Habari za Punde

DK. SHEIN AWAMBIA WANA CCM: UJASIRI WENU NDIO UMELETA USHINDI

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                             29 Mei, 2016
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewashukuru wanachama na wapenzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kufanikisha uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi, 2016 na kukipa ushindi wa kishindo chama hicho.

“Wana CCM mlionesha ujasiri mkubwa katika uchaguzi wa marudio hadi kukipatia chama chenu hatua ambayo ni utekelezaji wa wajibu wetu kikatiba kushinda dola zote mbili na kuongoza serikali zote mbili” Dk. Shein alieleza.

Amesema umoja na mshikamano ndio msingi wa ushindi wa CCM hivyo aliwahimiza wanachama na wapenzi wa chama hicho kuendelea kuimarisha mshikamano wao na upendo miongoni mwao.

Dk. Shein ambaye pia ni Makamo Mwenyekiti wa Chama hicho, aliwaeleza viongozi hao kuwa ushindi wa chama hicho ni uthibitisho wa imani waliyonayo wananchi wa Zanzibar kwa Chama cha Mapinduzi na viongozi wake.

Akizungumza leo kwa nyakati tofauti na viongozi wa chama hicho wa ngazi ya mashina hadi wilaya kwa wilaya za Chake Chake na Mkoani, Dk. Shein alisema huu ni wakati muafaka kwa uongozi wa chama hicho katika ngazi zote kutekeleza majukumu yao inavyopaswa.

“Ni lazima viongozi na watendaji wa chama wafanye kazi kwa bidii ili kufikia malengo na isiwe chama kinakuwa hai wakati wa ziara za viongozi tu” Dk. Shein alisisitiza.

Alibainisha kuwa chama hicho kina viongozi katika kila ngazi hivyo ni wajibu wa viongozi hao kuhakikisha kuwa shughuli za chama zinafanyika ikiwemo ofisi zake kuwa wazi wakati wote kutoa huduma kwa wanachama na wananchi kwa jumla.

Alisisitiza kuwa kumalizika kwa uchaguzi uliopita ni kuanza kwa maandalizi ya uchaguzi ujao wa mwaka 2020 hivyo ni wakati muafaka kwa CCM kujidhatiti na maandalizi hayo ili kupata ushindi wa kishindo.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai aliwapongeza wana CCM wa kisiwani Pemba kwa msimamo wao wa kukienzi na kuthamini chama chao bila ya kujali vituko wanavyofanyiwa na wapinzani kisiwani humo ili kuwakatisha tamaa.      

Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.