Habari za Punde

Dk Shein: Moyo wa Kujitolea Umeiwezesha CCM Kutekeleza Malengo yake Inayojiwekea.

STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                             02 Mei, 2015
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewapongeza wanachama na wapenzi wa Chama cha Mapinduzi kwa moyo wao wa kujitolea ambao daima umekiwezesha chama hicho kutekeleza malengo yake iliyojiwekea.
Akizungumza katika harambee ya kuchangia chama hicho Mkoa wa Magharibi –kichama iliyofanyika katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort mjini Unguja jana, Dk. Shein alisema amefurahishwa na ari na moyo waliokuwa nao washiriki wa harambee hiyo ambapo ilikiwezesha chama hicho kukusanya jumla ya shilingi milioni 644.54.
 Aliipongeza Kamati ya Maandalizi ya Harambee hiyo pamoja na viongozi wa Chama hicho mkoa sio tu kwa maandalizi mazuri lakini pia kwa wao wenyewe kujiwekea utaratibu wa kuchangia harambee hiyo jambo ambalo limewahamasisha wachangiaji wengine.
Dk. Shein aliwashukuru wageni mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo wakiwemo wanachama na wapenzi wa CCM pamoja na wafanyabiashara mbalimbali wa hapa Zanzibar na Tanzania Bara.
Aliwaeleza wana CCM na wageni waliohudhuria hafla hiyo kuwa alikuwa na hakika wakati alipotoa rai kwa viongozi wa CCM tarehe 24 Aprili, 2013 kufanya harambee kuchangia maendeleo ya chama hicho kuwa  zoezi hilo litafanikiwa.
Hadi sasa mikoa iliyokwishafanya harambee hizo ni mikoa ya yote ya kichama ya Unguja ambayo ni Kaskazini, Kusini, Mjini na Mkoa wa Magharibi.
Kati ya fedha zilizokusanywa, shilingi 120.7 zilikuwa fedha taslim, milioni 490.8 ahadi na hundi ilikuwa shilingi milioni 33.
Dk. Shein alichangia shilingi milioni 15 wakati Mke wake Mama Mwanamwema Shein alichangia shilingi milioni 5.
Miongoni mwa wachangiaji walikuwa ni pamoja na Waziri Mkuu wa zamani Mheshimiwa Edward Lowasa milioni 50, Kampuni ya Simon Group shilingi milioni 30, Kampuni ya ujenzi ya MECCO shilingi milioni 20 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mheshimiwa Benard Membe milioni 10.
 Katika harambee hiyo marafiki wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda waliahidi mchango wa shilingi milioni 203 wakati yeye mwenywe alichangia shilingi milioni 10.
 Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu Pinda alisema ari iliyooneshwa katika harambee hiyo inadhihirisha msemo wa ‘kutoa ni moyo si utajiri’.
 Alisifu ari ya washiriki wa hafla hiyo na kueleza kuwa ilikuwa ya hali ya juu na yeye binafsi ametiwa moyo sana na kitendo hicho cha wana CCM katika harambee hiyo.
 Katika hafla hiyo vitu mbalimbali vya asili pamoja na picha za kumbukumbu za kitaifa zilinadiwa na kununuliwa kwa fedha nyingi ikiwemo picha ya kuchora ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Shein ambayo ilinunuliwa kwa shilingi milioni 23.
 Kitu kingine kilichovutia katika mnada ni keki yenye rangi ya Chama cha Mapinduzi ambayo mnada wake ulishamirishwa na Mke wa Rais Mama Mwanamwema Shein na hatimae kununuliwa kwa shilingi milioni12.
  


Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.