Habari za Punde

Dkt Bilal Afungua Kongamano la Kitaifa Kuhusu Watoto Walioko katika Mazingira Hatarishi.

HOTUBA YA  MHE. DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL, MAKAMU WA RAIS WA  JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,  KWENYE KONGAMANO LA KITAIFA KUHUSU WATOTO WALIO KATIKA MAZINGIRA HATARISHI, UKUMBI WA MWL. JULIUS NYERERE,
DAR ES SALAAM,  TAREHE 18  FEBRUARI 2015


Mhe. Dkt. Seif Seleman Rashid (Mb)
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii;

Waheshimiwa Mawaziri mliopo;

Mhe. Said Mecky Sadick
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali;

Waheshimiwa Mabalozi wa Nchi mbalimbali;

Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;

Wawakilishi wa Wadau mbalimbali;

Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya;

Waheshimiwa Wakurugenzi wa Halmashauri;
Ndugu Wanahabari;

Ndugu Wananchi;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana.

Awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kutupa uzima na afya njema, na kuweza kukusanyika hapa katika Kongamano hili muhimu. Nitumie nafasi hii pia kukushukuru wewe binafsi Mhe. Dkt. Seif Seleman Rashid, na uongozi mzima wa Wizara wa Afya na Ustawi wa Jamii, kwa heshima kubwa mliyonipa, kunialika kufungua kongamano hili.

Mheshimiwa Waziri;
Shughuli ya leo ni muhimu na imekuja wakati muafaka kwa kuwa Taifa letu bado linakabiliwa na ongezeko la watoto walio katika mazingira hatarishi pamoja na matukio ya ukatili, unyanyasaji, utelekezaji na unyonyaji dhidi ya watoto. Hivyo tuna kila sababu kukaa na kuumiza vichwa, ili kupata namna bora ya kuondokana na matatizo haya katika jamii yetu.

Ndugu Washiriki wa Kongamano;
Mabibi na Mabwana;
Nchi yetu kama zilivyo nchi nyengine za Kusini mwa Jangwa la Sahara imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na janga la UKIMWI, umaskini, migogoro ya kijamii, ukatili na unyanyasaji. Matatizo haya yamesababisha ongezeko kubwa la watoto walio katika mazingira hatarishi kutokana na kudhoofika kwa mifumo ya kijamii ya utoaji huduma katika ngazi ya familia. Taarifa za tafiti na chambuzi mbalimbali zinaonesha kwamba wapo watoto milioni 2.5 ambao ni yatima kutokana na janga la UKIMWI (TDHS 2010). Matokeo ya zoezi la utambuzi wa watoto walio katika mazingira hatarishi uliofanyika katika halmashauri 111, unaonesha kuwa wapo watoto 897,913 wakiwemo wasichana 422,019 na wavulana 475,894 wanaoishi katika mazingira hatarishi (Taarifa ya utambuzi hadi 2013).  

Vile vile Utafiti wa Hali ya Ukatili na Unyanyasaji (VAC 2009) uliofanyika Tanzania, umeonesha kuwa watoto watatu  kati ya 10 wa kike, na mtoto mmoja  kati ya saba  wa kiume, wamefanyiwa ukatili wa kingono kabla hawajafikisha umri wa miaka 18. Utafiti huo umeonesha pia robo ya watoto wote wa kiume na wa kike, wamefanyiwa ukatili wa kimwili kabla ya kufikisha umri wa miaka 18. Takwimu hizi zinatuonesha kwamba watoto wetu hawako katika hali ya usalama jambo linaloathiri makuzi na maendeleo yao na Taifa zima kwa ujumla  kwa sababu watoto ndio Taifa la kesho.

Ndugu Washiriki wa Kongamano;
Mabibi na Mabwana;
Hali ya watoto wetu nchini hairidhishi kwa kuwa watoto walio wengi na hasa wale walio katika mazingira hatarishi wanakumbwa na vidokezo vya hatari katika umri mdogo. Vidokezo hivyo ni pamoja na afya duni, lishe duni, malezi duni ndani ya familia au kaya, watoto kuishi na kufanya kazi mitaani, kukinzana na sheria, vitendo vya ukatili kama vile kubakwa, kupigwa, kutumikishwa nk. Watoto hawa wako katika hatari zaidi ya kuathirika katika makuzi yao kimwili kiakili na kisaikologia jambo ambalo si jema kwa maendeleo na maisha yao ya baadae. Vilevile watoto wengine  wanapoteza maisha na wengine wanapata ulemavu wa kudumu, kwa mfano wale wanokatwa sehemu za viungo vyao kutokana na imani potofu zilizopo katika jamii. Nafarijika sana kuona kwamba mmetambua umuhimu wa kuwashirikisha watoto katika Kongamano hili ili wao wenyewe waweze kuzungumza yale yanayowasibu. Rai yangu ni kwamba, ujumbe utakaowasilishwa na watoto hawa, upewe kipaumbele na mapendekezo yao, yaingizwe katika mikakati ya utekelezaji wa mpango huu.

