RISALA YA
RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA
LA MAPINDUZI, MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN
YA KUUKARIBISHA MWAKA MPYA WA 2016.
NduguWananchi,
Assalam Aleikum,
Kwa hakika tuna wajibu wa kumshukuru
Mwenyezi Mungu, Mtukufu, Muweza wa Kila Kitu kwa kutupa uhai tukaweza kufika hadi
siku hii ya leo tunapouaga mwaka 2015 na
kuukaribisha mwaka mpya wa 2016. Hii ni neema kubwa aliyoturuzuku Mola wetu,
Subhana Wataala kwani katika kipindi kama hiki mwaka jana, tulikuwa na wenzetu
ambao kwa hivi sasa wamekwishatangulia mbele ya haki. Tumuombe Mwenyezi Mungu
awasamehe makosa yao na awape malazi mema.
Na sisi tulio hai atujaalie khatma njema.
Wakati mwaka 2015 unamalizika ni vyema
japo kwa muhtasari tukatafakari baadhi ya masuala muhimu tuliyokabiliana nayo
katika mwaka huo. Hatua hiyo, itatuwezesha
kufanya tathmini ya mafanikio na changamoto tulizokumbana nazo ili tuweze
kujipanga na kuweka dhamira ya kuzifanyia kazi kwa lengo la kupiga hatua zaidi
za maendeleo kwa mwaka ujao.
Ndugu
Wananchi,
Katika mwaka wa 2015, nchi yetu ilikuwa
na hali ya amani na utulivu jambo ambalo tunapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu
kwa kutupa neema hiyo ambayo imetuwezesha kutekeleza kwa mafanikio mipango yetu
ya maendeleo ikiwemo Dira ya Maendeleo ya
Mwaka 2020, MKUZA II, Malengo ya Milenia na Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2010 – 2015 ambayo tuliweza
kuitekeleza kwa asililmia 90. Kuwepo kwa
amani kumetuwezesha wananchi kuendelea na shughuli zetu za kila siku kwa
utulivu. Kutokana na amani na utulivu
uliopo wageni wengi wameendelea kuitembelea
nchi yetu. Jumla ya watalii 254,699 waliitembelea Zanzibar katika kipindi cha
Januari-Novemba, 2015 na kupelekea sekta hii kuimarika kwa kiasi kikubwa.
Kufuatana na takwimu za robo mbili za mwanzo
wa mwaka 2015, uchumi wetu umeendelea kuimarika. Sura halisi itafahamika baada ya kumalizika
kabisa kwa mwaka huu na tathmini kamili ya hali ya uchumi kufanywa. Kwa upande mwengine, huduma za jamii zikiwemo
upatikanaji wa maji safi na salama, huduma za afya pamoja na elimu zimeimarika.
Ndugu
Wananchi,
Katika mwaka huu, tumepiga hatua kubwa
katika kuimarisha miundombinu. Tumeweza kumaliza ujenzi wa barabara muhimu na
kuzizindua Unguja na Pemba, ikiwemo barabara ya Wete Gando na Wete Konde.
Tumeimarisha bandari zetu pamoja na viwanja vya ndege. Sote ni mashahidi wa
kazi kubwa tuliyoifanya katika kukiimarisha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha
Abeid Amani Karume pamoja na Kiwanja cha ndege cha Pemba ambacho tayari
tumekitia taa za kurukia ndege. Katika mwaka 2015, tulikamilisha na kuzindua
mradi wa ujenzi wa maegesho ya ndege (Apron) na njia za kupitia ndege (taxiway)
katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume. Kadhalika, tumeendeleza ujenzi wa jingo la
abiria litalokuwa na uwezo wa kuchukua abiria milioni 1.6 kwa mwaka.
Hatua tuliyofikia katika ujenzi wa
viwanja hivi tayari imepelekea kuwepo kwa ongezeko kubwa la idadi ya ndege za Kimataifa
zinazokuja Zanzibar, jambo ambalo limepelekea kuimarika kwa sekta ya utalii na
shughuli za biashara.
Ndugu
Wananchi,
Miongoni mwa masuala muhimu ya
maendeleo ambayo nchi yetu imeyapata katika mwaka uliomalizika ni kufanikiwa
kwa lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, la kuwapatia
meli mpya wananchi wa Zanzibar. Serikali
iliweka dhamira ya dhati ya kupambana na tatizo la uhaba wa vyombo vya
kuaminika vinavyofanya safari zake kati ya Unguja, Pemba na Dar es Salaam. Tulifanikiwa kuitengenezesha meli mpya, yenye
mitambo ya kisasa katika Kampuni ya “Daewoo International” ya Jamhuri ya Korea
ambayo ina utaalamu na uzoefu mkubwa wa kutengeneza meli.
Tayari meli hiyo tuliyoipa jina la MV
Mapinduzi II, iliwasili nchini tarehe 2 Disemba, 2015. Nasaha zangu kwenu nyote wananchi ni kuwa,
tuithamini na kuienzi meli yetu hiyo.
Tukumbuke msemo wa Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, kuwa “kithamini kilicho chako mpaka usahau cha
mwenzako” .
Katika mwaka 2015, tumefanya juhudi
kubwa katika kuhakikisha kuwa dhamira yetu ya kujenga bandari ya Mpiga Duri
tunaanza kuitekeleza. Juhudi kubwa
zimefanywa katika kutafuta fedha za mradi huu.
Hivi sasa Serikali inakamilisha mazungumzo ya kupata fedha kwa njia ya
mkopo kutoka “Exim Bank” China. Kwa
kuanzia ujenzi wa bandari hii, utachukua eneo la mita 300 kutoka Kusini kwenda
Kaskazini na utajumuisha ufukiaji wa bahari, eneo lenye urefu upatao mita
490. Ujenzi wa bandari hii utategemea
kuanza wakati wowote katika mwaka 2016.
Ujenzi huo utakapomalizika utapunguza msongamano uliopo katika bandari
ya Malindi na utaimarisha kwa kiasi kikubwa ukuaji wa biashara hapa Zanzibar. Kadhalika, gati hiyo itatoa ajira kwa
wananchi na kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wetu.
Vile vile, katika mwaka huu unaomalizika tumepata
mafanikio katika juhudi zetu za kusambaza huduma za umeme vijijini. Vijiji mbali mbali kama vile Kijini
na Mbuyu Tende katika Mkoa wa Kaskazini Unguja vimepatiwa huduma hizo. Aidha,
kwa kuwatumia wataalamu wazalendo tumeweza kuufikisha umeme huko Kisiwa Panza na
Kisiwa cha Makoongwe kwa upande wa Pemba.
Kadhalika, katika mwaka 2015, tumetekeleza
kwa mafanikio miradi ya maji safi na salama katika maeneo mbali mbali, Unguja
na Pemba. Tumeshuhudia ongezeko la
uchimbaji wa visima katika maeneo kadhaa. Vile vile, tunatarajia kulipatia
ufumbuzi, tatizo la maji safi na salama katika Manispaa ya mji wa Zanzibar
kufuatia kutiwa saini Mkataba wa Mradi wa Maji Mjini tarehe 29 Disemba, 2015.
Mradi huo utagharimu jumla ya Dola za
Marekani 21,000 zikiwa ni mkopo kutoka Benki
ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itachangia
asilimia 10. Kampuni zinazohusika ni
NSPT LTD na SPENCON SERVICES LTD zilizosajiliwa nchini Tanzania. Maeneo yatakayofaidika ni Mji Mkongwe na
maeneo yanayopakana na mji huo.
Tumeanza kuifanyia kazi changamoto ya
ukosefu wa huduma za umeme katika sehemu tulizochimba visima, jambo ambalo kwa
kiasi kikubwa huathiri juhudi zetu za
kuwafikishia wananchi huduma hizi muhimu. Matumaini yangu ni kuwa ifikapo mwishoni
mwa mwaka 2016 changamoto hii itakuwa imeshapatiwa
ufumbuzi na kukidhi matarajio ya wananchi.
