Na Abdulla Ali Maelezo- Zanzibar 21/01/2015
Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Mhe. Nassor
Ahmed Mazrui amesema kutokuwepo kwa mashine za kisasa za kupimia bidhaa ndiko
kunakopelekea kukosekana kwa vipimo vya kisasa, vya kitaalamu na vya uhakika
vya bidhaa hizo na kupelekea uingizwaji wa bidhaa feki.
Hayo ameyaeleza katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi
Chukwani Zanzibar wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani Mhe. Ali
Salum Haji.
Waziri Mazrui ametanabahisha kuwa kutokana na ukosefu
wa vifaa hivyo ikiwemo mashine ya ICP kunafanya baaadhi ya bidhaa kushindwa
kufanyiwa vipimo wakati zinapoingizwa nchini na kusababisha hasara na madhara
makubwa kwa watumiaji wa bidhaa hizo kwani nyingi zao huwa ni feki.
Waziri Mazrui amesema kutokana na ukuaji wa biashara
nchini kumejitokeza baadhi ya wafanyabiashara ambao huingiza bidhaa feki za
kulainisha vyombo vya moto kama vile Girisi na
Oil pamoja na vyakula vilivyokwisha muda wake.
“Kwanza naomba kukiri kuwa kwa hivi sasa Wizara yangu
haina utaratibu wa kukagua bidhaa za vilainisho ingawa nakubaliana na mjumbe
kuwa hii ni mojawapo ya bidhaa au huduma nyengine zinazopaswa kusimamiwa”,
alieleza Waziri Mazrui.
Aidha Waziri Mazrui amewaomba viongozi na Wajumbe wa
Baraza hilo kushirikiana na taasisi nyengine za serikali kuangalia mfumo bora
wa kusimamia biashara hizo ambazo kwa sasa hazina mfumo mzuri wa kuzisimamia
sambamba na kuwataka wananchi kutoa taarifa kwa Wizara yake pale ambapo
wanagundua uingizwaji au uuuzwaji wa bidhaa feki madukani.
No comments:
Post a Comment