Na Mwantanga Ame
TUME ya
Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imesema haina sababu ya kusitisha zoezi la upigaji wa
kura ya maoni juu ya katiba inayopendekezwa.
Mtaalamu wa sheria katika tume hiyo, Khamis
Issa Khamis, aliyasema hayo wakati akitoa ufafanuzi juu ya hoja inayotolewa na
baadhi ya wanasheria kwamba Zanzibar haitaweza kupiga kura ya maoni kwa vile
sheria iliyotumika kuunda Bunge la Katiba, haikuridhiwa na Baraza la
Wawakilishi.
Alisema madai hayo hayana ukweli, kwa vile
kifungu cha 64 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,
imeeleza wazi masharti yanayoipa haki Zanzibar ya kuendesha zoezi hilo.
Alisema ni kweli wamezisikia hoja zinazotolewa
na baadhi ya wanasheria hao, lakini bado kinachoonekana wameshindwa kuiangalia
vizuri katiba hiyo.
Akifafanua kauli yake hiyo, alisema kwa mujibu
wa kifungu cha 64, kinachosimamia madaraka ya kutunga sheria, kifungu kidogo
cha (1) kimeeleza kwamba mamlaka yote ya kutunga sheria juu ya mambo mengine
yote yanayohusuyoTanzania Bara, yatakuwa mikononi mwa Bunge, huku kifungu
kidogo cha (2), kikieleza kuwa Mamlaka yoyote ya kutunga sheria katika Tanzania
Zanzibar, juu ya mambo yote yasio ya Muungano yatakuwa mikononi mwa Baraza la
Wawakilishi.
Alisema, katika kifungu kidogo cha (3),
kinafahamisha endapo sheria yoyote iliyotungwana Baraza la Wawakilishi, inahusu
jambo lolote katika Tanzania Zanzibar, ambalo liko chini ya mamlaka ya bunge
sheria hiyo itakuwa ni batili, na itatambulika na pia endapo sheria yoyote
iliyotungwa na Bunge inahusu jambo lolote ambalo liko chini ya Mamlaka ya
Baraza la Wawakilishi, sheria hiyo itakuwa ni batili na itatenguka.
Mwanasheria huyo, pia alisema katika suala hilo
bado kifungu kidogo cha 64 (4) kinaeleza kuwa, sheria yoyote iliyotungwa na
Bunge kuhusu jambo lolote, haitatumika Tanzania Zanzibar, ila kwa mujibu wa masharti
yalioainishwa ndani ya Katiba hiyo.
Akitaja masharti hayo, alisema, katika kifungu
kidogo cha (4) kipengele (a), kinaeleza sheria hiyo iwe imetamka wazi kwamba
itatumika Tanzania bara na vile vile Tanzania Zanzibar, au iwe inabadilisha,
kurekebisha, au kufuta sheria inayotoka Tanzania Zanzibar.
Kifungu (b), alieleza mtaalamu huyo, alisema,
kinaeleza kuwa sheria hiyo, iwe inabadilisha au kurekebisha au kufuta sheria
iliyokuwa inatumika tangu zamani Tanzania Bara, ambayo pia ilikuwa inatumika
pia Tanzania Zanzibar, kwa mujibu wa mapatano ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar, ya mwaka 1964 au kwa mujibu wa sheria yoyote ambayo ilitamka wazi
kwamba itatumika Tanzania Bara na vile vile Tanzania Zanzibar.
Aidha, haki hiyo, alisema pia imeoneshwa katika
kifungu kidogo cha © ndani ya katiba hiyo, kinachoeleza kwamba sheria hiyo iwe
inahusu mambo ya Muungano na kila inapotajwa Tanzania katika sheria yoyote
ifahamike kuwa sheria hiyo itatumika katika Jamhuri ya Muungano kwa mujimu wa
ufafanuzi uliotolewa na ibara hiyo.
Alisema kura ya maoni itafanyika kama
ilivyopangwa na hawaoni sababu ya kuahirisha zoezi hilo, kwa vile bado hakujawa
na sababu za msingi.
Akizungumzia juu ya suala la asasi za kiraia
ambazo zinatarajiwa kushiriki katika uchaguzi huo, alisema hadi sasa kwa upande
wa Zanzibar zilizoomba ni 135 huku kwa upande wa Tanzania Bara zimefikia asasi 375.

No comments:
Post a Comment