Na Abdulla Ali Maelezo- Zanzibar 21/01/2015
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mhe.
Mohamed Aboud Mohamed amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imeshatayarisha kanuni za usalama wa barabarani za kutoza faini za papo kwa
papo kama ilivyo sasa kwa upande wa Tanzania
Bara.
Hayo ameyaeleza katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi
Chukwani Zanzibar wakati akijibu swali la mwakilishi wa Jimbo la Kwahani Mhe.
Ali Salum Haji.
Waziri Mohamed amesema kuwa kanuni za sheria ya
usalama barabarani kwa upande wa
Zanzibar zipo kwa Mwanasheria Mkuu kwa
hatua za mwisho na zitaanza kutumiwa na Jeshi la Polisi mara baada ya
kukamilika rasmi kwa kutoza faini ya papo kwa papo kwa wote watakaofanya makosa
ya usalama wa barabarani.
Waziri Aboud ametanabahisha kuwa kwa sasa Zanzibar
Sheria Nambari 7 ya Mwaka 2003 (R.E 2006) ndio inayosimamia masuala ya usalama
barabarani na kwa mujibu wa sheria hiyo kifungu namabari 180 hadi 184
vimeelezea kuhusiana na utaratibu wa faini ya papo kwa papo kwa vyombo vya moto
vinavyovunja sheria za usalama wa barabarani Nchini.
Aidha amesema Jeshi la Polisi lina jukumu la kusimamia
na kutekeleza Sheria zilizotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ambapo
kwa upande wa Tanzania Bara Sheria inayohusika na usalama wa barabarani ni
Sheria nambari 168 ya Mwaka 2002.
“Miongoni mwa majukumu ya Jeshi la Polisi ni kusimamia
na kutekeleza Sheria zilizotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ”, alieleza waziri
Mohamed.
Hivyo ameeleza kuwa kupitia Sheria hiyo Jeshi la
Polisi hutekeleza sheria za faini ya papo kwa papo kwa vyombo vya moto
vinavyovunja sheria za usalama barabarani na kusaidia Serikali kukusanya fedha nyingi
zinazotokana na makosa hayo.
Jeshi la polisi ni Jeshi la Jamhuri ya muungano wa
Tanzania na limeundwa kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977
chini ya ibara ya 147 ya kuanzishwa kisheria chini ya kifungu nambari 3 cha
sheria ya polisi na polisi wasaidizi Cap.322 R.E ya mwaka 2002.
No comments:
Post a Comment