Ndugu
Wananchi,
Kwa upande wa huduma za afya, katika
mwaka 2015 tumeziimarisha huduma hizo kwa
kuongeza kasi ya kusomesha wataalamu, upatikanaji dawa na huduma mbali
mbali pamoja na kuziimarisha hospitali
zetu kwa kutekeleza miradi mbali mbali ya ujenzi. Katika mwaka wa 2015, tulianza kuijenga upya
hosptali ya Abdalla Mzee Pemba kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa
China. Ujenzi huo utakamilika mwaka
2016. Hivi sasa tunaendelea na uimarishaji
wa Hosptali ya Mnazi Mmoja kwa kujenga majengo mapya na kuongeza kasi ya utoaji
wa huduma mpya ili tufikie azma yetu ya
kuifanya hosptiali hii kuwa ya rufaa. Katika kipindi hiki tumeziondoa gharama za
kuchangia huduma za uchunguzi wa maradhi
kwa kutumia “X-Ray”, “CT-Scan” na “Ultra Sound” na sasa zinatolewa bila ya
malipo kwa wananchi wote. Katika mwaka
ujao wa 2016 juhudi zitafanywa za kuondoa kuchangia huduma za uchunguzi wa
maabara, ili nazo ziwe bila ya malipo.
Katika mwaka 2015 tumepata mafanikio makubwa
kwa upande wa elimu. Tumemaliza na kuanza upya miradi ya ujenzi wa skuli mbali
mbali na kuongeza fani za mafunzo katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu. Vile vile, tumeanza
kutekeleza lengo letu la kuondoa utaratibu
kwa wazazi kuchangia gharama za elimu maskulini kama nilivyotangaza tarehe 12
Januari, 2015. Lengo letu ni kuifanya
elimu ya msingi kuwa bure huku tukiandaa utaratibu ili elimu ya sekondari nayo
iwe bure kama ilivyodhamiriwa na Muasisi wa Mapinduzi yetu ya 1964.
Katika mwaka 2015, tulifikia uamuzi ya
kuwapatia pensheni ya kila mwezi wazee wetu wote waliofikia umri wa miaka 70
bila ya kujali kama waliwahi kuajiriwa Serikalini au hawakuajiriwa. Hatua hiyo itaanza kutekelezwa kuanzia mwezi
April mwaka 2016. Ni wajibu wetu kuwatunza
wazee wetu ambao wamefanya kazi kubwa ya kuijenga nchi yetu katika ujana wao.
Ndugu
Wananchi,
Katika mwaka 2015 tulipanga na kuanza
kutekeleza kwa kasi, mipango ya ujenzi wa miji na majengo ya kisasa katika
sehemu mbali mbali ili kuweza kujenga taswira mpya ya Zanzibar katika kipindi kifupi
kijacho.
Serikali
kupitia ZIPA ilipanga kutekeleza miradi mitano ambayo baadhi yake tayari imeshapata
wawekezaji na kuanza kutekelezwa katika eneo la Fumba. Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa miji ya
kisasa ya makaazi, uwekezaji wa viwanda vidogo vidogo, ujenzi wa kituo cha
kimataifa cha mikutano na maonyesho ya biashara. Serikali, kwa kushirikiana na Kampuni za “Union
Property Developer” na “Coastal Dredging” inaendelea na ujenzi wa barabara
katika maeneo yaliyopangwa kuendelezwa kwa kujengwa mji mpya wa kisasa huko
Fumba. Kwa sasa barabara kuu zenye urefu
wa kilomita 13 zimo katika hatua mbali mbali za ujenzi. Jumla
ya nyumba 1,300 zinatarajiwa kujengwa kwa ajili ya kuuzwa kwa wazalendo katika
kipindi cha mwaka mmoja ambapo kwa kuanzia, nyumba 150 zitaanza kujengwa mwezi
wa Februari, 2016.
Kwa
upande wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mradi wa ujenzi wa mji wa kisasa wa
kibiashara pamoja na hoteli kubwa ya nyota tano, utakaojengwa huko Ma temwe umeanza kutekelezwa na unatarajia
kuwekeza jumla ya Dola za Marekani milioni 800.
Kampuni ya “Pennyroyal ya Gibralter” ndiyo inayotekeleza mradi huo.
Kwa
upande mwengine katika mwezi wa Novemba 2015, Serikali ilitiliana saini Mkataba
na Kampuni ya “Quality Group Limited” ambayo itaanzisha mradi mkubwa wa
kuendeleza Hoteli ya Bwawani na maeneo yanayoizunguuka. Mradi huo utawekeza mtaji wa Dola za Marekani
kiasi cha Milioni 200 na utahusisha kulifanyia ukarabati mkubwa jengo la Hoteli
ya Bwawani na kuliwezesha kutoa huduma za hoteli ya nyota tano. Jengo hili la hoteli litaimarishwa ili kuhifadhi
kielelezo cha mafanikio cha Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya 1964.
Kadhalika,
Serikali imeidhinisha mradi wa upanuzi wa Hoteli ya Mtoni Marine, unaohusisha
utengenezaji wa ufukwe kwa ajili ya mapumziko ya wageni na wenyeji. Upanuzi huo, vile vile, unahusisha
uanzishwaji wa mji mdogo wa kisiwa kwa ajili ya watu wenye uwezo wa kifedha na
hivyo kupelekea Serikali kukusanya mapato yatayotokana na umiliki wa majengo
katika mji huo. Mwaka 2015, ulibeba shughuli nyingi za uanzishwaji wa ujenzi wa
miji mipya.
Sambamba
na juhudi hizo zinazochukuliwa na ZIPA za kushajihisha wawekezaji katika ujenzi
wa miji ya kisasa, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) nao unaendelea na
juhudi za kubadillisha taswira ya Zanzibar kwa kuwekeza katika ujenzi wa
majengo ya kisasa katika eneo la Mbweni. Mradi huu umejumuisha ujenzi wa jumla ya majengo 18 ya
ghorofa 7 kila moja, yatakayokuwa na nyumba 252. Ujenzi wa majengo hayo umeshaanza. Wakati tunamaliza mwaka huu 2015, tunapaswa
kujipongeza kwa kufanikisha ujenzi wa Viwanja vya Watoto, Kiwanja cha Kariakoo
kwa Unguja na Tibirinzi kwa upande wa Pemba. Kukamilika kwa ujenzi wa Mnara wa
Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika eneo la Michenzani,
kumeiletea haiba mpya mji wetu wa Zanzibar na umekuwa ni kielelezo kizuri cha
kumbukumbu ya Mapinduzi yetu ya 1964.
Ndugu
Wananchi,
Ili mafanikio haya tuliyoyapata yawe
endelevu, napenda nikumbushe kuhusu umuhimu
wa kuitunza miundombinu yetu yote ya maendeleo ambapo fedha nyingi zinatumika
katika kuitengeneza kwa ajili ya maendeleo yetu. Inasikitisha kuona kwamba katika mwaka
uliomalizika, baadhi ya watu waliendeleza vitendo vya kuharibu miundombinu
katika maeneo mbali mbali kwa kuweka mbele maslahi yao binafsi na kusahau
wajibu wa kutanguliza maslahi yetu sote.
Katika baadhi ya maeneo ya nchi yetu,
watu hao walikata nyaya za umeme na kusababisha hasara kwa shirika la umeme (ZECO)
na usumbufu kwa wananchi kwa kukosa huduma hiyo. Aidha, katika maeneo mengine vitendo vyao vimesababisha kukosekana
kwa huduma za maji safi na salama. Natao
wito kwa wananchi wote ili tuwe walinzi wa miundombinu yetu na tusichelee kuwafichua
wale wote wanayoiharibu.
Ndugu
Wananchi,
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa
neema ya mvua ambayo imetuwezesha kupata
mazao ya chakula na biashara hasa zao la karafuu katika mwaka
uliomalizika. Kwa mara nyengine tena
napenda niwashukuru wakulima wetu kwa jitihada zao katika kilimo, hali ambayo imesaidia sana kuwapo kwa uhakika
wa mazao ya chakula zikiwemo ndizi, muhogo, viazi, matunda na aina za mboga.
Kadhalika, natoa shukurani kwa wakulima wa mpunga wa kutegemea mvua kwa
jitihada zao, ingawa kwa bahati mbaya hali ya mavuno kwa mwaka uliomalizika
haikuwa nzuri sana.
Tayari maandalizi ya kilimo cha mpunga
wa kutegemea mvua kwa mwaka huu yamekwishaanza katika mabonde mbali mbali ya Unguja na Pemba kwa hatua ya
kuchimbua mashamba. Serikali inaendelea
kutoa ruzuku kwa huduma za matrekta na pembejeo za kilimo kwa wakulima ambapo
kwa msimu wa mwaka 2015/2016, tani 750
za mbolea na lita 15,000 za dawa ya kuulia magugu zimekwishanunuliwa.
Natoa wito kwa wakulima wetu kuzitumia
fursa zilizowekwa na Serikali ili kuongeza tija katika kilimo chetu. Kadhalika,
nawasihi wafuate maelekezo ya maafisa ugani ya kuzingatia misingi ya kilimo
bora kwa kutayarisha mashamba kwa wakati, kutumia mbegu bora, mbolea na dawa za
kuulia wadudu ili tupate mazao mengi yatakayotuwezesha tupunguze uagiziaji wa
mchele hatua kwa hatua kutoka nje ya nchi.
Ndugu
wananchi,
Kuhusu zao la karafuu, napenda nitoe pongezi
kwa wakulima wa karafuu kwa jitihada zao na kushirikiana na Serikali katika
kuliendeleza zao hilo. Wakulima wetu wameitikia vyema wito wa
Serikali wa kuuza karafuu zao katika vituo vya ZSTC ambapo katika msimu wa ununuzi
wa karafuu 2015/2016, hadi kufikia mwezi Novemba, 2015 jumla ya tani 962.7 za
karafuu zenye thamani ya TShs. Bilioni 13.471 zimenunuliwa katika vituo vya
ununuzi wa karafuu vya ZSTC Unguja na
Pemba. Kwa mara nyengine nalipongeza Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) kwa
kazi nzuri waliyoifanya ya kuliendeleza zao la karafuu pamoja na vikosi vyetu
vya ulinzi na wananchi wote kwa kupambana na magendo ya karafuu. Kwa lengo la
kuzidi kuliimarisha zao la karafuu na kuendeleza zaidi zao hili. Mnamo mwezi wa
August, 2015 tulizindua Mfuko wa Maendeleo
ya Karafuu Zanzibar kwa lengo la kuliendeleza zaidi zao hili. Kupitia mfuko huu, tuna matumaini ya kuongeza
ufanisi katika kulishughulikia zao la karafuu ili kuongeza tija.
Ndugu
Wananchi,
Mwaka 2015 ulikuwa ni mwaka wa Uchaguzi
Mkuu ambapo tarehe 25 Oktoba, wananchi wa Zanzibar walishiriki katika kuwachagua
Viongozi kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania. Uchaguzi Mkuu ulitanguliwa na kampeni za vyama
vilivyoshiriki uchaguzi huo na wananchi walishiriki kwa wingi katika kampeni zake.
Uchaguzi wa Viongozi wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania uliosimamiwa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania umemalizika na Chama cha Mapinduzi kimepata ushindi
mkubwa. Nampongeza Mheshimiwa Dk. John
Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais. Kwa upande wa Zanzibar Tume ya Uchaguzi
uliufuta uchaguzi huu hapo tarehe 28 Oktoba, 2015, baada ya kubainika kutokea
kwa kasoro kadhaa kama zilivyoelezwa na Tume hiyo. Aidha, uamuzi huo wa Tume ulitangazwa katika
Gazeti Rasmi la Serikali la tarehe 6 Novemba, 2015 kwamba Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar imeyafuta matokeo yote ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa tarehe 25
Oktoba, 2015 na kwamba uamuzi wa Tume wa tarehe nyengine ya kurudiwa Uchaguzi
Mkuu wa Zanzibar utatangazwa baadae.
Aidha, katika suala zima la hali ya
kisiasa ya Zanzibar, iliyojitokeza baada ya kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu, viongozi
wenu tulishauriana tukutane ili tufanye mazungumzo ya kutafuta suluhu kwa njia
ya amani, ili nchi yetu iendelee kuwa na amani, umoja na mshikamano. Hatimaye
tulikubaliana tuanze mazungumzo hayo. Mazungumzo haya yanatuhusisha viongozi
sita. Viongozi hao ni mimi nikiwa
Mwenyekiti, Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad na
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wakiwa wajumbe. Wajumbe wengine ni Rais Mstaafu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Zanzibar wa
Awamu ya Tano Dk. Salmin Amour Juma na Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya
Sita Dk. Amani Abeid Karume. Mazungumzo
hayo yamefikia hatua kubwa na bado yanaendelea. Taarifa kamili ya mazungumzo
hayo itatolewa mara tu yatakapokamilika.
