Habari za Punde

Maandalizi sherehe za miaka 51 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yakamilika

 Mkuu wa Wilaya ya Temeke Bi. Sophia Mjema akizungumza na waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam. Maadhimisho ya mwaka huu yatapambwa na Kauli Mbiu isemayo Miaka 51 ya Muungano, Tudumishe Amani Na Umoja ,Ipigie Kura ya Ndiyo Katiba inayopendekezwa na Kushiriki Uchaguzi Mkuu.

 Askari watakaoshiriki kwenye Gwaride la heshima litakalohusisha vyombo vya ulinzi na usalama wakati wa maadhimisho ya miaka 51 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wakiwa wamebeba bendera za Majeshi ya Tanzania ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mwisho ya sherehe hizo uwanja wa Uhuru leo jijini Dar es salaam.

 Askari wa Kikosi Maalum cha Jeshi la Maji wakipita mbele ya jukwaa kuu la uwanja wa Uhuru kwa mwendo wa kasi ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya sherehe za miaka 51 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar leo jijini Dar es salaam. 
Askari wa Kikosi Maalumu cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (Komando) wakipita mbele ya jukwaa kuu la uwanja wa Uhuru kwa mwendo wa kasi ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya sherehe za miaka 51 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. 

Na. Aron Msigwa - Dar es salaam.

Serikali imesema kuwa maandalizi ya Sherehe za Miaka 51 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar  yamekamilika na kwamba sherehe hizo zitafanyika  katika uwanja wa Uhuru Aprili 26 mwaka huu.

Akitoa ufafanuzi kuhusu kukamilika kwa maandalizi  ya sherehe hizo kwa niaba Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam leo, Mkuu wa Wilaya ya Temeke Bi. Sophia Mjema  amesema maadhimisho ya mwaka huu yatapambwa na Kauli Mbiu isemayo Miaka 51 ya Muungano, Tudumishe Amani Na Umoja ,Ipigie Kura ya Ndiyo Katiba inayopendekezwa na Kushiriki Uchaguzi Mkuu.

Amesema Tanzania katika kipindi cha miaka 51 ya Muungano imepata mafanikio makubwa katika Nyanja mbalimbali za maendeleo ya jamii, uchumi, Siasa,Ulinzi, Usalama na Uhusiano wa Kimataifa.


 Bi. Mjema amefafanua kuwa maadhimisho hayo yataongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete ambaye atakuwa mgeni rasmi na kupambwa na michezo ya Halaiki, ngoma za asili, vikundi vya burudani  na  Gwaride la heshima litakalohusisha vyombo vya ulinzi na usalama.

Pia yatapambwa na Wimbo maalum utakaoimbwa na vijana wa halaiki na ndege vita za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) zitakazopita mbele ya mgeni rasmi Kama sehemu ya shamrashamra ya sherehe hizo.

Ametoa wito kwa wananchi wajitokeze kwa wingi kuhudhuria maadhimisho hayo na kufafanua kuwa milango ya uwanja wa Uhuru itakuwa wazi kuanzia saa 12:30 asubuhi ili kuwawezesha wananchi kuingia kushuhudia sherehe hizo.

Aidha, ameutaka uongozi wa SUMATRA na wamiliki wa vyombo vya usafiri (Daladala) kuelekeza magari yao ya abiria kwenda uwanja wa Uhuru ili kurahisisha huduma ya usafiri kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.