STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 21.1.2015

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imo katika juhudi za kuhakikisha uwepo
wa madaktari bingwa wa fani mbali mbali wakiwemo wanaohusiana na maradhi ya
mfumo wa utoaji wa haja ndogo katika kipindi kifupi kijacho.
Dk. Shein aliyasema
hayo huko katika ukumbi wa Hoteli ya Breezes iliyoko Bwejuu Mkoa wa Kusini
Unguja, katika mkutano maalum wa
wataalamu wa maradhi yanayohusiana na mfumo wa utoaji wa haja ndogo kutoka Uingereza ambao kwa mwaka huu
wameichagua Zanzibar kuwa ni sehemu ya kufanyia mkutano wao.
Mkutano huo pia,
umehudhuriwa na madaktari bingwa wa maradhi hayo kutoka Tanzania Bara, Dk.
Shein alitoa shukurani kwa Jumuiya hiyo kwa kuamua kufanya mkutano huo hapa
Zanzibar huku akieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kuwapata wataalamu wakiwemo wa maradhi yanayohusiana na haja ndogo na maradhi
mengineyo.
Alisema kuwa
juhudi za makusudi zimekuwa zikichukuliwa katika kuimarisha sekta ya afya hapa
nchini ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo
kwa lengo la kupata Madaktari ili kuongeza utoaji huduma kwa wananchi ambapo
kwa hivi sasa Daktari mmoja amekuwa akitibu watu 9,708.
Katika
kuhakikisha idadi ya Madaktari inaongezeka Dk. Shein alisema kuwa kwa kupitia
Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA)
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kukiimarisha Chuo chake cha
Madaktari ambacho hivi sasa kina wanafunzi 99 wanaosoma kwa mwaka wa kwanza na
wa pili.
Aidha, alisema
kuwa Serikali inakiimarisha Chuo chake cha Afya kilichopo Mbweni Zanzibar
ambacho kinatarajiwa kuwa sehemu ya Chuo
Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) pamoja na kuhakikisha Hospitali ya rufaa ya
Mnazi Mmmoja inafikia lengo lililowekwa sambamba na ujenzi wa hospitali ya
kisasa ya Mkoani Pemba unaoendelea.
Dk. Shein
alitumia fursa hiyo, kutoa shukurani kwa
juhudi zinazochukuliwa na Jumuiya
ya Misaada ya Uingereza ya Uimarishaji
wa programu za Afya hapa Zanzibar (HIPZ), kwa kuunga mkono juhudi za Serikali
katika kutoa na kuimarisha huduma hizo katika hospitali za Makunduchi na Kivunge. “Natumia fursa
hii kutoa shukurani kwa Dk. Ru McDonagh na madakatari wote kwa huduma
wanazozitoa katika hospitali hizi....”,alisema Dk. Shein.
Aidha, alisema
kuwa kuimarisha huduma za afya ni
miongoni mwa vipaumbele vikuu vilivyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika juhudi za kupunguza umasikini katika jamii licha ya baadhi ya changamoto
zilizopo ambazo kwa juhudi za pamoja na kwa mashirikiano ya washirika wa
maendeleo ufumbuzi wake utapatikana.
Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kueleza mafanikio yaliopatikana katika kuimarisha sekta ya afya hapa
nchini ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Sera katika sekta hiyo huku akieleza
azma ya Serikali anayoiongoza kuangalia uwezekano wa kutoa huduma bure za afya
kama ilivyotangazwa mara baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na Marehemu
Mzee Abeid Amani Karume.
Sambamba na hayo,
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa historia ya Zanzibar na hatimae Aprili 26,
1964 ilipojiunga na Tanganiyika na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
pamoja na kutoa historia katika sekta ya afya hapa nchini kabla ya Mapinduzi ya
Januari 12, 1964, baada ya Mapinduzi na hatua zinazochukuliwa hivi sasa.
Nao Madaktari
bingwa wa maradhi ya mkojo walioshiriki katika mkutano huo wakitoa mada mbali
mbali ikiwa ni pamoja na hatua zinazochukuliwa na Jumuiya hiyo kutoka Uingereza
ya kitengo cha maradhi ya haja ndogo katika kuyatafutia ufumbuzi maradhi hayo
nchini Uingereza sambamba na mafanikio yaliofikiwa.
Aidha, Madaktari
hao walieleza historia ya maradhi hayo pamoja na kuonesha juhudi zilizochukuliwa
nchini Uingereza tokea miaka ya 1800 pamoja na namna ya kutafuta tiba sambamba kuonesha
tafiti mbali mbali zilizofanywa na Madaktari bingwa wa nchi hiyo.
Madaktari hao,
walipongeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta ya
afya na kuunga mkono azma ya Serikali katika kuhakikisha wataalamu wa kutosha
wa maradhi hayo katika kipindi kifupi kijacho wanapatikana hapa Zanzibar.
Nae Dk. Roger
Plail, akitoa neno la shukurani kwa Dk. Shein alieleza kufarajika kwao na
uamuzi wa kuja Zanzibar kufanya mkutano huo wa wataalamu kutokana na mashirikiano
mazuri yaliopo kati yao na Madaktari wa Zanzibar akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya
Afya, Dk. Saleh Mohamed Jidawi pamoja na uongozi wa Hospitali ya Mnazimmoja.
Kwa niaba ya
Madaktari hao Dk. Plail alimpongeza Dk. Shein ambaye ni mtaalamu katika fani ya
Patholojia, kwa kuwapa maelezo ya kina juu ya sekta ya afya hapa nchini,
historia yake pamoja na juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha
mafanikio zaidi yanapatikana huku wakitoa shukurani kwa mwaliko rasmi aliowapa wa
chakula cha mchana hapo kesho (Ijumaa Januari, 22 mwaka huu) Ikulu mjini
Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment