Habari za Punde

Mauwa Khamis Saateni, apata aradhi yake baada ya miaka 20


Bi Mauwa Khamis Saateni wa shehia ya Vitongoji wilaya ya Chakechake Pemba, akiwa ni mmoja kati ya wanawake 93 wa ukanda wa Mashariki wa kisiwa cha Pemba, ambao baada ya kupata elimu ya ushawishi na utetezi wa haki za wanawake na wanawake kumiliki ardhi na kushinda kesi hiyo mahakama ya ardhi, akiwa kwenye shamba lake ambalo kwa muda wa miaka zaidi ya 20, lilikuwa likishikiliwa na mama yake wa kambu na sasa limerudi mikononi mwake baada ya mafunzo ya VECA (picha na Haji Nassor, PEMBA)

Ni baada ya mafunzo ya kutambua haki zao yalitolewa na VECA

 Na Haji Nassor, PEMBA

‘’HIVI nnavyozugumza nawe, tayari ardhi yangu nimeshaikomboa kutoka mikononi mwa familia yangu, na sasa nshaipanda mahindi’’,alidakiza Bibi Mauwa Khamis Saateni wa Vitongoji Chakechake Pemba,

Nilimtaka arejee maneno hayo, akarejea kama yalivyo hapo juu, na akasema alikaa zaidi ya miaka 20 akiwa hana habari na ardhi yake, ilio kuwa mikononi mwa mama yake wa kambo.

Lakini baada ya Jumuia ya uhifadhi wa mazingira ya Vitongoji wilaya ya Chakechake Pemba, ‘VECA’ kumpa mafunzo ya ushawishi na utetezi wa haki za wanawake na wanawake kumiliki ardhi, hayo ndio matokeo.

“Sasa nna eneo langu karibu ekeri nne, lakini papatu ilipita, maana nilikwenda mahakama ya ardhi kwa muda wa minne, lakini bwana jaji mwisho akasema ardhi nirejeshewe mweyewe’’,alifafanua.

Mwanamke huyu jemedari alikuwa na hadithi refu juu ya mafunzo alioyapata hadi kuweza kutia mikononi ardhi yake, ambapo awali aliona kama mzaha mafunzo hayo.


‘’Kwe kweli VECA walipotuita kutupa mafunzo hayo, mimi niliona kama semina za kawaida tukachukue posho turudi nymbani, lakini yale mafunzo waliotupa yalikua darsa tosha kwangu’’,aliweka wazi.
Mauwa (48), baada ya kuwiva kimasomo kwamba na wao wanahaki ya kumiliki ardhi, na wana haki ya kwenda mahakamani, ndipo alipoanza safari ya kudai ardhi yake.

“Ardhi yake ya ekari nne ilikua inamilikiwa na mama yangu wa kambo, kwa miaka zaidi ya 20, maana tokea mwaka 1994 alikuwa akiitumia bila ya mimi kufahamu’’,alikumbuka.

Baada ya kumaliza mafunzo, alianza kumuuliza mama yake juu ya ardhi yake, ingawa hakupata jawabu nzuri jambo ambalo, baadae aliitisha kikao cha pamoja na kulizungumza hilo na hawakumfahamu.

Binti Saateni, aliamua kwenda mahakama ya ardhi, na baadae wakakutana juu ya kiriri na mama yake wa kambo, ambapo baada ya nenda rudi ya mahakamani, miezi minne baadae, alikabidhiwa ardhi yake.

‘’Mimi hadi leo sijaamini kwamba ardhi yangu nimeipata, maana mama hakua na hoja, na bwana jaji (hakimu) akaamua kuwa nikabidhiwe, na yeye bila ya kinyongo alinipa’’,alisema kwa furaha.

Hawakukosea wahenga waliposema, mwisho wa maji ni tope………..na ndio maana sasa bibi Mauwa, anadunda kwa kupanda mihindi kwenye ardhi yake akiwa na hati zote husika.

‘’Siku niliokabidhiwa na mahakama ardhi yangu, ndio nilipoona umuhimu wa yale mafunzo tuliopewa na VECA, na nasema ahasante jumuia hii’’,alisema kwa shauku.

