MAAZIMIO YA
MKUTANO WA AMANI ZANZIBAR ULIOFANYIKA KUANZIA TAREHE 19 HADI 20 SEPTEMBA 2015
KATIKA HOTELI YA ZANZIBAR BEACH RESORT –ZANZIBAR
Bismillahir Rahmaanir Rahym
1.
Ofisi ya Mufti
kwa kushirikiana na Friends of Zanzibar, ziandae utaratibu kuhakikisha mafunzo
ya Mkutano huu yanafika katika wilaya zote za Unguja na Pemba.
2.
Ofisi ya Mufti
ichukue jukumu la kuyawasilisha Maazimio ya Mkutano huu kwa Viongozi Wakuu wa
Serikali ya Umoja wa Kitaifa pamoja na Taasisi nyengine zote muhimu katika
kutunza amani nchini.
3.
Tume ya
Uchaguzi Zanzibar, iwajibike katika kusimamia na kuendesha Uchaguzi ulio huru,
haki, uadilifu na uwazi ili kuepusha visababishi vya uvunjaji wa amani nchini.
4.
Tume ya
Uchaguzi Zanzibar pamoja na taasisi nyengine husika, wavifanyie kazi kwa haraka
VIASHIRIA VYA UVUNJAJI WA AMANI vilivyosababisha uvunjaji wa amani na
machafuko katika chaguzi zilizopita.
5.
Serikali na
Mamlaka zinazohusika na utunzaji wa amani, wawe waadilifu na kutumia busara
katika kukabiliana na matukio ya uvunjaji wa amani ili kuepusha mizozo isiyo ya
lazima nchini.
6.
Viongozi wa Siasa,
Viongozi wa Dini, Walimu wa Madrasa, Walimu wa Skuli, Wahadhiri wa Vyuo Vikuu
na Wakufunzi wajiepushe kutumia kauli zinazoweza kuwachochea wafuasi na wanafunzi
wao kuingia katika kuvunja amani ya nchi.
7.
Viongozi wa
Dini wawaelimishe Wazanzibari kushikamana na Misingi ya Dini yao inayohimiza AMANI
pamoja na kufanya juhudi za kurudisha hadhi ya kihistoria ya Zanzibar kama
chimbuko la ELIMU, MAENDELEO na USTAARABU.
8.
Viongozi wa
Dini wawe waadilifu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu kwa
kuepuka ushabiki wa kivyama ili kulinda hadhi na heshima yao.
9.
Washiriki wa
Mkutano huu, Waandishi wa Habari na Wadau wote wa Uchaguzi, waichukue na
kuitangaza Kauli Mbiu ya Mkutano huu inayosema “UCHAGUZI UTAPITA,
ZANZIBAR ITABAKIA, PIGA KURA KWA MAENDELEO NA AMANI ENDELEVU”.
10.
Waandishi wa
habari wazitumie kalamu zao vizuri kushajiisha jamii kudumisha AMANI
kuelekea Uchaguzi Mkuu na wasikubali kutumiwa kuchochea chuki, uadui na
migawanyiko itakayopelekea machafuko ya nchi.
11.
Friends of
Zanzibar kwa kushirikiana na Ofisi ya Mufti iwe tayari kuwajengea uwezo Wanawake
kupitia Taasisi zao ili kushiriki kikamilifu katika kushajiisha ujumbe wa AMANI,
UTULIVU na MSHIKAMANO miongoni mwa Wazanzibari.
12.
Friends of Zanzibar,
Ofisi ya Mufti na taasisi nyengine za dini, wawajengee uwezo Walimu wa Madrasa ili
kutekeleza jukumu la malezi ya watoto na vijana kwa azma ya kuwa na raia wema wa
sasa na baadaye.
13.
Friends of
Zanzibar, Ofisi ya Mufti na taasisi nyengine, wawe tayari kujenga uwezo wa vijana
kimaadili na kiuchumi ili kuwafanya watumike katika kuleta maendeleo ya nchi.
14.
Friends of
Zanzibar na Ofisi ya Mufti kwa kushirikiana na Taasisi nyengine za Kiislamu,
waandae mpango kazi wa utekelezaji wa Maazimio haya.
No comments:
Post a Comment