Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Makamu wa Rais Mstaafu wa Tanzania Dr. Moh’d Gharib Bilal wakati akiingia kwenye viwanja vya Msikiti Majumuat Islamiat Temeke Mjini Dar es salaam kumuwakilisha Waziri Mkuu wa SMT Mh. Majaliwa Kassimkwenye Maulidi ya kuzaliwa Mtume Muhammad { SAW }.
Mlezi wa Msikiti Majumuat Islamiat Temeke Rais Mstaafu wa Tanzania Al – Hajj Ali Hassan Mwinyi akitoa salamu kwenye maulidi hayo yaliyohudhuriwa na Umati Mkubwa wa Waumini wa Dini ya Kiislamu.
Baadhi ya Waumini wa Dini ya Kiislamu waliohudhuria Maulidi ya uzawa na Kiongozi wa Dini hiyo Mtukufu wa daraja Nabii Muhammad{ SAW }.
Baadhi ya Waumini wa Dini ya Kiislamu waliohudhuria Maulidi ya uzawa na Kiongozi wa Dini hiyo Mtukufu wa daraja Nabii Muhammad{ SAW }.
Mwenyekiti wa Shia Isnasheer Tanzania Sheikh Azam Dewj akiwasilisha salamu za Waumini wa Dini ya Kiislamu wa madhehebu hayo katika Maulidi hayo ya Msikiti wa Majumuat Islamiat Temeke Mjini Dar es salaam.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa niaba ya Waziri Mkuu Mh. Majaliwa Kassim akizungumza na Waumini wa Dini ya Kiislamu kwenye Maulidi ya uzawa wa Mtume Muhammad { SAW } hapo Temeke.
Balozi Seif akiagana na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Sheikh Alhad Mussa Salum baada ya kumaliza kwa hafla ya Maulidi.Kati kati yao ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar - es – salaam ambae pia ni MNkuu wa Wilaya ya Ilala mh. Raymond Mushi.Picha na – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis OMPR.
Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Majaliwa Kassim Majaliwa alisema maovu mengi yanayotishia usalama wa jamii na Taifa kwa ujumla yatapunguwa iwapo kila Mzazi na Mlezi atatekeleza wajibu wake ipasavyo.
Alisema katika kukabiliana na maovu hayo wazazi hawana budi kujitahidi kuwalea Vijana wao katika misingi bora ya Dini ambayo pamoja na mambo mengine inakataza wizi, ulevi,utumiaji na Dawa za Kulevya pamoja na uzalilishaji wa Kijinsia.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa nasaha hizo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika hafla ya Maulidi ya uzawa wa Mtume Muhammad { SAW } katika Msikiti wa Majumuat Islamiat Temeke mwisho Jijini Dar es salaam.
Alisema salama na utulivu wa familia hadi Taifa utapatikana kama jamii itarejea katika mufundisho ya Dini yaliyosisitiza kwamba kila mmoja katika jamii ni mchunga na kila mchunga ataulizwa jinsi alivyochunga kilicho chini yake.
Mh. Majaliwa alieleza kwamba maovu mengi ndani ya familia yanaonekana kuongezeka mara dufu na kutishia ustawi wake jambo ambalo ni hatari kutokana na mkusanyiko wa ngazi ya Familia unaojenga Taifa kukosa utulivu katika mazingira ya kimaisha.
Aliwaomba Waumini wa Dini ya Kiislamu kuitumia mikusanyiko ya Dini hasa ile ya maulidi inayowakutanisha watu wengi kuhimizana katika kuyaepuka mambo yanayoleta mifarakano na kuhimizana juu ya umuhimu kwa kudumisha amani na upendo miongoni mwao.
“ Sisi sote ni waislamu na waislamu wote ni ndugu kama alivyosema muumba wa viumbe vyote Subuhanahu Wataalah katika aya ya 10 ya surat Hujarat { Waislamu wote ni ndugu na suluhusheni baina yenu } ”. Alisema Mh. Majaliwa.
Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania alisisitiza umuhimu wa Wazazi na walimu wa madrasa kuendeleza jukumu lao la kuwafunza Watoto Sera ya Mtume Muhammad { SAW } ili kutekeleza wajibu wao.
Alisema kusomwa maulidi yanayoambatana na usomaji wa Quran, mawaidha pamoja na Dua katika mikusanyiko ya waumini wa Dini ya Kiislamu inayodumisha Umoja, Upendo pamoja na Mshikamano ni mambo yenye kuleta kheri na Baraka nyingi.
