Habari za Punde

Rais wa Ujerumani kuwasili Zanzibar kesho

na Othman Khamis Ame, OMPR
 
Rais wa Shirikisho la Ujerumani Bwana Joachim Gauck anatarajiwa kuwasili Zanzibar kesho asubuhi kwa kufanya ziara ya kutwa moja akitokea Mjini Dar es salaamu.
 
Bwana Joachim atapokea na Mwenyeji wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein, Mawaziri wa Serikali, Viongozi wa Kisiasa na baadhi ya raia wa Ujerumani waliopo Zanzibar huko Bandari ya malindi Mjini Zanzibar.
 
Matayarisho ya mapokezi ya ujio wa Kiongozi huyo wa Shirikisho la Ujerumani yamekamilika ambapo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipata wasaa wa kufika Bandari ya Malindi kukagua matayarisho hayo.
 
Mshauri wa Rais wa Zanzibar  anayesimamia Uchumi, Uwekezaji na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Moh’d Ramia Abdiwawa alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba hatua zote zilizopangwa kuchukuliwa katika matayarisho hayo zimetekelezwa kwa mafanikio makubwa.
 
Balozi Ramia alisema Mgeni huyo anatazamiwa kuwasili kwa Boti iendayo kwa Kasi ya Kilimanjaro wakati wa asubuhi na kupata fursa ya kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed  Shein Ikulu Mjini Zanzibar.
 
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Zanzibar Balozi  Silima Kombo Haji alimueleza Balozi Seif kwamba utaratibu maalum umeandaliwa kwa Viongozi  wenyeji waliopangwa kumpokea Kiongozi huyo.

Balozi Silima alisema maafisa wa Itifaki watakuwepo Bandarini hapo kwa lengo la kuwaelekeza Viongozi wote waliopangwa kufika eneo hilo kwa shughuli hiyo muhimu ya Kimataifa.
 
Akitoa shukrani zake  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alielezea kuridhika kwake na hatua za maandalizi hayo na kuipongeza Kamati maalum iliyoundwa ya kuratibu mapokezi hayo.
 
Rais wa Shirikisho la Ujerumani Bwana Joachim Gauck awapo Zanzibar pia anatarajiwa kufanya mazungumzo na Viongozi wa Kidini katika Hoteli ya Serena iliyopo Forodhani Mjini Zanzibar.
 
Bwana Joachim anatazamiwa kuondoka  Zanzibar kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Amani Abeid Karume  Zanzibar wakati wa jioni kuekelea Mkoani Arusha kumalizia ziara yake Nchini Tanzania

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.