosa
lolote la uhalifu nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anaweza kukamatwa na
kupelekwa nchi ambayo atatuhumiwa kutenda kosa na kushitakiwa.
Amesema
Sheria hizo ni Sheria ya kubadilishana wahalifu Sura ya 368 (Extradition Act
Cap. 368) na Sheria ya kusaidiana katika mambo ya jinai Sura ya 254 (The Mutual
Assistance in Criminal Matters Act Cap. 254) sheria hizo zote zinaweka masharti
na utaratibu wa kubadilishana wahalifu.
No comments:
Post a Comment