Habari za Punde

Dk Shein: Kasi ya uimarishaji wa miundombinu ya afya uendane na utekelezaji wa majukumu

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                 05 Januari, 2016
---

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema wakati Serikali inatekeleza kwa kasi mpango wake wa kuimarisha miundombinu  ya sekta ya afya watumishi wa sekta hiyo hawana budi kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao ipasavyo na kwa kuzingatia miiko ya taaluma zao.

Akizungumza katika hafla ya kuweka mawe ya msingi ya majengo mawili ya huduma za wazazi na watoto katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja leo, Dk. Shein amesema katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Saba kasi ya uimarishaji wa sekta ya afya imeongezeka na kuifanya Zanzibar kupiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma za afya.

Alifafanua kuwa azma ya kuzipandisha hadhi hospitali za Mnazi Mmoja Zanzibar na Abdalla Mzee Mkoani Pemba pamoja na hospitali za Koteji Unguja na Pemba kuwa za wilaya imetekelezwa kwa kiwango kikubwa na wananchi hawana budi kujivunia mafanikio hayo.
“Tumeongeza huduma mbalimbali katika hospitali ya Mnazi Mmoja kama vile kuanzisha idara ya saratani, magonjwa ya njia ya chakula, kusafisha damu, upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo na nyinginezo” Dk. Shein alizitaja na kuongeza kuwa majengo aliyoyawekea mawe ya msingi ni muendelezo wa hatua hizo.

Dk. Shein alisisitiza kuwa azma ya Serikali ya kuiwezesha hospitali ya Mnazi Mmoja kutoa huduma za upasuaji wa moyo iko pale pale na kuongeza kuwa utekelezaji wake hauko mbali tena.

Alibainisha kuwa kuwa Zanzibar hivi sasa imepata mafanikio makubwa katika kuweka mtandao wa miundombinu ya afya na utoaji wa huduma hizo pamoja na kuwa ziko changamoto kadhaa katika kufikia ubora na malengo yaliyowekwa.


“Ni kweli tunakabiliwa na changamoto nyingi katika utoaji wa huduma za afya lakini changamoto hizo zisiwafanye wenzetu wengine kuyabeza mafanikio haya tuliyoyapata” alisema Dk. Shein na kusisitiza kuwa wazanzibari hawana budi kujivunia mafanikio hayo.

Alibainisha kuwa hatua zilizochukuliwa kuzipandisha hadhi hospitali hizo ni pamoja na kuzipatia vifaa bora na vya kisasa na wataalamu wanaotakiwa japokuwa kumekuwa na upungufu wa majengo ambao serikali imekuwa ukikabiliana nao hatua kwa hatua.

Majengo aliyoweka mawe ya msingi, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar, ni jengo la wazazi na watoto wachanga ambalo litakuwa na wodi ya kinamama, vyumba vya upasuaji, vyumba vya kujifungulia vya kisasa, sehemu ya huduma za dharura na huduma nyingine muhimu za kitabibu.

Jengo jingine ni la watoto wadogo litakalokuwa na wodi ya vitanda 100 kati yake 32 ni kwa watoto wenye magonjwa ya kuambukiza, 54 ya watoto wasiokuwa na magonjwa ya kuambukiza na 10 kwa ajili ya wagonjwa wanaohitaji huduma za kusafisha figo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Uholanzi kupitia shirika la ORIO ambayo kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inagharimia ujenzi wa jengo la Wazazi na Watoto na vifaa vyake kwa gharama ya Euro 9.9 milioni.

Aidha aliishukuru Serikali ya Norway kwa kutoa dola za kimarekani 600,000 na Bwana Trond Mohn raia wa Norway alietoa dola za kimarekani 821,000 kuchangia ujenzi wa jengo la Watoto wagogo ambalo litagharimu jumla ya dola za kimarekani 1,671,378 kati ya hizo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetoa dola 250,000.  

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo alieleza kuwa wizara yake imafarijika na mchango mkubwa wa Mheshimiwa Rais katika kuimarisha sekta ya afya tangu akiwa mtumishi wa sekta hiyo hadi sasa.

Waziri huyo alibainisha kuwa eneo la hospitali ya Mnazi Mmoja hivi sasa limekuwa dogo kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma kwa kuzingatia ongezeko la watu hivyo suluhisho sasa ni kutekeleza mradi wa ujenzi wa hospitali mpya ya Binguni.

Katika maelezo yake kwa mgeni rasmi Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dk. Saleh Mohamed Jidawi alieleza kuwa ujenzi wa Jengo la Wazazi na Watoto Wachanga ni sehemu ya Mradi wa ORIO ambao unajumuisha uimarishaji wa vituo 19 vya huduma za afya ya msingi Unguja Na Pemba.
Aliwashukuru watu mbalimbali waliochangia kwa hali na mali utekelezaji wa miradi hiyo ambao alisema wengine wamekuwa marafiki wa kudumu na wa kweli wa sekta ya afya ya Zanzibar akiwemo Bwana Trond.

Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.