Habari za Punde

Dk Shein awaapisha watendaji wa Serikali aliowateua jana

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                   15 Januari, 2016
---

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amemwapisha Bwana Chimbeni Heri Chimbeni kuwa Mshauri wa Rais Masuala ya Utamaduni kufuatia uteuzi alioufanya hapo jana ambapo aliteua pia watendaji wengine wa serikali.

Watendaji wengine walioapishwa leo ni Bwana Juma Hassan Juma Reli kuwa Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango, Bwana Mdungi Makame Mdungi kuwa Katibu Kamisheni ya Utumishi wa Umma na Bwana Kai Bashir Mbarouk kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria.

Bwana Reli ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo ya Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania anachukua nafasi ya Bi Amina Khamis Shaaban ambaye hivi karibuni aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kabla ya uteuzi wa kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma bwana Mdungi alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba Sheria.

Kwa upande wa Bwana Kai Bashir kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Wizara hiyo.

Hafla hiyo fupi iliyofanyika Ikulu ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Said Hassan Said.

Wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora Dk. Mwinyihaji Makame, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma Mheshimiwa Haroun Ali Suleiman, Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Maalim Abdulla Mwinyi na Makatibu na Manaibu Katibu wakuu wa wizara mbalimbali.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.