Habari za Punde

‘Zanzibar Doors’ inawasaidiaje wananchi?

Na Charles Kayoka
 
Siku ya Mwaka Mpya nilipata fursa ya kutembelea kitongoji cha Kidimni kilichopo Unguja ili kuongea na wachongaji milango ya Zanzibar ijulikanayo kwa jina maarufu kama ‘Zanzibar door’.
Nilipoulizia wapi inachongwa milango hiyo maarufu yenye nakshinakshi na baadhi kuwekwa maandishi yaliyonukuliwa kutoka katika aya za Quran tukufu, nikaambiwa kuwa Kidimni ndiko hasa inakopatikana.
Pia, milango hiyo inaweza kupatikana Kilwa Kivinje, Mikindani, Bagamoyo, Pangani na Tanga mjini Nilifunga safari ya nusu saa kufika Kidimni. Nikakuta mafundi wakiwa kazini katika karakana yao iliyoko pembeni mwa barabara kuu. Hapo ndipo kitovu cha milango hiyo kwa sasa. Lakini karakana hii haitumii vifaa vya kisasa na mafundi baadhi ni wa umri mdogo tena wakiwa mafunzoni. Wakubwa nao wanaendesha biashara kwa uzoefu.
Hakuna shule ya kujifunzia, unakua ukiiga kutoka kwa waliokutangulia na wewe unahitimu baadaye uweze kuwafundisha wengine. Mafundi hawa hawana ufahamu wa soko wala wapi pa kuuza ila kwa kusubiri wateja kuja kutoa hitaji lao na wao kuchonga kwa kadiri ya mahitaji ya wateja wao.

Mafundi hawa wengi siyo wenyeji wa Unguja Mjini ambako wateja wengi wanatokea. Pengine hawajasafiri nje ya Zanzibar. Nilipowaambia kuwa milango yao inauzwa kama mali kale (antiques), katika masoko ya bidhaa za sanaa na ufundi ndani na nje ya nchi, walishangaa. Hawakujua kama kitu hicho hufanyika.
Kuna uwezekano mkubwa kuwa wateja wao pia huwatumia kupata bidhaa kwa bei ndogo na wao wakaenda kuuza kwingine kwa bei kubwa zaidi.
Pia, kuna suala la michoro yenyewe. Mteja huomba maneno ya Quran. Lakini mtindo wa kuyachonga maandishi yenyewe na maua yanayozunguka mlango wenyewe ni ubunifu wa fundi.
Je, anawezaje kuulinda ubunifu wake usiibiwe na watu wengine na kwenda kuchonga kwingineko? Fundi huyu wa Kidimni hana uwezo huo wa kulinda hatimiliki ya ubunifu wake.
Atabuni mtindo fulani wa kuchonga na wengine wataiga, lakini hawezi au hajui pa kwenda kulalamikia kuwa alichobuni kimeigwa na wenzake.
Mafundi hawa hapa Kidimni siyo matajiri, vifaa wanavyotumia bado ni vya kizamani na hata uwezo wao wa kujilinda kiafya kutokana na uduni wa vitendea kazi ni mdogo. Matokeo yake ni kuwa maisha yao yanategemea wateja wao na uwingi wao wa kuja kuweka oda ya kutengenezewa milango.
0766959349
 
Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.