Habari za Punde

Vyama vyaigomea Zec kusaini mkataba maadili ya uchaguzi.

Na Rahma Suleiman

Wadau wa vyama vya siasa  Zanzibar, wamegoma kusaini mkataba wa maadili ya uchaguzi kati yao na Tume ya  Uchaguzi Zanzibar (Zec).
Uamuzi huo umekuja baada  ya Zec kuwaomba wadau hao kusaini mkataba ili wakubaliane kwa pamoja masuala muhimu ya kuzingatiwa katika uchaguzi mkuu.
Wakichangia mjadala huo, baadhi ya wadau walisema hawawezi kusaini hadi serikali, Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) nao waingizwe kwenye makubaliano hayo. 
Walisema chaguzi nyingi zimekuwa zikiingiliwa na vyombo vya usalama, jambo ambalo kila mhusika anatakiwa awajibike ipasavyo kwa nafasi yake katika uchaguzi na kufahamu mipaka ya kila mmoja.
Akijibu hoja hizo, Kamishna wa Zec, Zanzibar, Nassor Khamis Mohammed, alisema lengo na madhumuni makubwa ya kusaini mkataba huo ni kutaka kuona uchaguzi mkuu unaendeshwa katika misingi ya amani na utulivu.

“Hakuna sababu ya kulumbana, bali ukubaliane kwa pamoja ili mkataba  huu ukubaliwe na wadau ambao ndio nyinyi na kusainiwa kwa mujibu wa utaratibu,” alisema kamishna huyo ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili.
Hata hivyo, alikubaliana na hoja ya wajumbe na kupanga tena kukutana kwa ajili ya kusaini.
Mtaalam Mkuu wa masuala ya  uchaguzi kutoka Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Hamida Kibwana, alitoa angalizo kwa wadau hao kuwa makini na hoja zao za kutaka kuingiza vyombo vya usalama katika mkataba huo.
Alisema hajawahi kuona katika makubaliano ya kusaini mkataba wa maadili ya uchaguzi unahusisha vyombo vya usalama katika uzoefu wake wa uchaguzi na kuwa wakiamua hivyo, wawe waangalifu sana.
Mkutano huo wa wadau wa Vyama vya siasa  na Tume ya  uchaguzi Zanzibar  uliahirishwa hadi Julai 16, mwaka huu ili kusaini mkataba wa maadili ya uchaguzi kama Zec itakuwa  imeshirikisha  vyombo vya usalama  mchakato huo.
Mkutano huo ilivishirikisha vyama 21 vya siasa vikiwamo TLP, UDP, UMD, UPDP, NLD, NCCR-Mageuzi, Jahazi Asilia, DP, Demokrasia Makini na CUF.
Vingine ni ACT – Wazalendo, ADC, AFP, APPT Maendeleo, CCK,  CCM, NRA, Sau, Tadea, Chadema, Chauma na Chausta.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.