Habari za Punde

Zanzibar Press Club yatoa tamko kuelekea uchaguzi mkuu

Na Miza Othman-Maelezo Zanzibar  

Waandishi wa Habari Nchini wameshauriwa kujidhibiti na kufuata sheria za Taaluma yao hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki ili kuisaidia nchi kubaki katika hali ya Amani na utulivu.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waandishi wa Habari wa Zanzibar (Zanzibar Press Club ZPC)  Abdallah Abdulrahman  Mfaume  wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya umuhimu wa kujilinda wakati wakuandika habari za Uchaguzi huko Afisini kwao Kijangwani Mjini Zanzibar.

Amesema hatua ya mchakato wa Uchaguzi ilipofikia ni ngumu kuliko ilipotoka na kwamba Waandishi inawalazimu kuzifuata vyema Sheria zao ili kuiepusha nchi kuingia katika machafuko.

 “Tunawaomba kufanya kazi ya kufuatilia kwa  makini na kuwapasha wananchi matukio mbali mbali yatakayojiri katika siku ya kupiga kura na nyengine zitakazofuata kwakuzingatia haja ya kuwepo kwa amani na utulivu”alisema Mwenyekiti Mfaume.

Aidha Mwenyekiti huyo  amewakumbusha Wanahabari kuwa na subra na kufanya utafiti wa kina kwa kila jambo linalotokea kabla ya kuchapishwa au kutangazwa ili pia liwaepushie Waandishi   kuingia katika matatatizo kutokana na habari iliyotolewa na chombo husika.

“Mtakubaliana nami kuwa hakuna dhiki itakayoingia ndani ya nchi na kuwaweka kando baadhi ya watu katika nchi au jamii ile ile, hivyo kila mmoja wetu raia au mgeni aliyepo nchini anapaswa kuimba wimbo wa amani na utulivu”alisema Mwenyekiti huyo.


 Hata hivyo amewaomba vingozi wa Dini zote na kila Mtanzania kwa imani yake waendelee kuliombea taifa katika sala zao ili Mwenyenzi Mungu aujalie uchaguzi huo umalizuke katika mazingira ya haki, uhuru, amani na upendo.
Mwenyekiti Mfaume amelishukuru Jeshi la Polisi na taasisi zingine za ulinzi na usalama kwa kuweza kusimamia hali ya amani na utulivu toka katika kipindi cha uandikishaji wapiga kura, kampeni za uchaguzi na kuliomba liendelee kufanya hinyo katika hatua zilizobakia.

Amesema katika kuliunga mkono hili ni vyema vyama vya siasa vikawaelekeza washabiki na wanachama wao kuzingatia sheria za nchi na kuzitii kabla ya kushurutishwa ili kuepukana na usumbufu usio wa lazima.

Vilevile amezishukuru taasisi za umma na binafsi kwa kuendelea kutekeleza wajibu wao katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwani ni jambo litakalopelekea kutoa nafasi kwa wananchi kutumia haki zao kikatiba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.