Habari za Punde

Maelezo Kuhusu Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Waandishi wa Habari wa Vyombo mbalimbali vilioko Zanzibar kuhusiana na maadhimisho ya Sherehe za Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar, iliofanyika katika ukumbi wa Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais Vuga Zanzibar.
---------------------

Ndugu Wananchi,
Nachukua fursa hii kumshukuru Mola wetu Mtukufu kwa kuendelea kuijaalia nchi yetu amani na utulivu na kutuwezesha kuishi kwa umoja na mshikamano. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aiongezee nchi yetu kheri, baraka na mafanikio mema.

Ndugu Wananchi,
Kama ilivyo kawaida, kila ifikapo tarehe 12 Januari ya kila mwaka Nchi yetu huadhimisha sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964. Kwa mwaka 2016 tutakuwa tunatimiza Miaka 52 tangu Viongozi na wazee wetu walivyoikomboa Nchi yetu kutoka mikononi kwa wakoloni wa Kisultani na vibaraka wao tarehe 12 Januari, 1964. Bila shaka tukio hili ni jambo la kujivunia kwa kila mwananchi mpenda maendeleo na anayeifahamu vyema Historia ya Zanzibar kabla na baada ya Mapinduzi.

Ndugu Wananchi,
Kwa kawaida katika kipindi cha maadhimisho ya sherehe hizi, viongozi wetu na wananchi hushiriki katika shughuli mbali mbali zikiwemo ujenzi wa taifa, uwekaji wa jiwe la msingi na ufunguzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo, burudani na michezo na katika kilele cha maadhimisho hayo siku ya tarehe 12 Januari Uwanja wa Amaan au sehemu nyengine yeyote inayopangwa na Serikali. 

Ndugu Wananchi,
Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar yatafanyika kama kawaida na yamepangwa kuanza rasmi Jumapili ya tarehe 3 Januari, 2016 na kufikia kilele chake tarehe 12 Januari, 2016 katika Uwanja wa Amaan.  Kwa mujibu wa ratiba ya maadhimisho hayo, siku ya uzinduzi rasmi, Jumapili ya tarehe 3 Januari, 2016 itakuwa ni maalum kwa kazi za usafi wa mazingira katika maeneo yetu ya makaazi, sehemu za kutolea huduma za kijamii kama vile hospitali, sokoni na maeneo mengine yote.

Ingawa zoezi hili huwa tunalifanya kila tunapoanza kuadhimisha sherehe hizi kila mwaka, katika maadhimisho haya tunapaswa kuchukua juhudi maalum ili kuhakikisha kuwa maeneo yetu yanakuwa safi muda wote. Kama tunavyojua, nchi yetu hivi sasa inakabiliwa na tatizo kubwa la kuenea kwa maradhi ya kipindupindu. Hivyo, tutumie pia maadhimisho haya kuchukua hatua za kujikinga na kupambana na maradhi haya ambayo kwa kiasi kikubwa husababishwa na mazingira machafu ya sehemu tunazozitumia kwa shughuli zetu za kila siku.


Ndugu Wananchi,
Zoezi la usafi wa mazingira ni la lazima na kutaandaliwa utaratibu maalum kwa kila Mamlaka za Mikoa, Wilaya, Baraza la Manispaa, Mabaraza ya Miji na Halmashauri za Wilaya kuratibu zoezi hili kikamilifu. Viongozi wetu Wakuu wa Kitaifa wataungana nasi katika zoezi hili katika maeneo watakayopangiwa.


Ndugu Wananchi,
Kuanzia Jumatatu ya tarehe 4 Janauari, 2016 hadi Jumatatu ya tarehe 11 Januari, 2016 kutafanyika shughuli mbali mbali ikiwemo uwekaji wa mawe ya msingi na ufunguzi wa miradi ya maendeleo pamoja na burudani na michezo. Vyama vya Michezo na viongozi wa maeneo wanashajiishwa kuandaa burudani na kuendesha mashindano ya michezo ili kuamsha hamasa zaidi katika maeneo yao.

Ndugu Wananchi,
Mara tu itakapoingia tarehe 12 Januari, 2016 yaani saa 6.01 za usiku kutapigwa mizinga na Vikosi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania katika maeneo ya pembezoni mwa ufukwe wa Kizingo na viwanja vya Lumumba kwa Unguja na kiwanja cha Gombani na Wesha kwa Pemba.  Mizinga hii itakuwa salama na haitakuwa na madhara yeyote kwa wananchi. Aidha, sambamba na mizinga hiyo meli zilizopo bandarini na gari zilizopo barabaranizitapiga honi kwa angalau dakika mbili (2) kuashiria uingiaji wa siku maalum kwa wananchi wa Zanzibar.

Ndugu Wananchi,
Jumanne ya tarehe 12 Januari, 2016 itakuwa ni siku ya kilele cha maadhimisho haya hapo katika Uwanja wa Amaan. Kama kawaida siku hii wakati wa asubuhi hadi mchana itarindima kwa mambo mbalimbali  ikiwemo gwaride na maonesho ya kijeshi kutoka kwa vikosi vyetu vya ulinzi na usalama, burudani za ngoma za utamaduni pamoja na maandamano ya wananchi wa Mikoa mitano ya Zanzibar.  Sherehe zetu hizi zitahudhuriwa na viongozi mbali mbali mashuhuri  wa kichama na wa kiserikali kutoka Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Wakati wa usiku wa tarehe 12 Januari, 2016 kutakuwa na Taarabu rasmi itakayopigwa na Kikundi chetu Cha Taifa katika Ukumbi wa Salama, Hoteli ya Bwawani  sambamba na  fainali ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi (Mapinduzi Cup) katika Uwanja wa Amaan.

Ndugu Wananchi,
Kwa kumalizia, nachukua nafasi hii kukukumbusheni tena kuwa  mafanikio na maendeleo tuliyonayo hivi sasa hayakuja tu kwa miujiza, bali ni kwa imani na jitihada kubwa za viongozi wetu wanamapinduzi chini ya uongozi wake Jemedari Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume aliyeweka msingi imara wa ushirikiano, umoja, moyo wa uzalendo na wakupendana. Tuna kila sababu na ni haki yetu kusherehekea siku hii adhimu katika maisha yetu. Hivyo, tuambizane, tushajihishane na tushiriki katika matukio mbali mbali ya maadhimisho ya sherehe hizi tangu siku ya uzinduzi wake tarehe 3 Januari hadi siku ya kilele tarehe 12 Januari pale Uwanja wa Amaan.

Ndugu Wananchi,
Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa katika muda wote wa maadhimisho haya kunakuwa na hali ya utulivu na usalama mkubwa katika maeneo yote ya visiwa vyetu vya Unguja na Pemba.

Ni matumaini yangu kwamba sote tutashiriki tena kwa wingi katika maadhimisho hayo.  Nawatakieni maadhimisho mema ya Mapinduzi na heri ya mwaka mpya, wa 2016.


“  MAPINDUZI DAIMA  “

          AHSANTENI SANA.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.