STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
10.3.2015
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na
ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na China na kusifu juhudi za nchi
hiyo kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika sekta za maendeleo na uchumi.
Dk. Shein
aliyasema hayo leo huko Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na
Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania Mhe. Lv Youqing aliyefuatana
na ujumbe wake akiwemo Balozi mdogo anayefanyia kazi zake hapa Zanzibar Mhe.
Xie Yunliang.
Katika mazungumzo
hayo, Dk. Shein alisisitiza kuwa Zanzibar inathamini uhusiano huo na
ushirikiano na China ambao umeasisiwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume na
Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na kiongozi wa China wakati
huo Marehemu Mao tse tung.
Dk. Shein alisema
kuwa China inahistoria kubwa katika harakati zake za kuiunga mkono Zanzibar na
ni miongoni mwa nchi za mwanzo zilizoyatambua Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na
kuanzia hapo hadi leo inaendeleakuwa bega kwa bega na Zanzibar.
“Zanzibar na
China ni marafiki wa kweli... uhusiano wa Zanzibar na China ni wa kihistoria na
ulianza mara tu baada ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 ambapo kuanzia
hapo China imeweza kuiunga mkono Zanzibar katika shughuli zake mbali mbali hadi
leo hii.. wananchi wa Zanzibar wanathamini uhusiano huu na watauendeleza’,
alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein
alisema kuwa tokea wakati huo Zanzibar imeweza kupata misaada mbali mbali kutoa
China hatua ambayo imeweza kusaidia mafanikio yake makubwa yaliopatikana hapa
nchini hivi sasa.
Alisema kuwa China
imeweza kuisaidia Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za Maendeleo
zikiwemo afya, elimu, kilimo, michezo na nyenginezo ambapo kwa upande wa sekta
ya afya China imeendelea kutoa madaktari wake na wataalamu kuja kufanya kazi
Zanzibar tokea mwaka 1964.
Kwa upande wa
sekta ya michezo, Dk. Shein aliipongeza China kwa kuiunga mkono Zanzibar katika
kuimarisha miundombinu ya michezo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa uwanja wa Amaan
mjini Unguja sambamba na kusaidia sekta hiyo kwa ujumla.
Kutokana na
mafanikio hayo, Dk. Shein alisema kuwa azma ya China ya kuisaidia Zanzibar
katika ujenzi wa uwanja wa mpira wa Mao tse tung itasaidia kwa kiasi kikubwa
katika kuimarisha sekta ya michezo sambamba na kusaidia shughuli nyengine za
kijamii na kimaedeleo.
Dk. Shein pia,
alimueleza Balozi huyo hatua zinazoendelea za ujenzi wa Hospitali ya Abdalla
Mzee, Mkoani Pemba na kusisitiza kuwa ujenzi huo utsaidia kwa kiasi kikubwa
kuimarisha sekta ya afya na kuimarisha huduma zake.
Pamoja na hayo,
Dk. Shein alieleza hatua za ujenzi wa kiwanda cha Sukari Mahonda pamoja na
viwanda vyengine vidogo vidogo viliojengwa wakati huo ambapo nchi hiyo imeweza
kutoa ushirikiano na msaada mkubwa sambamba na kuendelea kutoa nafasi mbali
mbali za mafunzo nchini humo na kuleta wataalamu wa sekta kadhaa.
Dk. Shein pia,
alitumia fursa hiyo kumuelza Balozi Youqing kuwa miongoni mwa mafanikio makubwa
yaliopatikana Tanzania kutokana China ni pamoja na ujenzi wa Reli ya TAZARA
kati ya Tanzania na Zambia ambayo ni mfano mkubwa kwa nchi za Afrika.
Nae Balozi wa
Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Lv Youqing alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa
mafanikio makubwa yaliopatikana hapa Zanzibar na yanaoendelea kupatikana chini
ya uongozi wa Dk. Shein katika sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo kiuchumi,
kijamii na kisiasa.
Pamoja na hayo,
Balozi huyo alitumia fursa hiyo kumpongeza Dk. Shein kwa mara nyegine tena
pamoja na Serikali anayoiongoza kwa kutimiza miaka 51 ya Mapinduzi Matukufu ya
Januari 12, 1964.
Balozi huyo wa
China alimueleza Dk. Shein kuwa China inathamini sana uhusiano na ushirikiano
wa muda mrefu kati yake na Zanzibar na kuahidi kuuendeleza kwa manufaa ya pande
zote mbili.
Balozi Youqing
alimueleza Dk. Shein kuwa licha ya China kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na
Tanzania kwa jumla katika harakati zake za maendeleo nchi hiyo pia, inathamini sana
juhudi za Tanzania katika kuiunga mkono nchi hiyo kwenye Umoja wa Mataifa.
Aidha, Balozi
huyo aliipongeza Zanzibar kutokana na mafanikio iliyoyapata kwenye sekta ya utalii
huku akiendelea kusifu juhudi za kuendeleza amani na utulivu hapa nchini hatua
ambayo imeendelea kuijengea sifa kubwa Zanzibar duniani kote kutokana na juhudi
zake hizo.
Sambamba na hayo,
Balozi huyo alitumia fursa hiyo kutoa shukurani zake na pongezi kwa Zanzibar
ikiwa ni pamoja na kufikisha salam za Makamu wa Rais wa wa nchi hiyo Mhe. Li
Yuanchao aliyetembelea Zanzibar hapo mwaka jana kutokana na ukarimu mkubwa na
mapokezi aliyoyapata wakati wote alipokuwepo hapa Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment