Habari za Punde

BLW lafanya uchaguzi wa Mnadhimu na wajumbe watano wa NEC

Na Mwandishi, Wetu Zanzibar.

WAJUMBE wa Kamati ya Wawakilishi wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM ) Zanzibar  jana wamefanya Uchaguzi wa kuwapata  wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Katibu wa Kamati  hiyo.

Jumla ya Wawakilishi 22 watokanao na CCM wamejitokeza kuomba nafasi mbali mbali za uongozi zikiwemo Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Wawakilishi wote wa CCM pamoja na Wajumbe Watano (5) wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

Kati ya hao (22), watatu (3) wanaomba nafasi ya Unadhimu ndani ya Baraza la Wawakilishi  na 19 wanaomba nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kupitia Chombo hicho.

Akitangaza Matokeo hayo Mjumbe wa Kamati  Kuu na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd amemtangaza Mh. Ali Salum Haji kuwa mshindi wa nafasi ya Unadhimu ndani ya Chombo hicho kwa kupata kura 36 na kuwashinda wagombea wenzake wawili Mh.Ali Suleimani Ali (Shihata) 32 na Mh. Abdallah Ali Kombo aliyepata kura 10.

Kwa upande wa nafasi tano za Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) walioshinda ni Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohamed, aliyepata kura 51, Mhe. Issa Haji Ussi Gavu kura 36, Mhe. Mihayo Juma Nungha kura 24, Mh. Riziki Pembe Juma 43 na Mh. Asha Abdallah Mussa kura 33.

Uchaguzi huo umetokana na matakwa ya Ibara 106 (s) ya Katiba ya CCM , Toleo la 2012 inayoelekeza kuwa kila inapofika wakati wa Uchaguzi, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanaotokana na CCM watachagua Katibu wa Kamati za Wawakilishi wote wa Chama hicho (Mnadhimu).


Akifungua  Mkutano huo, Mjumbe wa Kamati Kuu na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd uliofanyika katika Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui Zanzibar amewataka viongozi waliochaguliwa  katika Uchaguzi huo kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa maslahi ya Chama na Taifa kwa ujumla.

Amesema CCM ni Chama imara chenye  viongozi weledi na makini waliokomaa kisiasa na fani mbali mbali za kiuchumi na kijamii hivyo viongozi waliochaguliwa  hawana budi kuwakilisha vyema wananchi.

Mkutano huo ulitanguliwa na Risala ya Wajumbe wa  Baraza la Wazee wa CCM Zanzibar  ambapo ilisisitiza suala la umoja na mshikamano miongoni mwa viongozi na wanachama wa chama hicho.

Akisoma Risala hiyo, Katibu wa Baraza hilo, Bw. Waziri Mbwana  amewapongeza wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kuchaguliwa na wananchi kwa kura nyingi kufuatia Uchaguzi Mkuu wa Marudio uliofanyika Machi 20 mwaka huu.

Risala hiyo, imewataka viongozi hao kufanya ziara za mara kwa mara matawini  kwa lengo la kuibua na kutatua kero  mbali mbali zinazowagusa wapiga kura wao majimboni kwa muda mwafaka.

Aidha, imewataka Wawakilishi hao kuvunja makundi  pale yalipokuwepo na badala yake  waelekeze nguvu katika kuunda kundi moja lenye nguvu litakaloweza kusimamia maslahi ya CCM kwa vitendo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.