Na Abdulla Ali Maelezo- Zanzibar 21/01/2015
Vitendo vinavyokwenda kinyume na maadili ya kijamii
vimekuwa vikishamiri kwa kasi miongoni mwa vijana wa Zanzibar licha ya viongozi
wa Dini, Wazee na Walimu kuvikemea vitendo hivyo.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Habari, Utamaduni, Utalii
na Michezo Mhe. Bi Hindi Hamad Khamis wakati akijibu swali la mwakilishi wa Jimbo
la Muyuni Mhe. Jaku Hashim katika mkutano wa
18 wa Baraza la Wawakilishi ulioanza
leo Chukwani Zanzibar.
Amesema kuwa hivi sasa imekuwa ni jambo la kawaida kwa baadhi ya vijana wa kiume hususan
wa Kizaanzibari kutoboa masikio, kusuka nywele na kujipodoa jambo ambalo ni
kinyume cha sheria, Silka na Utamaduni wa Mzanzibari.
Mhe Bi Hindi amesema Serikali imechukua hatua
mbalimbali katika kupambana na tatizo la uvunjifu wa Mila, Silka na Desturi ikiwa
ni pamoja na kushajihisha kutolewa elimu ya Dini na Malezi, Kulinda na Kuhimiza
uendelezaji wa Utamaduni pamoja na kusambaza ustaarabu wa Mzanzibari kwa njia
ya Sanaa ya Maonyesho, Semina na Makongamano.
Mhe. Bi Hindi ametanabahisha kuwa ili kuondokana na
vitendo hivyo viovu, Serikali inapitia upya sheria zilizopo zinazohusiana na
mambo ya Mila, Silka na Desturi kwa lengo la kuzipa nguvu ili kupunguza kasi ya
vitendo vinavyoipaka matope Zanzibar ambavyo kwa kiasi kikubwa vinachangiwa na
uwepo wa utandawazi duniani kote.
Aidha amesema tatizo liliopo sio kutokuwepo kwa sheria
bali ni usimamizi wa sheria hizo na kuthibitishwa kwa makosa mbele ya vyombo
vya sheria ili kuweza kuchukuliwa hatua zinazofaa.
“Kwa kulipatia ufumbuzi tatizo hili, sisi sote hapa ni
viongozi na wananchi kwa ujumla tunatakiwa kushirikiana kupiga vita vitendo
hivyo na kutilia nguvu usimamizi wa sheria tunazozitunga”, alieleza Naibu
waziri Bi hindi.
Mhe. Bi Hindi amewataka Viongozi, Walimu, Viongozi wa Dini na Wananchi kwa ujumla kushirikiana pamoja katika
kupiga vita vitendo hivyo viovu na kutilia mkazo usimamizi wa sheria ili
kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
Msitudanganye wenye kukemea na kukataza maovu hasa ni mashekhe wetu ambao mumewaweka jela.
ReplyDelete