Habari za Punde

Shule ya msingi ya Mtemani , Wingwi yapatiwa vifaa vya kisasa vya Maktaba

 Mwalimu mkuu msaidizi wa shule ya Mtemani akisoma risala kwa mgeni rasmi Bwana Yussuf Shoka Hamad
 Baadhi ya wanakamati wakifuatilia kwa kina hafla fupi ya kukabidhiana vifaa vya maktaba ya kisasa itakayofunguliwa katika shule ya msingi Mtemani, Wingwi
 : Baadhi ya vifaa vilivyokabidhiwa kwa ajili ya ujenzi wa maktaba ya kisasa shuleni hapo
 Bwana Yussuf Shoka Hamad akimkabidhi  pazia la projector Mwalimu mkuu wa shule ya msingi mtemani, Wingwi Bi Wahida Saleh Hamad katika hafla fupi ya kukabidhiana vifaa iliyofanyika shuleni hapo
 Mwalimu Mkuu shule ya msingi Mtemani, Wingwi  akipokea mashine ya LED projector kutoka kwa muhisani wao Bwana Yussuf Shoka Hamad
 Mwalimu Mkuu, shule ya msingi Mtemani, Wingwi akipokea Mashine ya Kompyuta kutoka kwa muhisani wao Bwana Yussuf Shoka Hamad
Bwana Yussuf Shoka Hamad akimkabidhi  kioo cha Kompyuta Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Mtemani, Wingwi Bi Wahida Saleh Hamad.

Na: Moh’d  Said
Shule ya msingi ya mtemani Wingwi iliyoko Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, imekabidhiwa vifaa vya kisasa kwa ajili ya ujenzi na uanzishaji wa maktaba ya kisasa (Digital Library) inayaotarajiwa kufunguliwa hivi karibuni.

Tukio hilo lilifanyika leo katika viwanja vya shule ya mtemani mbele ya kamati ya shule hiyo ambapo muhisani  na mdau wa maendeleo nchini ambaye pia ni mhadhiri kutoka chuo kikuu cha London, SOAS, Bwana Yussuf Shoka Hamad alikabidhi zawadi hizo kama sehemu ya ahadi zake alizozitoa mwaka jana katika hafla ya kuwazawadia wanafunzi waliofaulu vizuri darasa la saba mwaka 2013/14.

Akikabidhi zawadi hizo, Bwana Yussuf Shoka Hamad alisema;

‘Nia yangu ni kuleta mapinduzi ya kweli kwa jamii katika sekta ya elimu. Mapinduzi ya kweli kwa ulimwengu wa sasa yanatokana na kutegemea sana maendeleo ya sayansi na teknolojia. Hivyo, katika kipindi hiki cha miaka mitano (2015/20) nimenuilia kuanzisha maktaba za kisasa (digital libraries) kwa shule zote za Wingwi ili kusukuma mbele maendeleo ya elimu!’



Aidha mhisani huyo alisema kwamba wakati umefika kwa wanakijiji wa Wingwi kuamka na kuipa kipaumbele sekta ya Elimu kwa watoto wao kwani Elimu ndio silaha tosha inayoweza kuleta Mapinduzi nchini. Pia aliwasisitiza wanakamati wa shule hiyo, kuthamini michango inayotolewa na wahisani na wazazi wa wanafunzi kwa kutunza na kuenzi kila msaada unaopatiwa shuleni hapo.

Akitoa mchango wake mbele ya kamati katika hafla hiyo, Mwalimu mkuu wa shule ya Mtemani Bi Wahida Saleh alisema, anashukuru sana kupokea vifaa hivyo na ameahidi kuvitunza na kuvitumia ipasavyo ili kuweza kuleta matunda yanayotazamiwa kupatikana kutokana na uanzishwaji wa maktaba hiyo shuleni hapo.

Naye, mdau wa Elimu na mwanakamati wa shule hiyo Bwana Shoka Hamad Abeid ameinasihi kamati na jamii kwa ujumla kuvitunza vifaa hivyo na kuvienzi kwani kufanya hivyo kutepelekea lengo zima la kulete ufanisi shuleni hapo kufikiwa;

‘Kwa hakika changamoto kubwa linalotukabili kwa sasa sio kupata misaada bali ni jinsi gani tunavitunza na kuiendeleza misaada hiyo. Kwa sisi wanakamati, walimu na wanafunzi, tunao wajibu mkubwa wa kuvitunza vifaa hivi. Kinyume na hivyo tutaishia kupokea na kuomba misaada tu kila siku bila kufikia malengo tunayoyatarajia.’ Alisema Bwana Shoka.

Wakati huo huo, mdau na mtaalamu wa mambo ya takwimu wa kamati hiyo , Bwana Suleiman Said alimuomba Bwana Yussuf Shoka kuwapatia laptops zitakazoweza kusaidia walimu kuandaa masomo yao kwa ufanisi zaidi hata wawapo majumbani.

Shule ya msingi mtemani ni miongoni mwa vituo vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayotegemea zaidi nguvu za jamii na wahisani wazalendo katika kujipatia maendeleo shuleni hapo ambapo kwa sasa imeshapiga hatua mbali mbali za kimaendeleo ikiwamo ya ujenzi wa maktaba ya kisasa na maabara ya kompyuta ambayo inatarjiwa kufunguliwa katika siku za usoni.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.