Habari za Punde

Rais wa Zanzibar Dk Shein Ahudhuria Hitma ya Mzee Karume Afisi Kuu ya CCM Zanzibar.

  
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                                                                           7.4.2015
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein leo ameongoza hitma ya kumuombea dua Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu mzee Abeid Amani Karume, iliyofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini Zanzibar.

Hitma hiyo, ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Kharib Bilal, Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Sita, Mhe. Amani Abeid Karume, Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.

Viongozi wengine walihudhuria katika hitma hiyo ni  Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabhi, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, Sheikh wa Mkoa wa Dar-es- Salam Sheikh Mussa Salum na viongozi wengineo.

Wengine ni viongozi wa serikali zote mbili na viongozi wastaafu, viongozi wa vyama vya siasa, Masheikh kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, Wabunge na Wawakilishi, wananchi kutoka sehemu mbali mbali pamoja na Mabalozi wadogo waliopo hapa Zanzibar.

Hitma hiyo ya kumuombea dua Marehemu Mzee Abeid Amani Karume pia ni miongoni mwa maadhimisho ya Siku ya Mashujaa ilitanguliwa na Qur-an tukufu, iliyosomwa na Ustadh Sharif Muhidin na kuongozwa na Sheikh Jafar kutoka Masjid Noor Mohammad,iliopo Kwa Mchina Mwanzo.

Mara baada ya hitma hiyo, Sheikh Mkoa wa Dar-es-Salaam, Sheikh Mussa Salum alitoa mawaidha na kumuelezea marehemu mzee Abeid Amani Karume kuwa ni kiongozi aliyepigania maendeleo ya wananchi wa Zanzibar na kumuombea MwenyeziMungu ampe makaazi mema Peponi.

Akieleza kuhuhu umuhimu wa siku hii, Sheikh Mussa alisema kuwa siku ya leo ni muhimu sana kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kwa lengo la kumuombea dua Marehemu Karume pamoja na mashujaa wengine.

Aidha, Sheikh Mussa alitumia fursa hiyo kukumbusha juu ya umauti na kusisitiza kuwa ni  jambo ambalo litafika kwa kila kiumbe alichokiumba MwenyeziMungu na kusisitiza kuwa ni vizuri mwanaadamu akakumbuka asili yake na hatma yake.

“Kifo ni onyo, kifo ni mawaidha na kifo ni mazingatio...kutokana na hali hiyo kuna kila sababu ya kutenda mema, kuwa na mahaba, kuwa na udugu wa kiimani.. huku tukiendelea kumuombea dua mzee wetu huyu kwani yeye ameonja umauti kama ilivyoeleza Qur-an ikiwa na maana kuwa roho yake bado iko hai” alisema Sheikh Mussa.

Pamoja na hayo, Sheikh Mussa katika kutilia mkazo suala zima la udugu wa kiimani alitoa pongezi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuendelea kusimamia Serikali ya Mapindui ya Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa ambayo imewafanya Wazanzibari kuimarisha udugu wao na kuwa kitu kimoja kama Uislamu unavyotaka.

Alisema kuwa hatua hiyo imezidisha umoja sambamba na kuimarisha amani na utulivu uliopo na kuifanya Zanzibar kuwa tulivu na kusisitiza kuwa huo ndio udugu wa kiimani.

Baada ya kisomo hicho cha hitma ambacho hufanyika kila mwaka inapofika tarehe 7, Aprili, viongozi hao na wananchi waliohudhuria katika hitma hiyo walimuombea dua, marehemu mzee Abeid Karume katika kaburi lake lililopo pembezoni mwa afisi hiyo ya CCM Kisiwandui dua iliyoongozwa na viongozi wa dini tofauti akiwemo Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Omar Kabhi, Askofu Michael Hafidh kutoka Kanisa la Anglikana Zanzibar na Bhaguan Suria (Mshamba) aliyesoma kwa niaba ya Wahindu.

Viongozi na wanafamilia waliweka mashada ya maua katika kaburi la marehemu mzee Abeid Amani Karume akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Mohammed Kharib Bilal, Mzee Hamid Ameir aliyeweka shada la maua akiwakilisha wazee walioshiriki Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Tanzania Luteni Jeneral S.A. Ndomba, Balozi Ali Karume aliyewakilisha familia ya Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume na Balozi mdogo wa China anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Mhe. Xie Yualing aliyewawakilisha Mabalozi wenzake wa hapa nchini.

Aidha, Mama Mwanamwema Shein aliungana na akina mama wengine katika hitma hiyo katika Afisi hiyo ya CCM Kisiwandui, akiwemo mjane wa marehemu mzee Abeid Karume, Mama Fatma Karume, Mama Asha Bilali,Mama Zakia Bilal, Mama Asha Balozi na Mama Pili Balozi, Mama Shadya Karume na viongozi wengine wanawake wa kitaifa wakiwemo Mawaziri, Wabunge, Wawakilishini na wananchi kutoka sehemu mbali mbali ya Zanzibar na Tanzania Bara.

April 7, 1972 ndiyo siku aliyouawa Rais wa Kwanza wa Zanzibar marehemu Mzee Abeid Amani Karume na wapinga maendeleo nchini ambapo hivi leo imetimia miaka 43 tokea utokee msiba huo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.