Ndugu  Washiriki;

Mabibi na Mabwana;
Serikali yenu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imefanya jitihada kubwa katika kukabiliana na hali ya ongezeko la watoto walio katika mazingira hatarishi pamoja na matukio ya ukatili na unyanyasaji wa watoto. Hata hivyo utekelezaji wa jambo lolote haukosi changamoto. Nimearifiwa kwamba zipo changamoto kadhaa zinazokabili utekelezaji wa mradi huu  ambazo ni; Uhaba wa rasilimali, Jamii kutoona umuhimu wa kusaidia malezi, Matunzo na ulinzi kwa watoto walio katika mazingira hatarishi, Kiwango cha umaskini katika ngazi ya familia/kaya, Majanga mbalimbali ukiwemo UKIMWI, Wazazi kutengana na kuvunjika kwa ndoa pamoja na baadhi ya mila na desturi zenye madhara. Yote haya yamesababisha kuwepo ongezeko la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na matukio ya unyanyasaji na ukatili kwa ya watoto.

Ndugu Washiriki;
Mabibi na Mabwana;
Wito wangu katika kukabiliana na changamoto hizi, nawaomba wadau mbalimbali waendelee kushirikiana na kusaidia Serikali katika kuandaa na kutekeleza miradi mbalimbali ya Malezi, Matunzo, Ulinzi na Usalama kwa watoto.  Nitumie nafasi hii pia, kupongeza mashirika na taasisi ambazo kwa njia moja ama nyingine, zimekuwa mstari wa mbele kusaidia miradi mbalimbali ya kuboresha maisha ya watoto wetu. Kipekee, napenda kushukuru mashirika yafuatayo kwa misaada yake mbalimbali ikiwemo ya fedha na utaalamu. Mashirika hayo ni pamoja na; Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Shirika la Kimataifa linaloshughulikia Masuala ya Wanawake (UN Women), Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID), Abbot Fund, Save the Children, Plan International, World Vision, European Union, Catholic Relief Service pamoja na wadau wengine wote ambao wanashirikiana na Serikali katika kutekeleza mipango mbalimbali ya kuwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi tangu mwaka 2000. Napenda pia kuwapongeza Viongozi na watendaji katika halmashauri zote za Tanzania Bara kwa kazi wanayoifanya ya usimamizi na utekelezaji wa Mpango wa Huduma kwa Watoto Walio Katika Mazingira Hatarishi. Hongereni sana, ongezeni bidii, msirudi nyuma. 

Ndugu Washiriki;
Mabibi na Mabwana;
Naamini kwamba tumekusanyika pamoja katika Kongamano hili ili kuweza kutafakari kwa pamoja hali ya watoto walio katika mazingira hatarishi hapa nchini. Hivyo mijadala yenu katika siku tatu hizi ichambue na kuangalia mambo yafuatayo;
1.       Majukumu ya kila mmoja wenu katika kuboresha hali ya
          malezi, matunzo na ulinzi kwa watoto hao,
2.       Hali ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Watoto
          Walio katika Mazingira Hatarishi (2013 – 2017) na namna
          ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza,
3.       Kutumia vyombo vya habari katika kutoa hamasa na
mafunzo kwa umma juu ya umuhimu wa malezi na ulinzi wa watoto,
4.       Kuandaa mikakati endelevu ya kuimarisha upatikanaji wa rasilimali kwa ajili ya huduma kwa watoto walio katika mazingira hatarishi, na
5.       Uimarishaji wa mifumo ya ulinzi na usalama kwa watoto.

Ndugu Washiriki wa Kongamano;
Mabibi na Mabwana;
Kongamano la leo litupe fursa ya kutambua kwamba jukumu la kulea, kutunza na kulinda watoto wetu ni letu sote, hivyo kila mmoja wetu anapaswa kuendelea kutekeleza wajibu huu muhimu kwa kasi zaidi na kuhakikisha kuwa masuala ya watoto hawa, yanapewa kipaumbele na kuingizwa katika mipango ya maendeleo katika ngazi zote. Ni imani yangu kwamba washirika wetu wa maendeleo, watazidi kuunga mkono juhudi zetu za kuboresha maisha ya watoto walio katika mazingira hatarishi. Napenda pia niwakumbushe  viongozi wa wizara mbalimbali kwamba tunao wajibu wa kutekeleza matamko tuliyojiwekea wakati wa Uzinduzi wa Mpango Kazi wa Pili wa kitaifa wa Huduma kwa Watoto Walio katika Mazingira Hatarishi na Uzinduzi wa Matokeo ya Utafiti wa Hali ya Ukatili na Unyanyasaji kwa Watoto nchini.

Ndugu Washiriki wa Kongamano;
Ndugu Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Kwa kuhitimisha hotuba yangu, natoa wito kwa wananchi wote kila mmoja wetu awajibike ipasavyo katika suala zima la kulea na kutunza watoto wetu ipasavyo. Sisi sote tuna jukumu la kuhakikisha kwamba watoto wetu wanaishi katika hali ya usalama na wanalelewa na kukuzwa katika maadili mema.

Baada ya kusema hayo, kwa heshima kubwa na taadhima natamka kwamba;Kongamano la Kitaifa la Watoto Walio Katika Mazingira Hatarishi,  limefunguliwa rasmi.
Nawatakia majadiliano mema. Tuwajibike Kuwalinda Watoto Wetu
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.