Habari za Punde

Hamad aonya baadhi ya makundi kutengwa

Na Abdi Shamnah
MLEZI wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Hamad Rashid Mohammed, amesema vita vya kidemokrasia vinavyoendelea kote duniani, vinatokana na baadhi ya watu, taasisi au makundi ya kijamii kukosa fursa ya kushirikishwa katika mabaraza ya kutunga sheria au katiba za nchi zao.

Alisema hali hiyo huwalazimisha wananchi kudai haki bila ya kuzingatia sheria na kupelekea kuibuka vurugu kubwa, maandamano na hatimae mauaji.

Alisema hayo katika hoteli ya Bwawani, wakati akichambua mada ya amani na utulivu katika kampeni za upigaji kura wa katiba inayopendekezwa, pamoja na uchaguzi mkuu,katika kongamano lililoandaliwa na Kamati ya Amani na Utulivu inayoundwa na wajumbe kutoka dini tofauti.

Kongamano hilo liliwashirikisha viongozi wa dini, wanasheria, walimu wa madrasa, masheha na baadhi ya wajumbe wa lililokuwa bunge la katiba waliopo Zanzibar.


Hamad, ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Wawi, alisema hali hiyo inapokuwa kinyume chake kwa jamii husika kupewa fursa na kukataa kushiriki katika vikao halali vya maamuzi, basi malalamiko yoyote yatakayotolewa  baadae huwa hayana msingi wowote.

Nae Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Thabit Norman Jongo, akizungumzia mada  hiyo alisema, imekuwa ni kawaida kila nchi inapokabiliwa na jambo kubwa na muhimu, hutokea migongano na kupelekea uvunjifu wa amani.

Alisema nchi imeamua kuwepo kura ya maoni, huku baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wakiwashawishi wanachama wao kususia kupiga kura hiyo.

Alisema maamuzi ya baadhi ya viongozi katika majukwaa ya kisiasa yanaweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani,hivyo kusisistiza haja ya wananchi wenyewe kuwa na uhuru katika kufikia maamuzi ya mwisho katika mambo makubwa au  mustakbali wa maendeleo ya nchi yao.

“Huwezi kumtawala binaadamu kwa nguvu, unapaswa kutumia hekima, busara na maneno mazuri,vinginevyo kauli hizo hatimae zitawahamasisha unaowashawishi kuchukua silaha,” alisema.

Aidha alisema baadhi ya wanasiasa huwatumia vibaya viongozi wa dini ili kupandikiza chuki miongoni mwa wananchi na serikali yao pamoja na kutumia kasoro mbali mbali zilizopo nchini, ikiwemo suala la ajira ili kuibua vurugu.

Aliwataka viongozi walioshiriki katika kongamano hilo kuwaelimisha watu  walio karibu nao, umuhimu wa kuisoma katiba inayopendekezwa.

Nae Katibu wa Kamati hiyo, Father Damas Mfoyi, alisema wajumbe hao ni watu walio karibu zaidi na jamii, hivyo aliwataka kutumia ushawishi na kila aina ya hekima kuwafikia wananchi na kuwapa elimu hiyo, ili hatimae taifa liweze kupata katiba ilio bora.

Mapema Mkuu wa wilaya ya magharibi, Ayoub Mohammed, akimuwakilisha Mkuu wa mkoa wa mjini magharibi, alisema wakati serikali ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya matayarisho ya katiba inayopendekezwa kuna watu kwa makusudi wana malengo ya kuipotosha.

Aliwataka washiriki kuifahamu vilivyo katiba inayopendekezwa na kuwa mabalozi kwa wenzao ili pale watakapotokezea  wale wenye dhamira ya kuipotosha, watu hao wawe tayari wameshaelimika.

Wakichangia katika kongamano hilo, baadhi ya washiriki walisema kumekuwa na juhudi za makusudi zinazofanywa na baadhi ya watu wasioitakia mema nchi, kwa kupotosha ibara mbali mbali zilizomo katika  katiba hiyo.


Miongoni mwa Ibara zilizotajwa mara kadhaa kuwa zimekuwa  zikipotoshwa kwa makusudi ili kuwatia hofu na uchungu Wazanzibari  ni pamoja na ile ya 23 (1) na (2) na 24,26 na 27 kuhusu ardhi, maliasili na mazingira.    

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.