Habari za Punde

Juwaza yastushwa na idadi ya wazee wasio na mafao wanaoishi maisha ya kubahatisha

Na Haji Nassor, PEMBA
JUMUIA ya wastaafu na wazee Zanzibar JUWAZA, imesema inaendelea kuwapigania wazee  48,511 wa Zanzibar, ili serikali iwawezesha katika nyanja mbali mbali, ikiwa ni pamoja na kupatiwa fedha za kujikimu katika maisha yao.
JUWAZA imesema idadi ya wazee wote wa Zanzibar kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, ni 58,311 sawa na asilimia 4.5 ya idadi wa wananchi wote wa Zanzibar milioni 1, 303,569  ambapo kati ya idadi hiyo ya wazee, ni wazee 7,800 pekee ndio wanapata mafao yao kupitia wizara ya fedha na mfuko wa hifadhi wa jamii Zanzibar ZSSF.
Msaidizi Katibu wa JUWAZA Yussuf Nuh Pandu, alieleza hayo jana ukumbi wa mikutano wa Chuo cha mafunzo ya Amali Vitongoji Chake chake Pemba, wakati akizungumza na maofisa wa wilaya nne za Pemba.
Alisema kundi kubwa la wazee bado wanaishi kwenye mazingira magumu, na ndio maana JUWAZA, imekuwa ikiendelea kutetea haki za wazee wote, ili wapate mafao hata kama hawakuwa waajiriwa ili waishi sawa na wengine.
Alieleza kuwa jumuia hiyo, bado haijaridhishwa kuona ipo idadi ya wazee zaidi ya 48,000 ambao wanaendelea kuishi maisha ya kubahatisha.
“Lazima sisis kama JUWAZA, tutaiendelea kuiomba serikali wazee wote wa Zanzibar kuanzia miaka 70 na kuendelea wapewe fedha kila mwisho wa mwezi kama walivyowengine’’,alisema.
Katika hatua nyengine Msaidizi Katibu huyo alisema tokea kuanzishwa kwake mwaka 2001, JUWAZA mambo kadhaa yameshafanywa ikiwa ni pamoja na kutetea haki za wazee hadi kwenye Katiba inayopendekezwa.  
Akifungua mafunzo hayo ya siku mbili, Afisa Mdhamini wizara ya nchi, ofisi ya rais Ikulu na utawala bora Pemba, Jokha Khamis Makame, alisema bado juhudi zinahitaji ili kuwaokoa wazee na hali ngumu ya maisha.
Alisema kama JUWAZA haitoshirikiana vyema na Idara ya hifadhi ya jamii, basi suala la umaskini na kukosa uhakika wa maisha kwa kundi la wazee linaweza kuwa kudumu.
“Taarifa za utafiti wa mapato na matumizi ya kaya wa mwaka 2010 umeonyesha kuwa asilimia 11.4 ya kaya zinazoongozwa na wazee wenye umri wa miaka 65 na kuendelea, ambapo hapo hata umaskini unaweza kujitokeza’’,alifafanua.
Katika hatua nyengine Afisa mdhamini huyo alisema, dhana ya uhifadhi wa jamii inaonekana kama mpya kwa wadau wa karne hii, ingawa imeanza kufanya kazi tokea mwaka 1964.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, walisema kama kuna taarifa ya kila mzee wa mzanzibar kuweza kupatiwa wastani wa shilingi 20,000 kwa aliefikia umri wa miaka 70, ni vyema suala la umri likangaliwa upya.
Afisa Mipango wilaya ya Wete Omar Hamad Small alisema umri wa miaka 70 kwa wananchi wa Zanzibar kundi kubwa huwa halifikiwa, hivyo ni vyema ukapunguzwa hapo badae.
JUWAZA ambayo imeanzishwa mwaka 2001 ambapo inamakao makuu yake ZSSF Unguja, inaendesha mradi wa miaka mitatu wa program kuhusu namna ya kupanga na kutekeleza uhifadhi wa jamii Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.