Alifahamisha kwamba mahudhurio ya waumini hao katika hafla ya uzawa wa kiongozi wao wa Umma wa Kiislamu ni ishara na dalili ya wazi juu ya mapenzi yao kwa Mtume Muhammad { SAW }, mapenzi ambayo kila Muumini wa Dini ya Kiislamu anapaswa kuwa nayo.
Alisema Waumini wa Dini ya Kiislamu wanawajibika kumpenda zaidi Mtume wao Muhammad { SAW } zaidi kuliko mapenzi yao kuyaelekeza kwa wazazi wao,watoto wao na kuliko watu wote kwa ujumla.
Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ameipongeza bodi ya wadhamini ya Msikiti wa Majumuiat Isamiat kwa kuandaa hafla hiyo muhimu katika kuwajumuisha pamoja waumini wa Dini ya Kiislamu jambo ambalo huleta faida na neema kubwa.
Akitoa salamu Mlezi wa Msikiti wa Majumuat Islamiat Temeke Mwisho ambae pia ni Daktari wa Heshima Rais Mstaafu na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Al – Hajj Ali Hassan Mwinyi amewapongeza Waislamu wa Tanzania kwa bahati waliyoipata ya kuishi katika ardhi iliyojaa Baraka ya Amani, Utulivu na Mshikamano.
Al – Hajj Mwinyi alisema Tanzania ina wakaazi wa Dini mchanganyiko lakini cha kupendeza zaidi ni kuwaona Wananchi wake wenye pia madhehebu tofauti wanaendelea kuishi katika mazingira ya pamoja ya upendo bila ya kubaguana.
Alisema zipo Nchi kadhaa Duniani zenye kufuata Katiba na misingi ya Dini ya Kiislamu lakini zimekosa utulivu na amani unaopelekea Wananchi wake kushindwa kutekeleza Ibada pamoja na kuendelea kwa harakati zao za kimaisha za kila siku.
Mlezi huyo wa Msikiti Majumuat Islamiat aliitahadharisha Jamii ya Kiislamu kuendelea kuishi kwa amani na waumini wa Dini nyengine ili yale mafunzo waliyoachiwa na Kiongozi wao Mtume Muhammad { SAW } yaiweke Dunia katika hali ya utulivu.
Mapema Mhadhiri wa Chuo Kikuu katika mambo ya ustaarabu Sheikh Ali Mohammed Mbwera alisema uislamu kwa mujibu wa mfumo wake kamwe hauhusiki kabisa na matukio yeyote ya dhulma na husda yanayoonekana kutokea Duniani na kuhusishwa waumini wa Dini hiyo.
Sheikh Mbwera alisema vipo vikundi vya watu vinavyovaa mavazi ya Kiislamu kwa malengo yao na kufanya vitendo viovu yakiwemo mauaji,unyang’anyi, Dawa za kulevya pamoja na udhalilishaji wa kijinsia na baadaye vitendo hivyo kuhusishwa waumini wa Dini hiyo jambo ambalo si sahihi.
Mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu katika Mambo ya ustaarabu alifahamisha kwamba Mtume Muhammad { SAW } aliikuta Dunia na watu wake wakiishi katika maisha ya vurugu na dhulma na ndipo alipowajibika kutumia mawazo, busara na elimu aliyopewa kuyakemea maovu hayo kupitia Kitabu Kitukufu cha Quran Karim.
Alitahadharisha kwamba matukio yanayoibuka ndani ya Jamii za Kiislamu kama mauaji, wizi na dhulma wahusika wa matendo hayo wafahamu kuwa wanabeba mzigo wa dhambi moja kwa moja na wala Dini ya Kiislamu haitakuwa dhamana kwa matendo yao maovu.
Sheikh Mbwera aliwathibitishia Waumini wa Dini ya Kiislamu waliohudhuria hafla ya Maulidi ya Kuzaliwa kwa Mtume Muhammad { SAW } kwamba Dunia itaendelea kuwa ya Utulivu iwapo viumbe iliyovibeba vitaishi kwa Amani, upendo na kuvumiliana.
Alisema yanayotokea katika jamii za kiislamu na kuleta sintofahamu yanatokana na ukosefu wa uvumilivu kati ya wenyewe Waislamu pamoja na waislamu na wale wa Dini nyengine.
No comments:
Post a Comment