Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Makamo Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya CNOOC kutoka Nchini China Cui Hanyun wakati alipofika ikulu mjini Zanzibar leo na ujumbe aliofuatana nao.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza Ujumbe wa Kampuni ya China National Offshore Oil Company ltd (CNOOC) ulifoka Ikulu Mjini Zanzibar kuonana na Rais ukiongozwa na Balozi wa China nchini Tanzania Xie Yunliang (wa pili kulia) na Makamo Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya (CNOOC) Cui Hanyun (katikati) wengine ni viongozi wa juu wa kampuni hiyo,[Picha na Ikulu.]
STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 16.12.2015

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amesema kuwa azma ya Kampuni ya China National Offshore Oil
Company (CNOOC) ya kutaka kuanzisha ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi hapa
nchini itasaidia katika kutekeleza lengo la Zanzibar la kuinua uchumi wake.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo huko Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na Ujumbe wa
Kampuni ya China National Offshore Oil (CNOOC) uliofuatana na Balozi mdogo
anayefanyia kazi zake hapa Zanzibar Mhe. Xie Yunliang.
Katika mazungumzo
hayo, Dk. Shein alisema kuwa China ina historia
kubwa katika harakati zake za kuiunga mkono Zanzibar tokea mwaka 1964 na
kuanzia hapo hadi hii leo iko bega kwa bega na Zanzibar hivyo azma ya Kampuni
ya CNOOC kutoa ushirikiano wake kwa Zanzibar katika kuendeleza juhudi za
Serikali katika kuinua sekta ya nishati itasaidia kukuza uchumi na maendeleo ya
Zanzibar.
“Uhusiano wa Zanzibar
na China ni wa kihistoria na ulianza muda mrefu hivyo, kujitokeza kwa Kampuni
ya CNOOC kutoka nchini humo kutazidisha
ushirikiano kama ilivyo kwa sekta nyenginezo hatua ambayo itasaidia lengo na
madhumuni ya Zanzibar katika kuimarisha uchumi wake”, alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alisisitiza
kuwa jambo muhimu katika ushirikiano huo ni kupata utaalamu na uzoefu kutoka
kwa Kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa nafasi za masomo zinazohusiana na
sekta hiyo kwa wazalendo hatua ambayo itasidia kufikia lengo lililokusudiwa.
Dk. Shein alisema kuwa
Zanzibar imeweza kupata ushirikiano mkubwa kutoka nchi hiyo ikiwa ni pamoja na
kuungwa mkono katika sekta zake za maendeleo hivyo azma ya China katika kuiunga
mkono Zanzibar kwenye eneo hilo jipya itasaidia kwa kiasi kikubwa kuinua uchumi
na maendeleo ya Zanzibar.
Alisema kuwa Zanzibar ina
mengi ya kujifunza kutoka kwa ndugu zao wa China hivyo, kwa upande wa sekta ya
mafuta na gesi Zanzibar itapata mafanikio makubwa na kuweza kupiga hatua kibiashara
na kitaalamu.
Dk. Shein alisema kuwa
juhudi za makusudi zimechukuliwa na Serikali zote mbili ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha suala la mafuta na gesi
linatekelezwa na kusimamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hatua ambayo
inatoa fursa kwa Zanzibar kushirikiana na Kampuni yoyote yenye sifa na uwezo kutoka
nje.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alisema kuwa baada ya kufuatwa kwa taratibu husika za kiserikali katika
kutekeleza azma hiyo, Zanzibar itakuwa na matumaini makubwa katika kupata
mafanikio kwa kuendeleza ushirikiano huo kwa pande zote mbili.
Nae Makamu wa Rais wa
Kampuni hiyo ya CNOOC Bwana Cui Hanyun alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Zanzibar
kwa kuendeleza uhusiano na ushirikino
kati yake na China ambao umedumu kwa muda mrefu.
Bwana Hanyun alisema
kuwa Kampuni ya CNOOC ni Kampuni kubwa na ya Kitaifa nchini China ambayo
imeanza mwaka 1982 ambapo hivi sasa inafanya kazi sehemu mbali mbali duniani zikiwemo
nchi za Amerika, Ulaya, Asia, Afrika na Australia.
Miongoni mwa nchi za
Afrika ambazo kampuni hiyo inaendeleza shughuli zake ni Kenya, Nigeria, Uganda,
Garbon na nchi nyenginezo za Bara la Afrika na kueleza hatua zinazoendelea
katika uendelezaji wa sekta hiyo katika nchi hizo.
Bwana Hanyun alisema
kuwa Kampuni hiyo imekuwa ikitoa ushirikiano kwa njia mbali mbali ikiwa ni
pamoja na kutoa utaalamu juu ya sekta ya mafuta na gesi sambamba na ushauri
elekezi.
Pamoja na hayo
Kiongozi huyo wa Kampuni hiyo aliahidi kutoa ushirikiano wake mkubwa katika
kuhakikisha Zanzibar inaimarika katika sekta ya mafuta na gesi na kuweza kupata
manufaa ya kimaendeleo na kiuchumi.
Nae Balozi Mdogo
anaefanyia kazi zake hapa Zanzibar Mhe. Xie Yunliang alimuhakikishia Dk. Shein
kuwa China itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake na Zanzibar katika kuimarisha
sekta mbali mbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuendelea kuipa nafasi za
masomo nchini humo.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment