Habari za Punde

Kisiwa cha Kokota Chalia na Nyumba za Waalimu.

Na.Zainab Atupae,PEMBA
Kutokuwepo kwa nyumba za walimu katika skuli ya Kokota shehia ya Mtambwe Kusini Wilaya ya Wete Pemba, ni miongoni mwa changamoto kubwa inayowakabili walimu wanaotoka nje ya kisiwa hicho, ambayo huzorotesha maendeleo ya elimu kwa wanafunzi.
Walimu hao hutumia masafa yasioyopungua kilomita 25 kufika katika skuli hiyo, jambo ambalo limekuwa kikwazo kikubwa kwao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mwalimu mkuu wa skuli hiyo, Juma Hamad alisema kuwa, kutokana kutokuwepo kwa nyumba za walimu katika kisiwa hicho, imekuwa ni tatizo kubwa linalo pelekea wanafunzi kukosa masomo yao kwa baadhi ya wakati.

“Kwa kweli hili ni tatizo kubwa, kwani siku nyingi walimu hukosa vipindi vya mwanzo na kupelekea baadhi ya wanafunzi kukosa kusoma”, alisema.
Alisema kuwa, walimu hao hutumia usafiri wa mashua kwenda katika kisiwa hicho, ambapo wakati mwengine huchelewa kutokana na hali ya hewa kuwa mbaya.
Mkuu huyo alieleza kuwa, iwapo zitaweza kujengwa nyumba za walimu kisiwani huko, kutaondosha usumbufu kwa walimu pamoja na wanafunzi kupata elimu kwa wakati.

“Nyumba za walimu ni muhimu sana kisiwani humu, kwani kinyume na hivyo inaweza kuwa ni sababu kubwa kwa wananchi kukosa elimu ambayo ndio ufunguo wa maisha”, alisema mkuu huyo.
Mmoja wa wanafunzi hao Seif Rashid(14)alisema kuwa, kukosekana kwa nyumba za walimu imekuwa ni kikazo kwa kwao, kwani hupelekea kukosa baadhi ya masomo kutokana na muda wanaotumia kuwa ni mdogo.
“Elimu kwetu ni matunda na tunayafurahia kwani wazee wetu hakuna aliweza kuipata, sasa tunataka tuitumie, hivyo tunaiomba serikali ichukue juhudi ya kujenga nyumba za walimu, ili tuweze kusoma kwa wakati”, alisema mwanafunzi huyo
Kwa upande wake, Naibu wa sheha wa shihia hiyo Adam Khamis, alisema hicho ni kilio cha muda mrefu kwa walimu na wanafunzi wa skuli hiyo, ambayo huzorotesha maendeleo yao kwa ujumla.
“Wanafunzi katika kisiwa hichi wanapenda kusoma sana, kwani wazee waliowengi hawakuipata, hivyo naishauru serikali iwajengee walimu nyumba ili kuweza kurahisisha”, alisema Naibu huyo.
Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Salum Kitwana Sururu, amewataka walimu waskuli hiyo,kuendelea kuwa na ustahamilivu kwani Wizara inaendelea  kukamilisha majukumu ya skulinyengine ambazo zimejengwa kwa nguvu za wananchi wenyewe.
Alisema kuwa endepo wakimaliza majukumu hao  hakunabudi  kuwajengea nyumba nyumba moja ya kukaa, huku wakiwataka jumuiya ya community foresty kuwapatia msaada wanyumaba hiyo.
“Wizara inamajukumu mengi sio kama hatuki ila tunaendelea kushulikia majukumu mengine,”alisema huyo.
Aidha Afisa mdhamini huo aliwataka  wanalimu na wanachi wa kisiwa hicho,kujuwa wizara inamajukumu  mengi hivyo hawana budi  kuwa wastahamilivu zaidi.

Kisiwa cha Kokota kina wananchi zaidi ya 450, ambapo kina skuli yenye madarasa manne na walimu watano ambao wanakaa nje ya kisiwa hicho, jambo ambalo ni kikwazo kutokana na baadhi ya siku kuchelewa na kukosa vipindi vya mwanzo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.