STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 19 Oktoba, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema serikali ina imani kuwa Zanzibar itakuwa katika utulivu na amani wakati wote wa uchaguzi kwa kuwa uchaguzi huo utafanyika kwa misingi ya uhuru na haki kwa mujibu wa sheria zilizopo.
Akizungumza na Balozi wa Switzerland nchini Mheshimiwa Florence Tinguely Mattli Ikulu leo, Dk. Shein alimueleza balozi huyo kuwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ambayo ndicho chombo makhsusi kinachosimamia uchaguzi kinatekeleza majukumu yake kwa uwazi na kwa kufuata sheria zote zinazohusiana na majukumu yake.
“Tume inatekeleza majukumu yake kwa uwazi bila ya kuingiliwa kwa kuwa masuala yote ya uchaguzi yamewekwa wazi ikiwa ni pamoja na utaratibu wa kupiga kura na kuhesabu kura ambao unafanyika mbele ya maafisa wa Tume, mawakala wa vyama na wagombea pamoja na watazamaji wa ndani na nje” alifafanua Dk. Shein.
Alibainisha kuwa uamuzi wa kuunda serikali yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa ulilenga kuondosha misuguano iliyokuwa imezoeleka baina vyama na wafausi wao mara baada ya uchaguzi na amefarijika kuwa katika kipindi chake ameweza kuongoza vyema na kulifikia lengo hilo.
“Ilikuwa ni changamoto kubwa kwangu kuongoza serikali katika mfumo huo lakini kwa kuwa kila siku nimekuwa na dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi na kuiona Zanzibar katika utulivu na amani tumefanikiwa”alieleza Dk. Shein na kusisitiza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa kila mtu katika serikali.
Kwa hivyo katika hali kama hiyo Dk. Shein alieleza kuwa serikali na wananchi hawatarajii kutokea watu kufanya vitendo vya kuhatarisha amani na utulivu kwa kuwa kila tahadhari imechukuliwa kuweka mazingira ya uchaguzi kuwa huru na haki.
Hata hivyo alisema pamoja na matarajio hayo serikali imejiandaa vya kutosha kukabiliana na vitendo vyovyote ambavyo vinaweza kuhatarisha amani na utulivu wakati wote wa uchaguzi.
Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa idadi kubwa ya wagombea katika nafasi ya Urais katika uchaguzi wa mwaka huu ni ishara kuwa watu wengi wanataka kuitumikia nchi yao na katika nafasi hiyo.
“Wote hao (wagombea) wana lengo moja la kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo; afya bora, elimu bora, uchumi imara na kufikia malengo ya mipango yetu ya maendeleo kama vile Dira ya Zanzibar 2020” Dk. Shein aliongeza.
Kwa hivyo alibainisha kuwa hivi sasa kinachofanyika ni kwa vyama kunadi sera na Ilani zao ili kuwashawishi wananchi wawachague wagombea wao hivyo maamuzi ya mwisho ya nani ataongoza nchi yatafanywa na wananchi.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali na wananchi wa Uswizi kwa misaada yao kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
“nchi zetu zimekuwa marafiki kwa miaka mingi kabla ya Uhuru hadi tumepata uhuru wetu na wakati wote tumekuwa tukishirikiana. Chini ya ushirikiano huo Uswizi imekuwa ikisaidia Tanzania katika sekta nyingi za maendeleo na huduma za jamii ikiwemo afya, uchumi na harakati zetu za kupambana na umasikini” Dk. Shein alieleza.
Katika mazungumzo hayo Balozi Florence alimueleza Mheshimiwa Rais kuwa amefurahi kuiwakilisha nchi yake Tanzania nchi ambayo ni mshirika mkubwa wa Uswizi.
Alimhakikishia Dk. Shein kuwa Uswizi itaendelea kushirikiana na Zanzibar na Tanzania na kuimarisha uhusiano na ushirikiano na nchi yake na Tanzania.
Balozi huyo alieleza matumaini yake kuwa wananchi wa Tanzania wanatumia fursa ya kuchagua uongozi wa nchi yao kwa mafanikio makubwa na kuihakikishia nchi yao amani na utulivu.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822
No comments:
Post a Comment