Habari za Punde

Malimu Seif Ahutubia Viongozi wakati wa Mkutano wa Amani Zanzibar.

Na: Hassan Hamad (OMKR).
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema suala la utoaji wa haki kwa wananchi litabaki kuwa msingi wa kuwepo amani na utulivu nchini.

Amesema bila ya wananchi kutendewa haki, wataanza kulalamika na kuonesha kutokuridhika na hatimaye kufanya vitendo vinavyoweza kuvuruga amani ya nchi.
Maalim Seif ameeleza changamoto hiyo wakati akiufunga rasmi mkutano wa siku mbili wa amani uliofanyika hoteli ya Zanzibar Beach Resort nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Amesema utoaji wa haki unakwenda sambamba na kuwepo utawala mwema, ukiwa ni utaratibu uliowekwa na mataifa mbali mbali katika kuhakikisha watu wanaishi kwa salama na amani.

Amefahamisha kuwa kukosekana kwa misingi ya utawala mwema kama vile watu kunyimwa haki zao za kibinadamu, inaweza kuwa chanzo kikuu cha kukosekana kwa amani na kusababisha wananchi kukumbwa na madhara makubwa.

Hivyo amesema rasilimali zilizopo pamoja na haki nyengine za msingi ziwekewe utaratibu mzuri, ili kila raia aone kuwa anatendewa haki, na kuondosha uwezekano wa kuwepo madaraja ambayo ndio chachu ya kuvurugika kwa amani.

Mbali ya utoaji wa haki, Maalim Seif ameutaja mchakato wa uchaguzi kama sababu nyengine kuu inayopelekea  uvunjifu wa amani katika nchi mbali mbali duniani ikiwemo Zanzibar.

Hata hivyo amesema baada ya wadau wakuu wa uchaguzi Zanzibar kujitathmini na kufikia maridhiano mwaka 2009, Zanzibar kwa mara ya kwanza iliweza kufanya uchaguzi wa amani mwaka 2010, na kuudhihirishia ulimwengu kuwa inawezekana kufanyika uchaguzi wa amani.

Amesema hatua hiyo inapaswa kuendelezwa kwa kujiepusha na chokochoko na matendo yanayoashiria kuvunjika kwa amani kama vile kutoa kauli za uchochezi na kusababisha vurugu zisizo za ulazima.

Amesisitiza kuwa wadau wa uchaguzi wana wajibu wa kuhimizana katika suala la utoaji wa haki , ili amani iliyopo iendelee kudumu.

Aidha amesema iwapo maazimio yaliyotolewa na mkutano huo wa amani ya Zanzibar yatatekelezwa kwa vitendo, Zanzibar itabaki kuwa nchi ya amani wakati na baada ya uchaguzi na kuwa mfano wa kuigwa duniani.

Maalim Seif akiwa pia mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Wananchi (CUF)ameahidi kutoa kila aina ya ushirikiano ili kuona kuwa amani ya Zanzibar inaendelea kuwepo.

“Tunataka Zanzibar ibaki kuwa njema” alisisitiza Maalim Seif.

Mapema akisoma maazimio ya mkutano huo, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Sheikh Abdallah Talib, amesema Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar pamoja na wadau wote wa uchaguzi, wanapaswa kuvifanyia kazi viashiria vyote vya uvunjifu wa amani kabla ya kuleta madhara kwa jamii.

Aidha ameshauri viongozi wa dini na siasa kuepuka kutoa kauli zinazoashiria chuki, ubaguzi na uchochezi kwa wananchi.

Akitoa neno la shukrani, mlezi wa marafiki wa Zanzibar Prof. Abdulhafoor El-Busaidy amewashukuru washiriki wa mkutano huo kwa michango waliyoitoa, sambamba na kuwapongeza Makamu wa Kwanza na wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa ushiriki wao, hali inayoashiria kuguswa na amani ya Zanzibar.

Mkutano huo wa siku mbili wa Amani ya Zanzibar, umezishirikisha nchi mbali mbali zikiwemo Kenya, Uganda, Namibia, Msumbiji na Malawi.
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.