Ndugu
Wananchi,
Kama inavyofahamika kuwa kila mwaka inapofika mwezi wa Januari, huwa tuna
maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari, 12 mwaka
1964. Katika mwezi wa Januari wa mwaka
2015, tuliadhimisha sherehe za miaka 51 ya Mapinduzi kwa matukio mbali mbali
yaliyojumuisha uzinduzi na uwekaji wa mawe ya msingi wa miradi ya maendeleo kwa
Unguja na Pemba. Wengi wetu, tulishiriki
katika maadhimisho ya siku ya kilele, tarehe 12 Januari, 2015 kwenye Uwanja wa
Amaan na sherehe hizo zilifana sana.
Tarehe 12 Januari, 2016, panapo
majaaliwa tutaadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi, ambapo kama kawaida, sherehe
hizo zitatanguliwa na matukio mbali mbali ya shughuli za uzinduzi wa miradi ya
maendeleo na uwekaji wa mawe ya msingi.
Wito wangu kwa wananchi wote ni kujitokeza kwa wingi katika matukio
mbali mbali yaliyopangwa katika maadhimisho hayo. Tukumbuke kuwa Mapinduzi yetu
ni kielelezo muhimu cha ukombozi wa nchi yetu na uzalendo. Aidha, kushiriki kwetu kwenye sherehe ya
maadhimisho haya ni hatua ya kuyaendeleza malengo ya Mapinduzi kwa shabaha ile
ile waliokuwa nayo waasisi wetu.
Ndugu
Wananchi,
Wakati tunapoukaribisha mwaka mpya na
tukiwa katika maandalizi ya sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi, napenda
nisisitize umuhimu wa kuendeleza usafi wa mazingira katika maeneo tunayoishi. Mazingira
yaliyo machafu ni chanzo kikubwa cha maradhi mbali mbali ya miripuko ikiwa ni
pamoja na maradhi ya kipindupindu. Taarifa kutoka Wizara ya Afya zinaeleza
kuendelea kuwepo kwa maradhi ya kipindupindu katika baadhi ya maeneo nchini na hali
bado si ya kuridhisha sana. Hata hivyo, Serikali
inachukua hatua za kukabiliana na maradhi hayo kwa kuendeleza kambi za matibabu
na kutoa elimu ya afya juu ya namna ya kujikinga nayo.
Natoa wito kwa wananchi nyote mzingatie
kanuni za afya ikiwa ni pamoja na kuimarisha usafi, kutotupa taka ovyo, kuepuka
kuweka bidhaa chini hasa katika kipindi cha
mvua na kuhifadhi vyakula hasa vinavyouzwa barabarani. Aidha, Baraza la Manispaa, Mabaraza ya miji
kwa Pemba na Halmashauri zote za wilaya zichukue hatua ya kusimamia uzoaji wa taka
na kuzipeleka katika maeneo yaliyotengwa pamoja na kuishughulikia misingi
ya maji machafu kama hatua ya dharura ya
kukabiliana na maradhi ya mripuko. Sote tushiriki katika kuisafisha Miji yetu na
maeneo tunayoishi hapo tarehe 3 Januari, 2016, kama ilivyopangwa katika ratiba
ya Maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi kwa mwaka huu.
Ndugu
Wananchi,
Namaliza risala yangu, kwa kukukumbusheni
kwamba kesho tarehe 1 Januari ni siku yetu ya kujitokeza sote kufanya
mazoezi. Tujitokezeni kwa wingi. Nakutakieni kheri ya mwaka mpya viongozi wote,
wananchi, nchi marafiki, washirika wetu wa maendeleo pamoja na mashirika ya
Kimataifa kupitia mabalozi na wawakilishi waliopo nchini. Namuomba Mwenyezi
Mungu atujaalie kheri, baraka na neema nyingi katika mwaka mpya wa 2016. Atuzidishie amani, umoja na masikilizano.
Atujaalie uwezo zaidi wa kuitekeleza mipango yetu kwa ufanisi ili kuimarisha
uchumi na ustawi wa maendeleo ya nchi yetu.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment