Na: Hassan Hamad (OMKR).
Chama cha Wananchi CUF kimesema kimejipanga ili kuhakikisha kuwa kinaweka historia mpya ya Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa Oktaba mwaka 2015.
Katibu Mkuu wa chama hicho Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad ametoa kauli hiyo leo katika hafla ya kukabidhi mashine tisa za boti kwa ajili ya matawi ya chama hicho jimbo la Mji Mkongwe.
Mashine hizo zenye thamani ya shilingi milioni 36 zimetolewa na Mbunge wa jimbo hilo(CUF) Mhe. Ibrahim Sanya, ambaye pia amekabidhi shilingi milioni 27 kwa ajili ya ununuzi wa boti.
Maalim Seif amesema katika kutekeleza mkakati huo chama hicho hakitomvumilia kiongozi yoyote aliyevunja mkataba wa chama, ikiwa ni pamoja na wabunge walioshindwa kutekeleza ahadi zao kwa wananchi.
Amesema CUF kitafanya uhakiki wanachama wote watakaojitokeza kugombea nafasi za kitaifa na baadae kuwahanyia usaili, ili kuhakikisha kuwa viongozi watakaochaguliwa wanalinda maslahi ya chama hicho na wala sio kutafuta maslahi binafsi.
Amempongeza Mbunge huyo kwa kutekeleza ahadi zake, kitendo ambacho amesema kimekijengea heshima chama hicho kwa kuonesha uaminifu kwa wapiga kura.
Amesema daima chama hicho kitaendelea kusimamia na kutekeleza ahadi kinazozitoa kwa wananchi, na kuwatahadharisha viongozi wa chama hicho kutoa ahadi zinazotekelezeka.
“Kama ahadi unayoitoa haitekelezeki tafadhali usiitoe kwa wananchi, hakikisheni viongozi kuwa mnatoa ahadi mnazoweza kuzitekeleza, vyenginevyo itakivunjia heshima chama chetu na hatutokubali jambo hilo”, amesema Maalim Seif wakati akihutubia katika mtaa wa Mwembe Tanga jimbo la Mji Mkongwe Zanzibar.
Katika hatua nyengine, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema wataendeleza jitihada zao ili kuona kuwa uchaguzi mkuu ujao unafanyika katika hali ya amani na utulivu.
Ametahadharisha kuwa iwapo kutakuwa na njama zozote za kuvuruga uchaguzi au matokeo ya uchaguzi huo, yeye hatohusika kuwashawishi vijana kwa lolote, na badala yake atawaachia watetee haki yao.
“Mwaka huu sishawishiki, hata aje IGP kuniambia niwaondoshe vijana wangu sitokubali, kwa hivyo nawaambia kabisa viongozi wa kitaifa mlijue hilo”, alisemaMaalim Seif.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mji Mkongwe Ibrahim Sanya, amewataka wananchi wa jimbo hilo kuzitumia mashine hizo kwa uangalifu ili ziweze kutumika kwa muda mrefu na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Amesema ataendelea kushirikiana na wananchi wa jimbo hilo katikajitihada za kuleta maendeleo, na kuahidikutekeleza ahadi zake zote alizozitoa kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Mapema akisoma risala ya wanachama wa CUF jimbo la Mji Mkongwe, katibu wa vijana wa jimbo hilo Mahamoud Ali Mahinda, amesema kitendo cha Mbunge huyo kutekeleza ahadi zake kwa wananchi, kimekijengea heshima chama hicho na kujenga imani kwa wananchi wa jimbo hilo.
Amesema mashine hizo pamoja na boti, zinasaidia kuongeza kipato kwa wananchi hao na kupunguza tatizo la ajira kwa vijana wengi wa Mji Mkongwe.
No comments:
Post a Comment