Habari za Punde

Taarifa ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa vyombo vya habari kuhusu uchaguzi mkuu kesho 25 Oktoba



TUME YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR TAARIFA YA MWENYEKITI WA TUME YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR MHE. JECHA SALIM JECHA KWA VYOMBO VYA HABARI TAREHE 25 OKTOBA 2015 
Ndugu Wananchi, Kesho Jumapili tarehe 25 Oktoba 2015 ni siku ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar ambapo wananchi wa Zanzibar watapiga kura kumchagua, Rais wa Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani kwa upande mmoja na kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wabunge kwa upande mwengine. 
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imekamilisha taratibu zote muhimu zitakazowawezesha wapiga kura kupiga kura bila ya usumbufu. Aidha, vifaa vyote muhimu vinavyohusika na kazi ya kupigisha kura vimepatikana na vimeshasambazwa katika vituo vyote vya kupigia kura Unguja na Pemba. 
Ndugu wananchi, uchaguzi ni zoezi ambalo hufanyika kwa misingi ya Sheria, linalohitajia utulivu na usalama wa hali ya juu. Kwa hivyo, siku ya kupiga kura, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inawaomba wananchi wote kuzingatia ipasavyo maelekezo ambayo yametolewa na yatakayotolewa na Tume ya Uchaguzi katika vituo vya kupigia kura, kwani maelekezo hayo yatatolewa kwa kufuata mwongozo wa Sheria na yanalenga kudumisha utulivu wakati wote wa kupiga, kuhesabu na kujumlisha kura katika vituo. 
Tume ya Uchaguzi inawasihi wapiga kura wote kuwa endapo katika zoezi la upigaji kura kutajitokeza tatizo kwa upande wa vifaa ni vyema wafuate taratibu za sheria katika kulitafutia ufumbuzi na kamwe yasipitishwe maamuzi yanayokizana za sheria.

 Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inawaomba wananchi kuyafahamu na kuyaelewa mambo yafuatayo kuwa:- 

1. Upigaji kura utafanyika katika vituo vya kupigia kura ambavyo vitakuwa na wastani wa wapiga kura 350. Kila kituo cha kupigia kura kitakuwa na Msimamizi ambaye atakuwa ndiye kiongozi na mdhamini wa shughuli za uchaguzi katika kituo husika. Pia, kutakuwa na Wasimamizi Wasaidizi wa kituo ambao watafanya kazi chini ya dhamana ya Msimamizi wa kituo. 

 2. Kila mwananchi aliyejiandikisha kuwa mpiga kura kwa uchaguzi wa Zanzibar na aliyekuwa na shahada ya kuandikishwa kuwa mpiga kura kwa Uchaguzi wa Zanzibar, na ambaye taarifa zake zitakuwemo katika Daftari la wapiga kura atakuwa na haki ya kupiga kura kumchagua Rais wa Zanzibar, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na Diwani kwa upande mmoja na kwa upande mwengine atapiga kura kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

3. Upigaji kura utafanyika katika eneo ambalo mtu amejiandikisha au karibu na sehemu hiyo. Katika kila kituo cha kupigia kura kutakuwa na watendaji wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na Tume ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na maandishi yanayowaelekeza wapiga kura kujua wapi watapiga kura kwa ajili ya kumchagua Rais wa Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Diwani kwa uchaguzi wa ZEC na Rais wa Jamhuri ya Muungano na Mbunge kwa upande wa NEC. Aidha, katika kila kituo cha kupigia kura, kutakuwa na mawakala wa vyama vya siasa ambao watakuwa na jukumu la kuwakilisha na kulinda maslahi ya wagombea wa vyama vyao katika kituo, kugundua watu wanaojifananiza (personation) na kushirikiana na Msimamizi wa kituo na Wasimamizi Wasaidizi wa vituo juu ya usimamizi mzuri wa sheria katika kituo.
 4. Kuwa vituo vyote vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1.00 asubuhi na kufungwa saa 10.00 jioni. Muda huo utakapomalizika hakuna mpiga kura atakayeruhusiwa kujiunga katika msitari wa kuingia katika kituo cha kupigia kura, bali watakaokuwa katika misitari ya kuingia kituoni ndani ya muda huo, wataendelea na upigaji kura hadi mtu wa mwisho atakapomalizika. Itakapofika saa 10 kamili askari atasimama nyuma ya mtu wa mwisho katika mstari. Mtu yeyote atayekuja baada ya hapo hataweza kupiga kura. 
5. Kila mpiga kura ajitahidi kufika mapema katika kituo cha kupigia kura na ahakikishe kuwa amechukuwa shahada yake ya kupigia kura. Na kuwa, iwapo atawakuta watu wengine wamejipanga katika mstari, ajipange nyuma yao bila ya usumbufu. 
6. Wapiga kura wagonjwa na ambao hawawezi kupiga kura wenyewe, wanaruhusiwa kwa mujibu wa Sheria kwenda vituoni na watu wanaowaamini ili kuwasaidia kupiga kura. Hairuhusiwi na ni marufuku kwa mtu asiyekuwa na sifa za kupigiwa kura kupigiwa kura. Endapo itabainika Mkuu wa Kituo cha kupigia kura au Msaidizi wake ataruhusu mtu au watu wasiostahiki kupigiwa kura hatua za kinidhamu na sheria zitachukuliwa mara moja. Tume inawasihi Wakuu wa Vituo na Wasaidizi wao kuwa waangalifu sana na makosa hayo. 
7. Hairuhusiwi kuendesha kampeni ya aina yoyote katika vituo vya kupigia kura. Na kuwa, si ruhusa kwa mpiga kura au wapiga kura kuvaa sare au alama za vyama vyao vya siasa au wagombea wanapokwenda kupiga kura. Aidha, ni marufuku kwa wapiga kura kwenda katika vituo vya kupigia kura wakiwa wamebeba silaha za aina yoyote kwa njia ya dhahiri au kificho. 
8. Mtu yeyote haruhusiwi kubaki kituoni baada ya kupiga kura yake. Hivyo, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inawasihi wapiga kura mara wanapomaliza kupiga kura waondoke vituoni na kurejea nyumbani au kwenda katika shughuli zao nyengine. Inasisitizwa mzunguuko wa mita mia mbili kutoka kituo cha kupigia kura hapatakiwi kuonekana mtu yeyote asiyestahiki. 
9. Kila mgombea anaruhusiwa kuweka wakala mmoja katika kituo cha kuhesabia kura na kujumlishia kura. Kila wakala wa mgombea atapatiwa nakala ya fomu ya matokeo ya hesabu ya kura kituoni baada ya kura kuhesabiwa katika kituo na nakala ya fomu ya matokeo ya jimbo au wadi baada ya kura kujumlishwa. 
10.Hakuna mtu mwengine yeyote zaidi ya watu waliotajwa katika Sheria ya Uchaguzi anayeruhusiwa kuwepo katika eneo la kuhesabia kura. Aidha, hakuna mtu zaidi ya waliotajwa katika sheria atakayeruhusiwa kuwepo katika masafa ya mita mia mbili kutoka pahala panapohesabiwa kura. 
11.Kazi ya kujumlisha na kuhesabu kura kwa wagombea Uwakilishi na Udiwani kwa vituo itafanywa katika vituo maalum katika kila jimbo. Katika vituo hivyo, wagombea wote watakaoshinda kwenye chaguzi hizo (Uwakilishi na Udiwani) ndimo watakamotangazwa na Wasimamizi wa Uchaguzi wa majimbo husika. 
12.Kazi za kujumulisha hesabu za kura kwa wagombea Urais wa Zanzibar zinafanywa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa mujibu wa Sheria, na ni Tume ya Uchaguzi peke yake ndiyo yenye madaraka ya kumtangaza mshindi wa kiti cha Urais wa Zanzibar baada ya kuthibitisha matokeo ya mshindi. 
13.Ni makosa kufanya mambo yafuatayo wakati wa zoezi la upigaji wa kura:- 
 Kutaka kupiga kura kabla ya kituo hakijafunguliwa au baada ya kufungwa. 
 Kupiga kura au kukusudia kupiga kura kama huna haki ya kufanya hivyo. 
 Kupiga kura au kukusudia kupiga kura zaidi ya mara moja katika uchaguzi mmoja. 
 Kupiga kura kwa jina la mtu mwengine, aliyehai, aliyekufa au kwa njia ya udanganyifu. 
 Kutia ndani ya sanduku la kura kitu chengine chochote zaidi ya kura. 
 Kuingiza au kuharibu karatasi ya kura au shahada ya matokeo au fomu yoyote inayohusiana na uchaguzi.  Kujaribu kumshawishi mpiga kura kumchagua mgombea maalum. 
 Kutaka kujua mgombea ambaye mpiga kura anakusudia kumpigia kura au aliyempigia kura. 

Ndugu Wananchi na Viongozi wa Vyama vya Siasa cha muhimu kuliko yote katika maelezo yangu ni matokeo baada ya zoezi la kupiga na kuhesabiwa kwa kura. Katika hilo naomba kuwakumbusha kuwa katika ushindani wowote ule kuna kushinda na kushindwa. 
Hivyo, ni vyema kwa wagombea na wafuasi wa wagombea na vyama vyao kuwa tayari kwa matokeo ya ama kushinda au kushindwa. Na pale ambapo mgombea hakuridhika na matokeo ni vyema akatumia njia au taratibu za kisheria katika kutoa malalamiko yake. 
Njia nyengine yoyote mbadala wa hiyo wakati wa kushughulikia maalamiko ya kiuchaguzi inaweza kuondoa utulivu na kupelekea hasara kubwa kwa nchi yetu. Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa upande wake inafanya kila linalowezekana katika kuendesha Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa tarehe25 Oktoba 2015 kwa salama na amani na pia itahakikisha kuwa Uchaguzi mwaka 2015 unakuwa huru na wa haki. 
14. Ndugu wananchi imebainika tabia kwa baadhi ya wafuasi wa vyama vya Siasa kuwa siku ya kupiga kura au kabla ya hapo kuwanyanganya vitambulisho vya kupigia kura wapiga kura wa Chama au vyama vyengine au kuvinunua kwa madhumuni ya kuwazuia kupiga kura na eti kupunguza kura za vyama vyengine, mara nyengine huwatisha au kuwasusia huduma za kijamii. Hayo ni makosa yasiyovumilika. 
Tume ina waonya watu wote wenye tabia ya aina hiyo waache mara moja. Atayebainika na vitendo hivyo atachukuliwa hatua za kisheria. Mpiga kura yeyote atayepatwa na kadhia ya aina hizo atoe taarifa kwenye mamlaka zinazohusika kama vile Tume yenyewe au Polisi. 
Vyama vya siasa vinaombwa kuwatahadharisha wafuasi wao kutojingiza katika makosa ya aina hiyo. 
Nawatakia wananchi wote wa Zanzibar kila kheri na mafanikio katika upigaji wa kura kesho tarehe 25 Oktoba, 2015. Ahsanteni kwa kunisikiliza. 
JECHA SALIM JECHA MWENYEKITI, TUME YA UCHAGUZI ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.