HOTUBA YA MAKAMU WA PILI
WA RAIS WA ZANZIBAR, MHESHIMIWA BALOZI SEIF ALI IDDI YA KUFUNGA MKUTANO WA PILI
WA BARAZA LA WAWAKILISHI, ZANZIBAR TAREHE 29 JUNI, 2016
UTANGULIZI:
1.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi
Mungu Mtukufu
kwa kutujaalia uhai na afya njema na kutuwezesha kufanikiwa vizuri kushiriki na
kukamilisha Mkutano huu wa Pili wa Baraza la Tisa la Wawakilishi ulioanza
tarehe 18 Mei, 2016 kwa lengo la kujadili Bajeti ya Serikali yetu ya Mapinduzi
ya Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2016/2017. Kwa uwezo wake Mola Mtukufu, kazi zote zilizopangwa katika ratiba ya mkutano
huu wa pili tumezikamilisha kwa mafanikio mkubwa.
2.
Mheshimiwa
Spika,
shukrani maalum nazitoa kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa kuendelea kuiongoza nchi yetu
katika hali ya amani na utulivu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu amzidishie uwezo,
hekima na busara ili aendelee kuiongoza na kuzidi kuiletea maendeleo nchi yetu
katika kipindi hiki cha pili cha uongozi wake.
3.
Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa, napenda kutoa shukurani
zangu za dhati kwako wewe binafsi, Naibu Spika, Wenyeviti na wasaidizi wako
wote kwa kukusaidia kuliendesha Baraza hili Tukufu kwa umahiri na umakini
mkubwa. Pia, nawashukuru Waheshimiwa Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati mbali mbali
za Kudumu za Baraza hili kwa michango, ushauri na maelekezo yao kwa Serikali
katika utekelezaji wa majukumu yake.
4.
Mheshimiwa
Spika,
nawapongeza Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza hili
la Tisa la Wawakilishi, Mawaziri, na Naibu Mawaziri kwa umahiri wao mkubwa
katika kuchangia mijadala na hoja mbali mbali ndani ya Baraza hili. Aidha,
nawashukuru Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Watendaji wote
wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao ya
kila siku kwa mafanikio makubwa.
5.
Mheshimiwa Spika, nachukua pia fursa hii kuelezea kuridhika kwangu na
upeo na uelewa mkubwa walionao Waheshimiwa Wawakilishi kwa jinsi walivyotoa
michango ya kujenga na sio ya kubomoa, kushutumiana au kukomoana. Nawapongeza
sana kwa uelewa na ukomavu wao kisiasa na jamii kubwa ya Wazanzibari na wengine
wanajifunza kwa utendaji wetu vipi kiongozi anapaswa kuwa hasa anapojadili
masuala ya wananchi. Katika kuchangia
hoja mbali mbali za Serikali, wapo waliochangia kwa hamasa, wapo waliochangia
kwa upole, wapo waliochangia kwa jazba na hata kulia lakini wote hao nia yao ni
kuikosoa na kuishauri Serikali ili ifanye kazi zake kwa usahihi zaidi.
6.
Mheshimiwa Spika, nimeona dalili ya baadhi yetu kutetea mambo ya
kibinafsi kuliko yale ya wananchi walio wengi, hili naomba tuliache,
tuwasilishe katika chombo chetu hichi mambo ambayo wananchi yanawagusa na
ambayo wametutuma tuje kuyatetea, tupite kwa wananchi tujadiliane nao na
mnachokubaliana nao ndicho tukiwasilishe katika Baraza hili Tukufu. Haitokuwa
vyema tukaongea vitu ambavyo tukirudi Majimboni kwetu wananchi wakatueleza kuwa
yale uliyokuwa unaongea Barazani sio shida zetu au sio tuliyoyapa kipaumbele.
7.
Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Wawakilishi
wajitahidi kuwatumikia wananchi wao kwa nguvu zao zote na hasa wale walioshinda
katika Majimbo ambayo kipindi cha nyuma yakishikiliwa na wawakilishi wa Chama
cha Upinzani, ambao wengi wao hawakuwa wanawaletea maendeleo wananchi wao ambao
wengi wao walihama katika Majimbo yao na kukimbilia mijini. Na baadhi yao
kutoka Majimbo ya Pemba walikimbilia na kuhamia Unguja. Wananchi wa Majimbo hayo walikata tamaa na
sasa nakuombeni sana mkae na wananchi hao na kuwarejeshea matumaini na pia
waweze kuona faida ya kuwa na Wawakilishi kutoka CCM.
8.
Mheshimiwa
Spika, naomba
nitoe mwito maalum kwa Waheshimiwa Wawakilishi kutenga muda wa kutosha kuzisoma
hotuba za bajeti na miswada inayowasilishwa na michango yetu ikakita katika
vitabu au nyaraka zilizowasilishwa kwa kufanya rejea ya maeneo hayo na kushauri
nini kifanyike. Baadhi yetu tumeonekana
kusikiliza msemaji aliyepita na kurejea yale yale hata kama hayamo katika
hotuba inayojadiliwa, si vibaya kurejea au kuzungumza jambo ambalo halikutajwa
katika hotuba husika mradi ina nia ya kujenga au kuondoa kero fulani
inayowasumbua wananchi wetu hata wageni wanaotembelea nchi yetu.
9.
Mheshimiwa
Spika, nimelazimika
kutoa ushauri huu baada ya kuona wachache kati yetu wamekuwa wakitoa michango
ambayo iko nje ya suala la msingi linazungumzwa au wanauliza kitu ambacho
majibu yake yamo katika hotuba inayojadiliwa.
Tukisoma kwa makini na kuchangia baada ya kukielewa kilichowasilishwa
tutaongeza ufanisi wa shughuli zetu kuokoa muda ambao tungeweza kuutumia kwa shughuli
nyengine za Baraza letu Tukufu. Aidha,
wananchi wetu wanafuatilia kwa makini sana kinachowasilishwa na michango yetu
na nimekuwa nikipokea maoni ya wananchi kuwa baadhi yetu tunatoka sana nje ya
mada za msingi.
10.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee naomba nimshukuru Mheshimiwa
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali
Mohamed Shein, kwa kuunda Baraza la Mawaziri pamoja na Naibu Mawaziri lenye
watu imara, mahiri, wenye ari ya kufanya kazi na wanaowajibika ipasavyo. Kazi yangu katika Baraza lako Tukufu imekuwa
nyepesi kutokana na utendaji wao mzuri. Napenda kuwapongeza Mawaziri hao na
Manaibu wao kwa kazi nzuri wanayoifanya Barazani na kwenye Wizara zao.
11.
Mheshimiwa Spika, Mawaziri na Naibu Mawaziri wengi wana muda mchache
katika ofisi zao, lakini kwa kipindi kifupi sana wameweza kuzielewa kazi zao na
changamoto zinazowakabili. Kinachonipa faraja zaidi ni kuwa hoja za Waheshimiwa
Wawakilishi zimeweza kujibiwa kwa usahihi na umakini mkubwa sana, nakupongezeni
sana.
12.
Mheshimiwa Spika, naomba pia nipongeze mashirikiano ambayo yapo baina
ya Waheshimiwa Wawakilishi na Mawaziri, hali inayopelekea kila changamoto
inayojitokeza kupatiwa ufumbuzi kwa mashirikiano, huku ndiko kujenga nchi. Hatuwezi
kupiga hatua ikiwa hatuna mshikamano na mashirikiano katika ujenzi wa nchi
yetu. Siasa chafu kama zinazofanywa na wapinzani zinalenga kuipaka rangi ya
ubaya nchi yetu na viongozi wake zimepitwa na wakati na tusiruhusu siasa
uchwara kuenea nchini mwetu.
13.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyokupongeza hapo awali, naomba niendelee
kukupongeza na kutambua usimamizi wako wa chombo hiki kikubwa katika nchi yetu.
Wewe mwenyewe binafsi, Naibu wako na Wenyeviti mmefanya kazi kubwa na ya weledi
mkubwa sana, kuendesha vikao vya Baraza la Wawakilishi kuna changamoto nyingi
ikiwamo kuzielewa Kanuni na Taratibu za Baraza hasa inapotokea mitazamo tofauti
juu ya hoja au suala linalojadiliwa. Ninachoweza kusema ni kuwa chombo kimepata
manahodha wanaokijua, wanaojua tunakoelekea na changamoto za kufikia
tunakokwenda, hongereni sana Mhe. Spika.
TAARIFA
YA MAMBO MBALI MBALI:
(i)
HALI
YA KISIASA:
14.
Mheshimiwa Spika, baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kupitia
Mwenyekiti wake kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015 kufuatia
kubainika kwa kasoro nyingi ambazo zingeyafanya matokeo hayo kutokuwa ya uhuru
na haki, Katibu Mkuu wa Chama cha CUF Maalim Seif Sharif Hamad amekuwa akipita
maeneo mbali mbali kuwadanganya wananchi hasa wanachama wa chama chake na
Jumuiya za Kimataifa kwamba, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alitoa amri kwa Mwenyekiti wa Tume ya
Uchanguzi Zanzibar, Mhe. Jecha Salum Jecha, kufuta matokeo hayo jambo ambalo
sio la kweli, na kauli hiyo ilikuwa kama tusi kwa Dk. Shein, maana amemaanisha
kuwa kama Dk. Kikwete asingemwamuru Mhe. Jecha kufuta uchaguzi, Dk. Shein
angekubali kudhumuliwa. Hii ni porojo
tu.
15.
Mheshimiwa Spika, napenda ieleweke kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
ni chombo huru chenye mamlaka na kinafanya kazi zake bila ya kuingiliwa na mtu
au chombo kingine chochote. Maamuzi ya
kufuta matokeo hayo yalikuwa ni halali baada ya kubainika kwa kasoro nyingi,
ukiukwaji mkubwa wa sheria na kanuni za uchaguzi hasa Kisiwani Pemba. Tume ya
Uchaguzi inafanya kazi zake ili kusimamia haki na kuhakikisha matakwa na ridhaa
za wananchi katika kuwachagua viongozi wanaowataka zinatimia bila ghilba na
udanganyifu wowote.
(ii)
ZIARA ZA MAALIM SEIF
SHARIF HAMAD:
16.
Mheshimiwa Spika, tokea kumalizika kwa uchaguzi wa marejeo
uliofanyika tarehe 20 Machi, 2016 na CCM kupata ushindi wa kishindo, Katibu
Mkuu wa Chama cha CUF, Seif Sharif Hamad pamoja na viongozi wengine wa chama
hicho wamekuwa wakifanya ziara mbali mbali ndani na nje ya nchi. Serikali imezifuatilia
kwa karibu ziara hizo na kubaini kwamba msingi wake ni kutapatapa kwa kiongozi
huyu baada ya kushindwa uchaguzi huo wa marejeo. Ziara hizo zimekuwa ni
muendelezo wa vitendo vya uchochezi na hujuma, kwani anayoyasema wakati wa
ziara hizo yanaongeza chuki na uhasama miongoni mwa wananchi wa Zanzibar. Tunayaona au kuyasikia yanayotokea huko Pemba
hivi sasa.
17.
Mheshimiwa Spika, nawaomba wananchi wasibabaishwe na kauli hizo za
Seif Sharif Hamad kwani haziwezi hata kidogo kuiteteresha Serikali halali
inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi iliyowekwa madarakani na wananchi wa
Zanzibar katika uchaguzi wa marejeo uliofanyika tarehe 20 Machi, 2016. Wala
kauli zao hizo haziwezi kututoa kwenye malengo yetu ya kuwaletea wananchi
maendeleo. Uchaguzi huo aliukataa yeye
mwenyewe na kilichobakia ni kusubiri uchaguzi mwengine hapo mwaka 2020 panapo
majaaliwa. Huko nchi za nje nako
alisikika akidai kuundwa kwa Serikali ya Mpito ya miezi sita itakayoongozwa na
Mzanzibari asiyefungamana na upande wowote wa kisiasa, Zanzibar na baada ya
hapo uitishwe Uchaguzi Mkuu utakaosimamiwa na Jumuiya au Taasisi ya
Kimataifa. Huu ni upuuzi mwingine kwani
jambo hilo haliwezekani kutokea hata siku moja.
Tunachojua sisi ni kuwa uchaguzi umekwisha, uchaguzi mwingine hadi
2020. Kabla ya hapo hakuna Serikali ya
Mpito wala ya Mpeta. Hapa ni Kazi tu ya
kuwatumikia wananchi ya kuzitatua kero zao na kutekeleza ahadi tulizozitoa
kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2015 – 2020.
(iii)
MATUKIO
YA UHALIFU NA HUJUMA:
18.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu imeshuhudia matukio mbali mbali ya
uhalifu na hujuma yanayopangwa na kutekelezwa na baadhi ya wafuasi wa Chama cha
Upinzani cha CUF wasioitakia mema nchi yetu, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya
viongozi wao ambao wana nia ya kuhatarisha hali ya amani na utulivu uliopo.
Matukio hayo yamejitokeza kabla na baada ya uchaguzi wa marejeo uliofanyika
tarehe 20 Machi, 2016, ikiwemo uchomaji moto nyumba, ofisi za CCM na vituo vya
afya; wananchi kunyimwa au kubaguliwa kwenye huduma za kijamii; na kukata na
kuharibu mikarafuu na mazao mengine, ikiwemo mpunga, muhogo, migomba na vipando
vingine.
19.
Mheshimiwa Spika, Serikali inasikitishwa sana na matukio hayo,
ambayo sio tu yanaathiri wananchi walengwa, bali pia yanaleta athari kubwa za
kimazingira kutokana na uharibifu mkubwa wa miti ya mikarafuu na mazao mengine.
Wanaofanya vitendo hivi ni wahujumu uchumi na watakaopatikana ni bora
kushitakiwa chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi.
20.
Mheshimiwa Spika, uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi Zanzibar unaonyesha kwamba Chama
cha CUF kimekuwa na mpango wa kuendeleza hujuma hizo katika maeneo mbali mbali,
ikiwemo nyumba za Viongozi Waandamizi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi. Kwa mujibu wa uchunguzi huo, vitendo hivi
vinatokana na maelekezo ya Chama cha CUF yaliyotolewa na Katibu Mkuu wao, Seif
Sharif Hamad. Aidha, upo ushahidi wa kutosha kwamba Seif Sharif Hamad amekuwa
akitoa hotuba za uchochezi kupitia mikutano yake ya ndani aliyoifanya katika
maeneo mbali mbali, hasa Kisiwani Pemba.
Serikali inakamilisha taratibu za kuwachukulia hatua za kisheria wale
wote waliohusika na vitendo hivyo.
Wasije wakailalamikia Serikali kwa hatua itakazochukua.
Nichukue
fursa hii kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoa pole kwa
wananchi wa Pemba kwa madhila waliyoyapata ya kuharibiwa na kuchomewa nyumba
zao, kukatiwa vipando vyao mbali mbali na kubaguliwa, Serikali iko pamoja
nao. Serikali itawashughulikia wahalifu
hao vipasavyo.
MARADHI YA KIPINDUPINDU:
21.
Mheshimiwa Spika, kama
tunavyofahamu kuwa nchi yetu bado imekabiliwa na maradhi ya kipindupindu katika
maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba. Kuanzia Septemba, 2015 hadi kufikia
katikati ya mwezi wa Juni, 2016, jumla ya wagonjwa 4,242 (Unguja 2,608 na Pemba
1,624) walilazwa katika vituo vilivyotengwa vya Unguja na Pemba, na kati ya
hao, watu 68 wamefariki dunia (Unguja 49 na Pemba 19). Serikali, imeendelea
kuchukua hatua mbali mbali za kukabiliana na maradhi haya zikiwemo utoaji wa
elimu ya kujikinga na maambukizi ya maradhi hayo. Serikali inaendelea kuwasisitiza wananchi
kutokufanya biashara za vyakula vya maji maji katika maeneo yasiyoruhusiwa.
22.
Mheshimiwa Spika, kutokana na
kupungua kwa kasi ya maradhi ya kipindupindu na kwa kuzingatia mahitaji ya huduma
za chakula katika mikahawa, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeamua kuzifanyia
ukaguzi sehemu za kuuzia vyakula na kuruhusu baadhi ya sehemu hizo baada ya
kukidhi vigezo vya afya. Nachukua fursa hii kuzitaka sehemu zilizoruhusiwa
kutoa huduma ya chakula kuendelea kuweka usafi na kuzingatia masharti ya afya
katika sehemu zao na kwa wale ambao sehemu zao hazijaruhusiwa wahakikishe kuwa
sehemu hizo zinakuwa safi ili kukidhi vigezo vya afya.
(iv)
UTOAJI WA PENSHENI KWA WAZEE:
23.
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni, Waziri wa Fedha na Mipango,
Mheshimiwa Dkt. Khalid Salum Mohamed kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein alizindua
Mpango wa Utoaji wa Pensheni kwa Wazee hapa Zanzibar. Chini ya Mpango huo,
Serikali hadi sasa imeorodhesha wazee 21,750 wenye umri wa miaka 70 na
kuendelea na kutoa pensheni kwa wazee hao kwa awamu mbili za malipo. Zaidi ya
Shilingi Milioni 400 zinatumika kulipia pensheni hizo za wazee kwa kila mwezi.
Nachukua fursa hii kukumbusha agizo la Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwamba watendaji wanaohusika na pensheni hizo
wawe makini na waadilifu katika kuwabaini, kuwafikia na kuwahudumia wazee hao.
Vyenginevyo, Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali watendaji watakaoharibu
mpango huo wa Serikali.
(v)
KUWAENDELEZA
WAJASIRIAMALI:
24.
Mheshimiwa Spika, katika jitahada za kuwaendeleza wajasiriamali,
Serikali imekifungua rasmi Kituo cha Kulelea na Kukuza Wajasiriamali kilichopo
Mbweni. Kituo hiki kimeweza kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana 815 wa
Unguja na Pemba, ambao wengi kati yao wameweza kujiajiri kupitia miradi midogo
midogo, na hivyo kujiongezea kipato. Nachukua fursa hii, kuwashajihisha vijana
wa kike na kiume kujiunga na kukitumia kituo hiki ili kupata taaluma na ujuzi
wa uzalishaji na kuendesha biashara kwa faida na tija. Ni mategemo ya Serikali kwamba kituo hiki
kitakuwa ni msaada mkubwa kwa vijana wetu katika kusaidia kutatua tatizo la
ajira.
(vi)
USIMAMIZI WA BEI ZA
BIDHAA MUHIMU:
25.
Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa bidhaa muhimu za chakula, ikiwemo
mchele, sukari na unga wa ngano umekuwa wa kuridhisha hapa nchini. Takwimu
zinaonyesha kwamba hadi kufikia Machi 2016, jumla ya tani 72,535 za mchele,
tani 16,322 za sukari na tani 29,472 za unga wa ngano zimekidhi mahitaji ya
matumizi ya soko la ndani. Mwenendo wa bei za bidhaa hizo uliendelea kuwa ya
utulivu (stable) kutokana na Serikali kuendelea kuchukua hatua za kisera za
kusimamia bei za bidhaa muhimu kwa kushirikiana na wafanya biashara. Nachukua
fursa hii kutoa shukrani kwa wafanya biashara kwa kuzingatia maelekezo ya
kisera na hali za wananchi katika kutoa huduma hizo za bidhaa muhimu.
(vii)
TATIZO LA AJIRA KWA WATOTO:
26.
Mheshimiwa Spika, suala la kuwepo kwa ajira kwa watoto hapa Zanzibar
bado ni kubwa na Serikali inaendelea na jitihada za kulikomesha tatizo hili ili
kuendana na sera na miongozo ya Kimataifa juu ya kuondokana na tatizo hili.
Serikali tayari imezisaidia familia masikini 1,500 katika Wilaya zote 11 za
Unguja na Pemba ambazo imegundulika kwamba watoto wao wanajishughulisha na kazi
mbali mbali za kujipatia kipato. Jumla ya watoto 5,067 kutoka familia hizo
ambao walitoroka skuli tayari wamerejeshwa kuendelea na masomo yao badala ya
kufanya kazi. Aidha, jumla ya familia 1,065 zimepatiwa sare za skuli kwa watoto
wao pamoja na vifaa vya kuanzishia miradi ya kiuchumi vikiwemo mafriji na
mifugo.
27.
Mheshimiwa Spika, kutokana na tatizo hilo la ajira kwa watoto kuwa
kubwa, nawasihi wazazi kuacha kabisa kuwatumikisha watoto katika kazi mbali
mbali na hasa zile hatarishi kwa kisingizio cha kujiongezea kipato cha familia
zao. Bado familia zina jukumu kubwa la kuhakikisha watoto wao wanapata haki zao
za msingi ikiwemo elimu na malezi bora ili kuwajengea mazingira mazuri ya
maisha yao ya baadae.
(viii)
UDHALILISHAJI WA
WANAWAKE, WATOTO NA WATU WENYE ULEMAVU:
28.
Mheshimiwa Spika, suala la udhalilishaji na ukatili kwa wanawake,
watoto na watu wenye ulemavu bado ni tatizo sugu hapa nchini. Kwa upande mmoja,
tatizo hili limekuwa likichangiwa na migogoro ya kifamilia, na kwa upande
mwengine linatokana na ucheleweshaji wa taratibu za kushughulikia tuhuma za
vitendo vya udhalilishaji na ukatili katika vyombo husika. Nachukua nafasi hii kutoa wito kwa wananchi
kujiepusha na migogoro ya kifamilia, na iwapo ikitokea waitatue kupitia vyombo
vinavyohusika. Aidha, navitaka vyombo vyetu vya sheria kuchukua hatua za haraka
katika kushughulikia malalamiko na kesi zinazohusu udhalilishaji na ukatilii
kwa wanawake, watoto na watu wenye ulemavu.
Malalamiko makubwa ya wananchi ni kwamba vyombo vya Sheria havichukui
hatua madhubuti za kushughulikia kesi za udhalilishaji wa kijinsia, na wakati
mwingine hazishughulikiwi kabisa hata kama ushahidi utakuwa wazi kiasi
gani. Naviomba vyombo vya Sheria
vichukue hatua za haraka kuwashughulikia wale wote watakaohusika na kesi za
aina hii. Kushughulikiwa kesi hizi kwa
haraka kutaepusha watu kuchukua sheria mikononi mwao.
(ix)
USHIRIKI WA ZANZIBAR
KATIKA JUMUIYA ZA KIKANDA NA KIMATAIFA:
29.
Mheshimiwa Spika, kwa suala la ushiriki wa
Zanzibar katika Jumuiya za Kikanda na Kimataifa, Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar itahakikisha kuwa inawakilishwa vizuri katika mikutano inayoandaliwa
na Jumuiya za Kikanda na Kimataifa. Mikutano hiyo itawahusisha Maofisa kutoka
katika sekta mbali mbali za Serikali. Madhumuni ya mikutano hii ni kuiwezesha
Zanzibar kunufaika na fursa zinazopatikana kwenye Jumuiya hizo pamoja na
kujenga mahusiano mema na nchi wanachama.
(xi) USHIRIKIANO NA
WAZANZIBARI WANAOISHI NJE YA NCHI:
30.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la ushirikiano wa Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi au
Diaspora, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kuwashirikisha
Wanadiaspora wa Zanzibar kushiriki maendeleo ya nchi yao. Katika kufanikisha
hilo, Serikali itahakikisha kuwa Sera ya Diaspora inamalizika na kuanza
kutumika. Sera hii itaweka miongozo sahihi na mazingira rafiki
yatakayowawezesha WanaDiaspora wa Zanzibar kushiriki kikamilifu katika maendeleo
ya Zanzibar. Aidha, katika mwezi Agosti
2016, Serikali itaandaa kongamano la Watanzania wanaoishi nje ya nchi hapa
Zanzibar.
(xii) SEKTA YA ARDHI:
31.
Mheshimiwa Spika, katika sekta hii, Serikali itafanikisha kazi za kutayarisha Hati Miliki
1,350 na Vitambulisho vya Umiliki Ardhi za Eka Tatu 60, kutayarisha Mikataba ya
ukodishaji ardhi 130, kuingiza taarifa za ardhi katika mfumo wa komputa sawa na
hati za mikataba itakayotayarishwa, kukagua maeneo yote yatakayohitajika
kutayarishiwa Mikataba ya Uekezaji na maeneo ya kilimo (Eka Tatu) pamoja na
kufanya utambuzi wa maeneo 6,000 kwa Shehia za Unguja na Pemba mijini na
vijijini.
32.
Mheshimiwa Spika, vile vile Serikali itaendelea kuhimiza matumizi bora na endelevu ya ardhi
na kuendelea kupanga miji midogo ya Zanzibar kwa kupanga matumizi ya ardhi ya
miji miwili midogo mji wa Wete huko (Pemba) na mji wa Makunduchi hapa (Unguja) sambamba na kufanya
mapitio ya mpango wa maendeleo ya utalii, katika eneo la Pwani ya Mashariki
kutoka Chwaka mpaka Nungwi.
Migogoro ya
ardhi:
33.
Mheshimiwa Spika, bado migogoro ya ardhi imekuwa
changamoto kubwa kwa Serikali yetu. Hii
ni kwa sababu ya wananchi wetu hawataki kuheshimu Sheria ya Ardhi ndiyo maana
kila siku migogoro ya ardhi inaibuka.
Kuimaliza migogoro hii, naiomba Mahakama ya Ardhi kuzishughulikia kesi
za migogoro ya ardhi kwa haraka iwezekanavyo.
(xiii) SEKTA ZA HABARI NA MICHEZO:
34.
Mheshimiwa Spika, katika sekta ya habari,
Serikali imo mbioni kukamilisha ujenzi wa Chuo cha Uandishi wa Habari kilichopo
Kilimani ili kiweze kupokea idadi kubwa ya wanafunzi katika fani ya habari,
ambapo Chuo kitaongeza madarasa matano (5) na kutoa fursa kwa wanafunzi wengi
kujiunga katika chuo hicho. Ujenzi utakapomalizika, Chuo kitakuwa na uwezo wa
kuchukua wanafunzi 304 kwa mwaka, ikilinganishwa na idadi ya sasa ya wanafunzi
204 kwa mwaka. Aidha, kutaanzishwa kozi nyengine mpya za masomo zikiwemo
Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia (International Relations & Diplomacy),
Language & Interpretation, Language Art of Public Speaking, Graphic Design
na Chinese Language & Chinese Culture. Hivyo Chuo kitaweza kukuza na
kuongeza upatikanaji wa habari kwa ufasaha na kukuza ajira kwa wanahabari.
35.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa sekta ya michezo,
nchi yetu imeshuhudia migogoro mbali mbali
hasa katika mpira wa miguu. Migogoro hii
inaathiri sana ukuaji wa michezo kwa namna moja ama nyengine nchini. Serikali
kupitia Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo kwa kushirikiana na
wadau mbali mbali wa michezo inaendelea kuchukua hatua za utatuzi wa migogoro
hiyo ili kuendeleza sekta ya michezo na kuleta tija kwa wananchi na Taifa kwa
ujumla.
36.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekusudia kujenga na kuviendeleza viwanja mbali
mbali vya michezo ili kuwawezesha vijana wetu kupata fursa ya kushiriki na
kukuza vipaji vyao vya michezo. Katika kulitekeleza hili, jumla ya viwanja tisa
vikiwemo Gombani, Mao-Tse-Tung, Tibirinzi, Nungwi na Matumbaku tayari
vimeshapimwa na vinasubiri kuanza kwa ujenzi.
Viwanja hivi vikikamilika kujengwa vitasaidia kuimarisha michezo nchini.
(xiv) SEKTA YA KILIMO:
37.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa sekta za kilimo,
mifugo na uvuvi, Serikali itaweka mkazo zaidi katika kuimarisha uzalishaji na
tija katika kilimo kwa kushajiisha matumizi ya teknolojia za umwagiliaji maji,
kushajiisha ufugaji wa kibiashara wa kuku na ng’ombe wa maziwa, kuimarisha
uwekezaji katika uvuvi wa bahari kuu na katika viwanda vya kusarifu matunda,
samaki na mwani pamoja na kuwaunganisha wakulima, wafugaji na wavuvi na masoko
ya ndani na nje ya nchi.
38.
