THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512,
2116898
E-mail: ikulucommpress@googlemail.com
Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S OFFICE,
STATE
HOUSE,
1 BARACK OBAMA ROAD,
11400
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete , Alhamisi, Machi 12, 2015, amefanya
ziara maalum ya kutoa pole kwa wahanga wa mvua iliyoandamana na mawe na
kusababisha upotevu wa maisha ya watu na uharibifu mkubwa wa mali katika vijiji
vitatu vya Kata ya Mwakata, Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga.
Rais Kikwete amewasili mjini Kahama
kiasi cha saa nane mchana baada ya ndege yake kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa
Mgodi wa Buzwagi na kwa muda wa kiasi cha saa tatu ametembelea familia ambazo
zimepata madhara makubwa zaidi kutokana na mvua hiyo iliyonyesha kwa kiasi cha
saa moja tu kuanzia saa nne usiku Machi 3, mwaka huu, 2015 na kuambana na upepo
mkali na mawe.
Watu 47 walipoteza maisha, 112
wakaumia, nyumba 657 zikabomolewa ama kuharibiwa na kaya 468 kuathirika katika
vijiji vitatu vya Kata ya Mwakata na tokea siku ya maafa, Serikali imetoa
huduma za dharura za chakula, sehemu za kulala, huduma za afya na huduma
nyingine muhimu kwa binadamu.
Baada ya kupatiwa maelezo ya kina na
uongozi wa Mkoa wa Shinyanga chini ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Ali
N. Lufunga, Rais Kikwete ameanzia ziara yake katika Kijiji cha Maghuhumwa,
nyumbani kwa Bwana Masemba Maburi, ambaye alipoteza watoto watano katika maafa
hayo. Rais Kikwete ametoa pole kwa wafiwa na kuzungumza na wananchi waliokuwepo
kwenye msiba.
Bwana Maburi ambaye sasa anaishi
katika nyumba ya jirani pamoja na familia yake na familia nyingine tatu
amemweleza Rais Kikwete jinsi nyumba mbili ambako watoto hao na mama yao
walipokuwa wamelala zilivyoanguka na mama huyo akalazimika kukimbilia nje kwa
nia ya kutafuta msaada lakini watoto wakazidiwa na kupoteza maisha.
“Sijawahi kuona mvua kubwa, kali na
yenye upepo mkali kiasi kile katika maisha yangu. Mvua ilianza saa nne usiku na
ikanyesha kwa muda mfupi sana, nyumba zikaanguka ama kubomolewa. Jameni
tusaidie kwa sababu tumekwazika,”Bwana Maburi amemwambia Rais Kikwete.
Baada ya kutoka katika Kijiji cha
Maghuhumwa, Rais Kikwete amekwenda katika Kijiji cha Nhumbi ambako amempa pole
Bwana Zacharia Limbe na familia yake ambayo ilipoteza wajukuu wanne katika
maafa hayo ya mwanzoni mwa mwezi huu.
Akiwa nyumbani kwa Bwana Limbe, Rais
Kikwete ametembea na kujionea makazi mapya ya dharura ya familia ambayo
yamejengwa kwa msaada wa Serikali.
Baada ya kuondoka kwa Bwana Limbe,
Rais Kikwete ametembelea eneo la makazi ya walimu wa Shule ya Msingi ya
Mwakata, ambako walimu hao wamehifadhiwa katika fremu za maduka kutokana na
athari za maafa hayo. Rais Kikwete amewapa pole walimu hao na kuwaambia: “Pole
sana. Tuko pamoja. Tutaendelea kusaidiana kuona jinsi gani mnavyoweza kurejea
katika maeneo yenu ya makazi ya kawaida.”
Rais Kikwete ataondoka kesho, Ijumaa,
Machi 13, 2015, kurejea Dar es Salaam baada ya ziara hiyo maalum ya siku mbili
katika Mkoa wa Shinyanga.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu
– Dar es Salaam .
12 Machi, 2015
No comments:
Post a Comment