Bibi Mauwa Khamis Saateni kwa sasa, baada ya kufanikiwa kuikomboa ardhi yake ambayo kwa muda wa zaidi ya miaka 20, ilikuwa mikononi kwa familia yake, mwanzoni mwa mwaka 2014, tayari kwa sasa ametinga tena mahakamani.

Safari hii akiwa kwenye kizimba cha mahakama ya ardhi, anaidai nyumba yake ya urithi, ambayo kwa sasa haimo mikononi mwake.

‘’Tena nailaumu sana ‘VECA’ mafunzo waliotupa sisi wanawake wa ukanda wa mashiriki wa kisiwa cha Pemba, kama wengetupa miaka kumi (10) iliopita, wanawake sisi twengekuwa mbali’’,alieleza kwa furaha.

Kesi hiyo ya kudai nyumba inatarajiwa kunguruma tena kwenye mahakama ya ardhi mwezi ujao mwaka huu wa 2015, mweyewe akiwa na tamaa kubwa ya kufanyiwa haki na Idara ya mahakama ya ardhi.

Bi Mauwa sio pekee ambaye alifanikiwa kupata ardhi yake baada ya mafunzo hayo, lakini hakimu wa mahakama hiyo Salim Hassan Bakari alisema mafunzo hayo yaliamsha idadi kubwa kesi za ardhi.

‘’Baada ya VECA kumaliza mradi wao kwa mwaka wa kwanza, wa ushawishi na utetezi wa haki za wanawake na wanawake kumilikia ardhi, kesi za wanawake pekee zilifikia 93, kwenye mahakama yangu’’,aliweka wazi Hakimu.

Aliddadavua kuwa, kati ya kesi hizo zinazohusu ardhi pekee za wanawake wa ukanda wa mashariki wa kisiwa cha Pemba, kesi 43 zimeshafanyiwa kazi na kutolewa maamuzi.

Miongoni mwa kesi hizo 17, wanawake walishinda akiwemo Bibi Mauwa Khamis Saateni, na sasa ardhi zao wameshakabidhiwa wenyewe na Mahakama na hati zote wameshapewa.

Ingawa kesi nyengine 26, wanawake walishindwa, kutokana na kukosa vithibitisho halisi, ingawa kimatiki inaonekana wamedhulumiwa na wanaume (kaka, ndugu, baba) zao.

Hakimu Salim Hassan Bakari, alitamka kuwa kesi 50 bado hazijamalizika na zinaendelea katika mahakama ya ardhi, zikiwahusu wanawawake wa ukanda wa mashirikia wa kisiwa cha Pemba.

‘’Unajua hata makarani wangu walishituka, baada ya kuona wanapokea kesi mfululizo za wanawake ndani ya miezi minne, tena na kushinda maana walipata ujasiri wa kusimama mahakamani’’, alisema.

VECA  ambayo ilipata ufadhili kutoka kwa ‘the foundation for civil society’ wa shilingi 135,000,000 kwa ajili ya mradi wa ushawishi na utetezi wa haki za wanaweake na wanawake kumilikia ardhi, kwa hakika umezaa matunda,

Maneno hayo ualiiungwa mkono na kijana Khamis Haji Makame, ambae nae alibahatika kushiriki mafunzo hayo yalioandaliwa na VECA kwa kushirikiana na ‘foundation’.

“Mimi nilikua sijui kuwa pia wanawake wanahaki ya kumiliki ardhi, nilijua ni mwanamme tu, maana ndie kiongozi wa familia na mwanamke yeye daima awe nyuma’’, alisema.

Khamis alisema mafunzo hayo ya ‘VECA’ ndio yaliomuamsha na kumpa uwelewa mpana, kwamba kumbe mwanamke kumiliki ardhi sio fursa bali ni haki yake.

Baada ya mafunzo hayo, Khamis yeye ameshamsaidia dadayake (Fatma) kumuelekeza kwamba, amdai kaka yao haki yake ya ardhi, walioirithi na kujimilikisha yeye kwa zaidi ya miaka 10 sasa.

‘’Dada Fatma baada ushawishi na utetezi wangu, na kufanya kikao cha familia, sasa dada ana ardhi yake na kaka aliitoa rahisi, bila ya kwenda mahakama ya ardhi’’,alisema Khamis.

Kubwa Khamis analolitaka kutoka kwa ‘VECA’ ni kuhakikisha mafunzo kama hayo, yanakua endelevu maana wapo wanawake kadhaa wengine hayajawafikia mafunzo hayo.

Mratibu wa mradi huo Mohamed Najim Omar, yeye alisema kwamba jamii ya kijiji cha Vitongiji na ya ukanda wa mashariki kwa ujumla, itajengwa na VECA kwa kushirikiana na ‘the foundation for civil society’ ambayo imekuwa ikiwanunga mkono kila mara.

Mradi huo, ambao ni mwa miaka mitano, ulianza tokea mwaka 2012, na ukitarajiwa kufunga nanga yake mwaka 2015, ingawa alisema yapo matunda kabla ya mradi kumalizika.

Mafanikio makubwa wanayojivunia ni kuona kuwa walengwa wa mradi huo ambao ni wanawake na jamii kwa jumla, wameanza kupata miguu ya kusimama na kudai haki zao.

 ‘’Wanawake wetu wa ukanda wa mashariki, walikua na dhana potofu kwamba, kwa vile mwanamme ndie msisimamizi wa familia, basi umiliki wa ardhi ni wajibu wake’’,alisema.

Kwa sasa hilo Mratibu anajivunia, na kusema idadi ya wanawake 93 kutoka ukanda wa mashariki wa kisiwa cha Pemba, kupeleka mashauri yao mahakama ya ardhi sio dogo.

Muhasibu wa mradi huo, bibi Sifuni Ali Haji, yeye alisema alipata mshangao wakati wa utoaji wa mafunzo hayo, jinsi wanawake wa ukanda wa mshiriki walivyokuwa wakitoa ushuhuda.

‘’Mwanamke anasimama kwenye mafunzo anasema yeye ardhi yake anayo kaka yake au mjomba wake na hujui kinachoendelea, lakini leo si haba ‘foundation’ lazima tujivunie VECA’’,alibainisha.

Sifuni alisema walinza na utekelezaji wa mradi huo kwa, mikutano ya hadhara, ikifuatiwa na mafunzo ya kamati za maendeleoa za vijiji 36 vya ukanda wa mashariki ikiwa ni pamoja na Uwandani, Ole, Kangagani, Furaha, Vitongoji na Pujini.

Watu 120 kwa hatua ya awali walitajwa kufaidika na mafunzo hayo, ambapo baadae VECA, ilikutana na viongozi wa dini na masheha wa shehia zilizo ukanda wa mashariki, huku nayo makundi maalumu yakihusishwa.

Mafunzo hayo yalikuwa na lengo lilelile na kuwapa uwelewa makundi hayo, kwamba yanaweza kufanya ushawishi na utetezi wa haki za wanawake na wanawake kumiliki ardhi.

Ndio maana sheha wa shehia ya Vitongoji Salim Ayoub, yeye aliesma kama jamii itayafanyiakazi mafunzo hayo, migogoro ya kuwania ardhi hasa kwa wanawake yataondoka.

Sheikh Omar Ali Mohamed, yeye alisema ni kosa kidini mwanamme kujimilikisha ardhi ya urithi, zawadi au ya kununua, ambayo ni ya mwamke na kutumia vibaya nguvu na madaraka yake.

Afisa tawala wilaya ya Chakechake Rashid Hadid Rashid, alinukuliwa akisema, juhudi za taasisi ys ‘Foundation’ wa kuifadhili VECA wala fedha zao hazipotei, maana wapo wanawake ambao leo wanajivunia kupata aradhi zao.

Mohamed Kombo Hamad, alisema kutokana na uwelewa walionao wanawake hao, kwa sasa wamekuwa wakijitokeza wenyewe wakati anapotokezea mwekezaji na kutaka kununua aradhi.

‘’Zamani ilikua ardhi ya mwanamke inauzwa na mwanamme, au kaka yake na kisha kilichopatikana hakipati, lakini sasa ni tofauti.

Wengi wanadhani kwamba endapo VECA itahitimisha mradi wake huo mwaka 2015, basi wanawake na jamii ya ukanda wa mashariki, suala la ufahamu wa sheria na sera za ardhi litakuwa pana na kupunguza migogoro ya ardhi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.