Na Zuhura Juma, PEMBA
WANANCHI kisiwani Pemba wametakiwa kuisoma na kuielewa kwa kina katiba iliyopendekezwa, ili kuweza kutoa maamuzi sahihi wakati ukifika wa kuipigia kura ya maoni katiba hiyo.
Hayo yalielezwa jana na Naibu Mrajis wa Mahakama, Mhe.Haji Omar Haji ‘Sumbu’ wakati alipokuwa akifungua mkutano wa siku mbili wa kupitia katiba inayopendekezwa, katika ukumbi wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzinbar Z.L.S.C Chake Chake Pemba.
Alisema kuwa kuisoma na kuielewa malengo yake katiba inayopendekezwa,ni jambo la muhimu kwa wananchi, ili kuweza kujua kile ambacho wanakwenda kukipigia kura ya ndio hapana wakati utakapofika.
Alifahamisha kuwa, suala la kuikataa na kuikubali katiba hiyo pendekezwa litakuwa halina msingi wowote kwa wananchi pindi ikiwa kundi hilo la watu hawajaisoma kwa kina na kuifahamu.
“Watu wanajadili tu bila ya kujua, hebu isomeni muifahamu na muwafundishe na wengine, ili ifikapo muda wa kuipigia kura mujue nini munakwenda kukipigia kura”, alifahamisha Naibu Mrajis.
Kwa upande wake Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC, tawi la Pemba, Fatma Khamis Hemed, alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kujenga na kuimarisha uelewa kwa wananchi, ya kile kilichomo ndani ya katiba iliyopendekezwa.
“Sisi lengo letu ni kupata uelewa wa kile kilichomo ndani ya katiba hii inayopendekezwa, sio suala la kutoa tamko la ipi katiba bora, ipi ya isio ya wananchi”, alieleza Mratibu huyo.
Hata hivyo amesema mafunzo ya aina hiyo yatakuwa endelevu na wananchi wa makundi mbali mbali watapa uwelewa baada ya kituo hicho kupata ruhusa rasmi ya kutoa elimu ya katiba inayopendekezwa.
Akitoa ufafanuzi wa katiba inayopendekezwa Naibu Mwenyekiti wa mahakama ya Ardhi, Salum Hassan Bakar alisema iwapo wananchi wataziangalia Ibara mbali mbali na kuzisoma kwa umakini, uhakika wao wa kupiga kura ya ndio au hapana itakuwa na maana.
“Kwa mfano Ibara ya 26 kwenye katiba hii pendekezwa imetaja kwamba maliasili zote za taifa ikiwa ni pamoja na madini, gesi na mafuta ni mali ya umma za serikali zote mbili zitaweka utaratibu wa matumizi ya sasa na vizazi vijanvyo’’, alisema.
Wakichangia mada ya ufafanuzi wa katiba hiyo pendekezwa, walisema ni vyema kila mmoja kuisoma kwa kina Ibara kwa ibara ili maamuzi yoyote watakayoyatoa yawe sahihi.
Mmoja wa washiriki hao Abdullakarim Mussa Said, alisema ni vyema kabla ya wananchi kuelekea kwenye vituo vya kupigia kura katiba hiyo, iwe tayari wameshaielewa kwa kina.
Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoandaliwa na kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC, yalikuwa na lengo la kuwaelewesha wananchi wakiwemo viongoziu wa dini na kijamii, kilichomo ndani ya katiba inayopendekezwa na kuweza kutoa maamuzi yaliyo sahihi wakati wakuipigia kura katiba hiyo.
No comments:
Post a Comment