Mheshimiwa Spika, suala la usimamizi wa
rasilimali zetu ni muhimu sana. Serikali itaendelea kupiga vita uvuvi haramu
kwa kuimarisha mfumo wa doria pamoja na kuandaa utaratibu wa kuwapatia wavuvi
wadogo wadogo zana bora za uvuvi. Aidha, Serikali itaendelea kudhibiti wimbi la
uvamizi wa maeneo yote ya kilimo, misitu na mifugo ambayo katika siku za hivi
karibuni uvamizi huu umeongezeka sana kwa watu kukata miti ovyo na kujenga
katika maeneo yenye rutuba hasa katika mabonde ya mpunga na katika maeneo ya
hifadhi ya misitu na kuchimba mchanga katika mashamba yanayofaa kwa kilimo.
Nachukua fursa hii kuwataka wale wote wanaojishughulisha na vitendo hivyo vya
kuharibu rasilimali zetu, waache mara moja tabia hiyo, vyenginevyo Serikali
itawachukulia hatua za kisheria mara moja. Aidha, Serikali itaendelea na utoaji
wa miche ya mikarafuu bila ya malipo na kuhakikisha kuwa pembejeo muhimu za
kilimo, ikiwemo mbolea, mbegu na madawa ya kuulia magugu yanapatikana kwa
wakati na kwa wingi unaohitajika ili kuweza kuleta mabadiliko ya tija na
uzalishaji kwa kilimo cha mpunga.
(xv) SEKTA YA NYUMBA NA MAKAAZI:
39.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Sekta ya Nyumba
na Makaazi, Serikali kupitia Shirika la Nyumba la Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano
na Usafirishaji itaendelea kuimarisha huduma bora za makaazi kwa wananchi wote
kwa kuendeleza miradi ya kuwapatia wananchi makaazi bora, salama na ya kisasa
na yenye gharama nafuu. Matarajio makubwa ya Serikali ni kutatua tatizo la
makaazi kwa wananchi hapa Zanzibar.
(xvi) UIMARISHAJI WA SEKTA YA ELIMU:
40.
Mheshimiwa Spika, katika
kuimarisha sekta ya elimu nchini Serikali imo katika hatua za kutayarisha
mpango mkuu wa miaka mitano 2016 hadi 2020 ambao utakuwa dira ya elimu kwa
kipindi hicho katika ngazi za maandalizi, msingi, sekondari na vyuo. Kupitia mpango huo changamoto zote za msingi
zinazoikabili sekta ya elimu kama vile, upungufu wa madawati, madarasa, maabara
na maktaba pamoja na miundombinu na vifaa vyengine zinapatiwa ufumbuzi.
41.
Mheshimiwa Spika, suala la mchango wa madawati ya
wanafunzi limezungumzwa sana katika vikao hivi vya Baraza lako Tukufu. Serikali
ilikuwa ikitoa fedha kupitia makusanyo ya Kodi ya Bandari kwa ajili ya
kununulia madawati ili kupunguza tatizo la vikalio katika skuli zetu. Mchango
huu ulianza kutolewa katika mwaka wa fedha wa 2012/2013. Jumla ya TZS
3,452,662,465.00 zilipatikana kupitia kodi hiyo ya bandari katika kipindi cha
miaka minne, na hadi kufikia mwaka 2015/2016, jumla ya Madawati 4,285, Viti
3,706 na Meza 3,704 yalinunuliwa kwa kutumia fedha hizi na kusambazwa katika
skuli za Unguja na Pemba na yanatumika kwa ajili ya wanafunzi na walimu
wetu. Niwaombe Waheshimiwa Wawakilishi
kutumia alau sehemu ndogo ya mifuko yao ya Majimbo kusaidia kupunguza matatizo
hayo, hasa upungufu wa madawati kwenye skuli zilizoko ndani ya Majimbo yao.
MAMBO MUHIMU
YALIOJITOKEZA BARAZANI:
42.
Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu wa pili, Baraza lako Tukufu lilikamilisha mambo makuu
tisa (9) yafuatayo:-
(a)
Kujibu maswali yaliyoulizwa na Waheshimiwa
Wajumbe.
(b)
Limepokea na kujadili Hotuba ya Mpango wa
Maendeleo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa 2016/2017.
(c)
Limepokea na kujadili Hotuba ya Bajeti ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka wa fedha 2016/2017.
(d)
Limepokea na kujadili Ripoti ya Mkaguzi na
Mdhibiti wa Hesabu za Serikali na Mashirika.
(e)
Limepokea na kujadili Mswada wa Sheria ya Fedha
(Finance Bill) na Uchaguzi wa Wabunge watano kuliwakilisha Baraza letu Tukufu.
(f)
Limefanya uchaguzi wa Mwenyekiti wa Baraza na
Uchaguzi wa Wajumbe wa Tume ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi.
(g)
Limepokea, kujadili na kupitisha Hotuba za
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara za SMZ kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
(h)
Limepokea na kujadili Mswada wa Sheria ya
Matumizi.
(i)
Limepokea na kujadili Mswada wa Dharura wa Sheria
ya kuanzisha Hospitali ya Mnazi Mmoja.
43.
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu
jumla ya maswali ya msingi 85 na maswali ya nyongeza 246 yaliulizwa na
Waheshimiwa Wajumbe na kujibiwa na Waheshimiwa Mawaziri wa Sekta husika.
Nawapongeza Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliouliza maswali ya
msingi na ya nyongeza ambayo yalikuwa na lengo la kudadisi utekelezaji na
ufanisi wa shughuli za Serikali. Aidha, nawapongeza na kuwashukuru Waheshimiwa
Mawaziri kwa kutoa majibu sahihi ambayo yamewejengea uelewa Waheshimiwa
Wawakilishi pamoja na wananchi kwa jumla.
