Habari za Punde

Balozi Seif afunga Mkutano wa Pili wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiufunga Mkutano wa Pili wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar uliokuwa ukijadili Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/2017 katika Ukumbi wa Baraza hilo uliopo Mbweni nje kidogo ya Kusini mwa Mji wa Zanzibar.
 Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakisikiliza Hotuba ya kufungwa kwa Baraza la Wawakilishi iliyotolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hayupo pichani.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakisikiliza Hotuba ya kufungwa kwa Baraza la Wawakilishi iliyotolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hayupo pichani.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kupanga Miji mengine  Miwili Midogo ya Wete Kisiwani Pemba na ule wa Makunduchi Unguja katika azma yake ya kuhimiza matumizi bora  na ya kudumu  ya ardhi hapa Nchini.

Mipango hiyo itaenda sambamba na kufanya mapitio ya mpango wa maendeleo ya Utalii katika eneo la Pwani ya Mashariki ya Kisiwa cha Unguja  inayoanzia kutoka Chwaka Wilaya ya Kati hadi Nungwi Wilaya ya Kaskazini “A”.

Akifunga  Mkutano wa Pili wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar uliokuwa ukijadili Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/2017 katika Ukumbi wa Baraza hilo uliopo Mbweni nje kidogo ya Kusini mwa Mji wa Zanmzibar, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba migogoro ya ardhi bado imekuwa changamoto kubwa inayoisumbua Serikali kwa muda mrefu sasa.

Balozi Seif  alionya kwamba Wananchi wengi hawataki kuheshimu Sheria ya Ardhi jambo ambalo linaibuwa migogo ya ardhi kila uchao. Hivyo katika kumaliza au kupunguza migogoro hiyo aliiomba Mahkama ya Ardhi kuzishughulikia Kesi za migogoro ya Ardhi haraka iwezekanavyo.


Alieleza kwamba  Serikali kupitia Wizara ya Ardhi itakagua maeneo yote yanayohitajika kutayarishwa mikataba ya uwekezaji na maeneo ya Kilimo { Eka Tatu } pamoja na kufanya utambuzi wa maeneo Elfu 6,000 kwa shehia za Unguja na Pemba Mjini na Vijijini.

Alisema Serikali itafanikisha kazi ya kutayarisha  Hati Miliki 1,350 na vitambulisho vya umiliki wa Ardhi za eka tatu tatu zipatazo 60, kutayarisha mikataba ya ukodishaji Ardhi ipatayo 130 pamoja na kuingiza Taarifa za Ardhi katika mfumo wa Kompyuta.

Akizungumzia tatizo la ajira kwa watoto Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwanasihi wazazi  kuwacha kuwatumikisha  kazi watoto wao  hasa zile hatarishi kwa kisingizio cha kujiongezea kipato cha familia ili kupunguza tatizo hilo lililolikumba Taifa kwa hivi sasa.

Balozi Seif alisema Familia bado zina jukumu kubwa la kuhakikisha watoto wao wanapata haki zao za msingi ikiwemo elimu na malezi bora kwa lengo la kuwajengea mazingira mazuri ya maisha yao ya baadaye.

Alifahamisha kwamba kuwepo kwa ajira za watoto hapa Zanzibar bado ni suala kubwa na Serikali inaendelea na jitihada za kulitafutia dawa ya kulikomesha kabisa  ili kuendana na sera na miongoizo ya Kimataifa juu ya kuondokana na tatizo hilo sugu.

Akigusia uimarishaji wa Sekta ya Elimu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali imo katika hatua za kutayarisha mpangoMkuu wa miaka Mitano 2016  hadi 2020 ambao utakuwa Dira ya Elimu kwa kipindi hicho katika ngazi ya elimu ya maandalizi, msingi, sekondari hadi vyuo.

Alisema kupitia mpango huo changamoto zote za msingi zinazoikabili sekta ya Elimu kama upungufu wa vikalio,madarasa, maabara, maktaba pamoja na miundombinu na vifaa vyengine zitapatiwa ufumbuzi.

Balozi Seif  alifafanua kuwa Serikali Kuu tayari imeshatoa fedha kupitia makusanyo ya Kodi inayotokana na Bandari kwa ajili ya ununuzi wa madawati ili kupunguza tatizo la vikalio katika skuli mbali mbali Nchini.

Alisema mchango huo ulioanza kutolewa  mwaka wa fedha wa 2012/2013 ukiwa na miaka Minne sasa umesaidia  kupatikana kwa shilingi Bilioni 3,452,662,465.00 ambapo umewezesha kununuliwa  kwa madawati 4,285, Viti 3,706 na Meza 3,704 na kusambazwa kwenye skuli mbali Unguja na Pemba.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewaomba Waheshimiwa Wawakilishi kutumia sehemu ndogo ya fedha zao zinazotokana na  mfuko wa Jimbo kusaidia kupunguza matatizo hayo hasa upungufu wa madawati katika skuli zilizomo ndani ya Majimbo yao.

Aidha Balozi Seif aliwapongeza Wajumbe wa Baraza hilo la Tisa la Wawakilishi, Mawaziri pamoja na Manaibu Mawaziri kwa umahiri wao mkubwa  katika kuchangia mijadala na hoja mbali mbali ndani ya Baraza hilo.

Alieleza kuridhika kwake na upeo na uelewa mkubwa wa Waheshimiwa hao kwa jinsi walivyotowa michango yao ya kujenga na kuepuka kubomoa, kushutumiana na kukomoana.

“ Nawapongeza sana kwa uelewa na ukomavu wenu wa kisiasa na jamii kubwa ya Wazanzibari na wengine wanajifunza kwa utendaji wenu vipi kiongozi anapaswa kuwa wakati akijadili masuala yanayowahusu moja kwa moja Wananchi ”. Alisema Balozi Seif.

Hata hivyo alisema katika mijadala hiyo alishuhudia baadhi ya Wawakilishi walijaribu kutetea mambo ya kibinafsi badala ya kutilia mkazo mkubwa yale mambo yanayowagusa wananchi walio wengi yanayopaswa kujadiliwa kabisa kabla ya kuwasilishwa Barazani.

Balozi Seif alifafanua  wazi kwamba haitakuwa vyema kwa Wawakilishi kuzungumza mambo ambayo wakirudi majimboni watasutwa na Wananchi wao kwamba waliyoongea katika Vikao sio masuala  halisi waliyoyapa kipaumbele cha mwanzo.

Aliwaasa Wawakilishi kujitahidi kuwatumikia Wananchi kwa nguvu zao zote  na hasa wale walioshinda katika Majimbo ambayo kipindi kirefu yameshikiliwa na Wawakilishi wa Kambi ya 

Upinzani walioshindwa kuwapelekea maendeleo Wananchi wao.
Alisema Wananchi wa Majimbo hayo walikata tamaa  na baadhi yao walihama katika Majimbo yao na kuhamia Mijini wakati wananchi wengine kutoka Majimbo ya Pemba walikimbilia na kuhamia Unguja.

Akielezea masikitiko yake kutokana na matukio ya uhalifu na hujuma  yaliyofanywa na baadhi ya wafuasi wa vyama vya upinzani dhidi ya Wananchi wasio na hatia yoyote kwa itikadi  tu za Kisiasa, Balozi Seif  alionyesha kukerwa na vitendo hivyo visivyolitakia mema Taifa hili.

Alisema Taifa limeshuhudia matukio mbali mbali ya uhalifu na hujuma yanayopangwa na kutekelezwa wafuasi wa Upinzani ikiwa ni utekelezaji wa maagizo waliyopewa na  Viongozi wao ambao wana nia ya kutaka kuhatarisha amani na utulivu uliopo Nchini.

Balozi Seif alieleza kuwa Matukio hayo sio tu kwamba yanaleta kero na kuathiri wananchi kwa kuhujumiwa mali na mazao  yao bali pia yanasababisha  athari kubwa ya  uchafuzi wa mazingira kutokana na uharibifu mkubwa wa miti ya Mikarafuu na mazao mengine.

Alionya kwamba uchunguzi wa awali uliofanywa na Jeshi la Polisi umebaini wazi kwamba wafuasi wa Chama cha Wananchi  wamekuwa na mpango wa kuendeleza hujuma hizo na ieleweke kuwa wanaofanya hivyo  ni wahujumu wa uchumi na watakaopatikana ni bora kushtakiwa chini ya sheria ya uhujumu uchumi.

Katika jitihada za kuwaendeleza wajasiriamali Nchini Balozi Seif alisema Serikali imeshafungua Kituo cha kulele na kukuza wajasiriamali ambacho tayari kimeshatoa  mafunzo kwa Vijana  mia 815 wa maeneo tofuauti Unguja na Pemba.

Alisema Vijana wengi waliopita katika kituo hicho wameweza kujiajiri kupitia miradi midogo midogo sambamba na kuongeza mapato yao na  Serikali inategemea kuwa Kituo hicho ni msaada mkubwa kwa Vijana wengi katika kusaidia kutatua changamoto za ajira.

Balozi Seif amewashajiisha Vijana wa kike na kiume kujiunga na kukitumia kituo hicho ili kupata taaluma na ujuzi wa uzalishaji na kuendesha miradi yao ya kujitegemea kibiashara kwa faida na tija.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwatakia Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na Wananchi wote siku kuu njema ya Eid –El – Fitri inayotarajiwa kusherehekewa hivi karibuni.

Baraza la Wawakilishi Zanzibar limeahirishwa hadi Jumatano ya Tarehe 19 Oktoba mwaka huu wa 2016 mnamo saa 3.00 za asubuhi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.