Habari za Punde

Raza atoa msaada wa vifaa vya michezo kwa timu ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais

 Mwanamichezo Maarufu Nchini ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Moh’d Raza Hassanali aliyesimama akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kabla ya kukabidhi vifaa vya michezo kwa Timu ya Soka ya Ofisi ya Makamu wa Pili.

Wa kwanza kulia ni Katiobu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Khalid Salum Moh’d,  wa mwanzo  kushoto ni  Mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya Tumu ya Ofisi ya Makamu wa Pili Tajo Hassan na Mwenyekiti wa Timu Haroub Gharib Bilal.

 Mwanamichezo Maarufu Moh’d Raza akimkabidhi seti ya Jezi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
 Balozi Seif wa Pili kutoka kulia akimpongeza Mwanamichezo Moh’d Raza kwa juhudi za Uongozi wa Kampuni yake ya Hassan and Son’s za kusaidia sekta ya michezo hapa nchini.

Na Othman Khamis Ame, OMPR

Mwanamichezo Maarufu Nchini ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Moh’d Raza Hassanali alisema Kampuni yake ya Hassan and Son’s  inakusudia kuanzisha mpango maalum wa kuzisaidia timu za Maskuli Unguja na Pemba ili ile ari na vugu vugu la michezo lirejee kama zamani.

Raza alisema hayo wakati wa hafla fupi ya kumkabidhi Seti za jezi, soksi na mipira Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa ajili ya Timu ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Hafla hiyo fupi iliyofanyika Ofisini kwa Balozi Seif Vuga Mjini Zanzibar pia ilihudhuriwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Khalid Salum Moh’d pamoja  na  Viongozi wa Timu ya Wizara hiyo.


Raza alisema wakati umefika kwa washirika wa michezo Nchini kuunga mkono mpango huo wa kurejesha mashindano ya mara kwa mara katika maskuli ya Zanzibar kwa lengo la kuwaandaa vijana kuwa na timu imara zitakazokuwa na uwezo wa Kimataifa.

Akipokea msaada huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alimpongeza Mwanamichezo huyo Maarufu wa Zanzibar Moh’d Raza kwa jitihada zake za kuunga mkono sekta ya Michezo hapa Nchini.

Alisema kitendo cha Mwanamichezo huyo ni miongoni mwa uzalendo aliouonyesha ambao unastahiki kuigwa na washirika pamoja na wanamichezo wengine.

Balozi Seif alisema juhudi za Mwanamichezo huyo zilipelekea kuteuliwa kuwa mshauri wa Rais anayesimamia michezo pamoja na kuwa Mwenyekiti wa Saidia Zanzibar Ishinde { SAZI } katika awamu zilizopita.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambalo limo ndani ya Ilani ya chama cha Mapinduzi ni kukuza  michezo hapa Nchini.

Alishauri Taasisi zinazosimamia michezo Nchini  kwa kushirikiana na Ofisi yake ziandae utaratibu wa kuanzisha Ligi Maalum za Mawizara ya Serikali na tayari Mwanamichezo Moh’d Raza ameonyesha nia shauku ya kuzisaidia Timu hizo kwa kuzipatia vifaa endapo ligi hiyo itaasisiwa rasmi.


2 comments:

  1. Wafanyabiashara jamani hebu kuweni serious zaidi. Hebu unganeni kidhati khasa mutusaidie sisi wanyonge Wa mungu. Hebu fanyeni kitu kama alichofanya Salim Turky. Haya mambo ya kusaidia udoho udoho Mara mtu kasaidia soksi mara utamuona jimboni kasaidia jezi. Haya mambo muhimu lakini sio mambo ya msingi sana kwa maisha duni ya wazanzibari. Leo hii ukiwa na mgonjwa maradhi yake huongezeka mara mbili akifikiri wapi atayapeleka. Zanzibar sekta ya afya taaban wananchi wengi tumekata Tamaa kabisa. Wekezeni kwenye sekta za Afya na Allah atakupeni kila la kheri duniani name akhera. Amiin.

    ReplyDelete
  2. Maneno yako ni kweli ndugu yangu lkn. uwekezaji ktk sula la afya sio mchezo lina changamoto nyingi ; ukitoa majengo,

    kuna suala la madaktari bingwa, ambao kwetu hapa ni wachache na wale wa Bara huwezi kuwaleta hapa hata kwa malipo gani kutokana na wingi wa kazi walizonazo!

    Pili ni vifaa tiba, bei zake na matengenezo pale vinapoharibika na

    Tatu ni ukosefu wa umeme mbadala, pindipo ule wa 'gridi ya taifa' unapokatika!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.