Kwa dhati kabisa, napenda kuwapongeza Mawaziri na Naibu Mawaziri wapya
ambao walijibu maswali katika Baraza hili kwa mara ya kwanza na kujibu vizuri
sana kwa umakini na kwa kujiamini.
44.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar,
Serikali imepanga kutumia Mkakati mpya wa maendeleo ambao unakusudia kuendeleza
mageuzi ya kiuchumi na kijamii kwa kuimarisha uchumi endelevu na kuimarisha
ubora wa huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya, mazingira endelevu na misingi
ya utawala bora.
45.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 maeneo yatakayopewa
kipaumbele katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Zanzibar yameainishwa
na kufafanuliwa vyema katika hotuba ya Serikali iliyotolewa na Mheshimiwa
Waziri wa Fedha na Mipango mwanzoni mwa kikao cha kwanza cha Mkutano wa Pili wa
Baraza hili la Tisa. Hata hivyo, kutokana na umuhimu wake mkubwa katika
kuendeleza uchumi wetu na kuimarisha huduma za jamii na utawala bora kwa jumla,
naomba nichukuwe fursa hii kukumbusha tena maeneo hayo ya kipaumbele
tuliyojiwekea kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
i)
Kuendeleza
miundombinu ya msingi ya barabara, bandari, viwanja vya ndege na nishati.
ii)
Kuendeleza
Mpango wa Matokeo kwa Ustawi (R4P).
iii)
Kuimarisha
huduma za kijamii hasa elimu, afya na maji.
iv)
Kuimarisha
kilimo.
v)
Kuimarisha
maendeleo ya Sekta ya Viwanda Vidogo Vidogo na vya kati.
vi)
Kuendeleza Program za Kukuza Ajira kwa Vijana.
vii)
Kuongeza
juhudi ya kutunza mazingira dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kitaifa na kijamii
kwa jumla.
viii)
Kufanya
tafiti katika sekta mbali mbali.
ix)
Kuimarisha
misingi ya utawala bora na sheria.
46.
Mheshimiwa Spika, ni wajibu wa Taasisi zote za Serikali kuhakikisha
kuwa mipango na programu zao zinaendana na utekelezaji wa malengo haya makuu ya
Serikali kwa mwaka 2016/2017. Aidha, mipango ya muda wa kati hadi kufikia mwaka
2020 haina budi kuendana na malengo ya Mkakati mpya wa Maendeleo wa Zanzibar wa
2016 – 2020. Kwa mnasaba huu, Taasisi zote za Serikali ni vyema zikaandaa
utaratibu wa haraka wa kufanya mapitio ya mipango mikakati yao (Strategic
Plans) ili kuoana na mpango mkuu wa Serikali unaochukua nafasi ya MKUZA II
ambao unamalizika muda wake mwishoni mwa mwezi wa Juni, 2016.
47.
Mheshimiwa Spika, mkutano huu pia umepokea na kujadili na kupitisha Hotuba ya Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar ya mwaka wa fedha 2016/2017. Jumla ya fedha TShs: Bilioni 841,477,500
zimepitishwa. Kati ya hizo, TShs: Bilioni 445.6 ni kwa ajili ya kazi za kawaida
na TShs: Bilioni 395.9 kwa matumizi ya kazi za maendeleo. Nawashukuru na
kuwapongeza Waheshimiwa Wawakilishi wote kwa kuipitisha Bajeti hiyo kwa kauli
moja.
48.
Mheshimiwa Spika, ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za
Serikali na Mashirika imewasilishwa Barazani na itajadiliwa na Waheshimiwa
Wajumbe wa Baraza lako Tukufu katika vikao vijavyo vya Baraza.
49.
Mheshimiwa Spika, mkutano huu pia ulijadili na kupitisha Hotuba za Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Wizara zote 13 za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka wa
fedha 2016/2017. Ni matumaini yangu kwamba Waheshimiwa Mawaziri watasimamia kwa
umakini utekelezaji wa malengo yaliyowekwa katika programu na programu ndogo za
Wizara hizo. Aidha, Waheshimiwa Mawaziri wajitahidi
kuzitekeleza ahadi walizozitoa Barazani hapa.
50.
Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu Wajumbe pia walipata fursa
ya kuwachagua Wajumbe watano wa Baraza hili watakaotuwakilisha katika Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Wajumbe hao
waliochaguliwa ni Mheshimiwa Machano Othman Said, Mheshimiwa Wanu Hafidh Ameir,
Mheshimiwa Amina Iddi Mabrouk, Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub na Mheshimiwa
Hussein Ibrahim Makungu. Kwa mara nyengine
tena nawapongeza kwa uchaguzi huo na pia nawaomba watuwakilishe vyema katika
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
51.
Mheshimiwa Spika, katika
mkutano huu wa Baraza lako Tukufu, Waheshimiwa Wajumbe walipata fursa ya
kujadili mambo mbali mbali muhimu kwa Taifa letu. Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na ukusanyaji wa mapato kupitia
Halmashauri na Manispaa; kuimarisha ulinzi katika bandari bubu (zisizo rasmi);
uimarishaji wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC); utatuzi wa migogoro katika
michezo; uvuvi wa bahari kuu; pembejeo za kilimo kwa wakulima; vifaa vya
kukabiliana na maafa; uimarishaji wa makaazi ya Viongozi wa Kitaifa na suala la
wafanyakazi hewa kwa kutaja machache.
52.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Halmashauri za Wilaya na
Mabaraza ya Miji itahakikisha ukusanyaji wa mapato unaongezeka
pamoja na kuziba mianya ya uvujaji wa mapato hayo. Hali hii itaiwezesha
Serikali kutekeleza mipango ya maendeleo iliyowekwa katika Halmashauri hizo na
Taifa kwa ujumla.
