STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 04 Februari, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein amesema ya ziara ya Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani humu nchini Mheshimiwa Joachim Gauck ni fursa nyingine muhimu ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Zanzibar na Ujerumani.
Akizungumza na Rais huyo wa Ujerumani Ofisi kwake Ikulu leo, Dk. Shein amesema kuwa historia inaonesha kuwa uhusiano kati ya Zanzibar na Ujerumani ulioanza mwaka 1847 ikiwa nchi ya tatu baada ya Marekani na Uingereza kuanzisha mahusiano na Zanzibar.
“tumefurahi ziara yako itaimarisha urafiki na uhusiano wetu kwa kuendelea kushirikiana katika maeneo ambayo tayari tunashirikiana sasa na hata kuanzisha maeneo mengine mapya” Dk. Shein alimueleza Rais Gauck.
Aliongeza kuwa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla zinajivunia uhusiano na ushirikiano mzuri wa kidiplomasia, kiuchumi na kibiashara uliopo kati yake na Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani.
Alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani kwa misaada yake mbali mbali kuunga mkono jitihada za wananchi za kujiletea maendeleo.
“Tunaishukuru serikali na wananchi wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani kwa kuendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada zetu za kujiletea maendeleo na kufanya hivyo sisi tunawaona nyinyi kuwa ni wenzetu na marafiki wa kweli” Dk. Shein alisema.
Alitaja baadhi ya maeneo ambayo Ujerumani inaisaidia Tanzania, Zanzibar ikiwemo kuwa ni pamoja na hifadhi ya mazingira, msaada katika bajeti, nishati na huduma za jamii.
Kwa hivyo Dk. Shein alimueleza Rais wa Ujerumani kuwa Zanzibar na Tanzania kwa jumla zingependa kuona nchi hizo zinashirikiana katika maeneo mapya ya kiuchumi na biashara ikiwemo uwekezaji katika sekta ya utalii.
Katika mazungumzo hayo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alimueleza Rais wa Ujerumani kuwa mafanikio yaliyopatikana hivi sasa Zanzibar yanatokana na wananchi kuishi kwa amani na utulivu huku wakizingatia uvumilivu wa kisiasa na kidini.
“Tumekuwa na ustahamilivu wa kidini Zanzibar kwa karne nyingi na katika historia ya nchi yetu, waumini wa dini zote wamekuwa wakiishi kwa mapenzi makubwa na huku Katiba zetu zote mbili zikimpa kila mwananchi uhuru wa kuabudu dini anayoitaka” Dk. Shein alieleza.
Aliongeza kuwa mwaka 1953 Zanzibar ilitoa stempu maalum ya kuonesha ustahamilivu wa kidini ambayo baadae Dk Shein alimkabidhi mgeni wake nakala ya stampu hiyo.
Dk. Shein alimhakikishia Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani kuwa hivi sasa Zanzibar iko katika utulivu mkubwa na kusifia ushirikiano mzuri uliopo katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliyo katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa.
“Katika miaka mine hii Serikali yetu iliyo chini ya Mfumo wa Umoja wa Kitaifa imekuwa ikifanya vizuri. Tuna ushirikiano ndani ya serikali na si rahisi kufahamu tofauti zetu za kisiasa kwa kuwa lengo letu ni moja la kujenga nchi yetu” alieleza Dk. Shein.
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani Mheshimiwa Joachim Gauck alimueleza Dk. Shein kuwa amefurahi kuona Zanzibar ni nchi yenye kukusanya watu wa tamaduni nyingi pamoja na dini tofauti lakini wamekuweza kuishi kwa amani na mashirikiano makubwa.
Rais huyo alieleza kuwa wananchi wa Ujerumani wanafahamu uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya nchi yao na Zanzibar na kwamba amekuja hapa kuangalia namna nchi hiyo inavyoweza kuimarisha zaidi uhusiano huo.
Mheshimiwa Gauck alisema watu wa Ujerumani wamekuwa wakipata taswira nzuri ya Zanzibar kutokana na watalii wanaotembelea Zanzibar na Tanzania mara kwa mara.
Kuhusu hali ya kisiasa nchini Rais Joachim Gauck alisema “Nimefurahi kuona wananchi wa Tanzania ni watu wanaowasiliana na kujadiliana mambo yao si watu wanaogombana na hilo ni jambo kubwa kwa maendeleo ya demokrasia”.
Alisisitiza kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla ili kuuenzi na kuimarisha uhusiano na ushirikiano huo.
Rais huyo aliwasili leo mchana kwa boti ya Kilimanjaro 4 inayomilikiwa na Kampuni ya Azam Marine na kupokelewa katika bandari ya Malindi Zanzibar na viongozi mbali mbali wakiongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Rais Joachim alipewa heshima zote kwa kupigiwa mizinga, nyimbo za taifa pamoja na kukagua gwaride maalum lililoandaliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania –JWTZ.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822

No comments:
Post a Comment