53.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la uimarishaji wa ulinzi katika bandari
zisizo rasmi (bandari bubu), Serikali inaendelea na mikakati ya kuzitambua na
kuziwekea utaratibu maalum bandari hizo ili kutoa huduma katika hali ya usalama
na kusaidia kuchangia upatikanaji wa mapato ya Serikali. Aidha, Serikali kwa
kushirikiana na Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo imekuwa ikifanya doria za mara
kwa mara katika maeneo yote ya mwambao wa visiwa vyetu ikiwemo maeneo ya
bandari bubu kwa lengo la kuhakikisha maeneo hayo hayatumiki kuendeshea
biashara haramu na yanabaki salama.
54.
Mheshimiwa Spika, katika hatua za kukabiliana na maafa nchini, Serikali
imeendelea kutekeleza mipango na mikakati mbali mbali inayowezesha kupunguza
athari za maafa iwapo yatatokezea. Miongoni mwa hatua muhimu zilizochukuliwa na
Serikali ni pamoja na kuanzisha Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa badala ya
Idara ili kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuratibu vizuri zaidi masuala ya
kukabiliana na maafa hapa nchini. Aidha,
Serikali kupitia Kamisheni hii imeendelea kutoa elimu ya kukabiliana na maafa
kwa jamii na kuandaa miongozo ya kujiandaa na kukabiliana na maafa katika ngazi
mbali mbali. Serikali itaendelea kuzijengea uwezo wa kitaaluma na kivifaa
Taasisi zote zinazohusika na masuala ya kukabiliana na maafa nchini.
55.
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha makaazi ya Viongozi Wakuu pamoja na
nyumba za Serikali zilizopo katika maeneo mbali mbali kwa Unguja na Pemba,
Serikali inaendelea kuzifanyia matengenezo na kuziwekea vifaa muhimu ili ziweze
kutumika kama zilivyokusudiwa.
56.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la wafanyakazi hewa, Serikali
inaendelea na uhakiki wa watumishi wote wa umma na itahakikisha wale wote
wasiositahiki kuwepo katika orodha ya watumishi wa umma wanatolewa. Aidha,
Serikali itawachukulia hatua kali za kinidhamu na kisheria wale wote
watakaobainika kwa namna moja au nyengine kushiriki katika uhaulifu huo.
HITIMISHO:
57.
Mheshimiwa Spika, kwa mara nyengine tena, naomba kuchukua nafasi hii kukushukuru na
kukupongeza wewe binafsi, Mheshimiwa Naibu Spika na Wenyeviti wa Baraza kwa
kuuendesha Mkutano huu wa Pili wa Baraza hili la Tisa kwa umahiri na umakini
mkubwa. Vile vile, narudia kuwapongeza
na kuwashukuru Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza hili Tukufu kwa michango yao
katika kupitisha bajeti ya Serikali na za Wizara zote katika mazingira ya
ushirikiano yenye lengo la kuleta tija na kuimarisha utendaji na uwajibikaji
Serikalini.
58.
Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana na kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri kwa kutoa ufafanuzi wa
hoja zilizotolewa na kujibu maswali ya Waheshimiwa Wajumbe kwa ufasaha. Pia nawashukuru waandishi wa habari na
wakalimani wa lugha ya alama kwa kazi yao nzuri ya kuwapatia taarifa wananchi
kuhusu majadiliano ya Baraza katika mkutano huu. Shukrani maalum nazitoa kwa
Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kwa kutangaza na kuonesha moja kwa moja
(live) shughuli zote za mkutano huu bila kusita.
59.
Mheshimiwa Spika, mwisho napenda kuvipongeza vyombo
vyote vya ulinzi na usalama pamoja na Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kwa mchango wao mkubwa katika kudumisha usalama na utulivu uliopo hapa
nchini.
60.
Mheshimiwa
Spika, zipo
kauli zinazosambazwa kupitia mitandao ya kijamii kuwa Serikali itachinja
ng’ombe waliowakamata na kuuza nyama kwa bei rahisi ya Shs. 3,000 kwa kilo na
kutolewa tahadhari kuwa watu wasinunue nyama hiyo eti siyo halali na ni nyama
ya kifo. Napenda kuweka bayana kuwa
kauli hizo hazina ukweli wowote. Hakuna
ng’ombe yoyote atakayechinjwa na Serikali na kuuzwa Maisara kwa bei
rahisi. Huu ni uongo na uzushi
mtupu. Vile vile kuna kauli nyeingine ya
kuwazuia watoto wasiende kufurahi Mnazi Mmoja wakati wa Sikukuu eti kutatokea
fujo na vurugu. Huu ni uongo mkubwa na
uzushi usio na kifani. Serikali
inawahakikishia wananchi kuwa hali ya nchi yetu iko salama na utulivu na
itabaki hivyo siku zote. Kauli hizo ni
propaganda za wapinzani kutaka kuwahamanisha wananchi wapenda amani. Wananchi wanahakikishiwa kuwa viwanja vyote
vya sikukuu vitakuwa salama.
61.
Mheshimiwa Spika, tukiwa tumo katika kumi la mwisho la Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani,
tunamuomba Mwenyezi Mungu atukubalie swaumu zetu na atujaaliye kumaliza faradhi
hii kwa salama. Kwa vile hatutokaa tena
katika kikao kama hiki kabla ya kumalizika mwezi Mtukufu wa Ramadhan, nachukua
fursa hii kuwatakia Waheshimiwa Wawakilishi pamoja na wananchi wote sikukuu
njema ya Eid-el-Fitri inayotarajiwa hivi karibuni INSHAALLAH. Kuluam wa Antum Bukheir.
62.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo
hayo, sasa naomba kutoa hoja ya kuliakhirisha Baraza lako Tukufu hadi
siku ya Jumatano, tarehe 21 Septemba, 2016 saa 3.00 barabara za asubuhi panapo
majaaliwa.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment